Home Habari za michezo ILE ISHU YA VIGOGO WA FIFA NA CAF KUTUA SIMBA KUMBE MCHEZO...

ILE ISHU YA VIGOGO WA FIFA NA CAF KUTUA SIMBA KUMBE MCHEZO MZIMA UKO HIVI AISEE..

FIFA na Kutua Simba

Wakati Klabu ya Simba jana ikihitimisha Mkutano Mkuu wake wa mwaka kwa amani na usalama na kisha kuchagua viongozi wao wapya watakaoiongoza kwa kipindi kingine cha miaka minne, imetangaza rasmi kuwa ni moja kati ya klabu zitakazoshiriki michuano ya Africa Super League ambayo inatarajiwa kuanza Agost

Klabu ya Simba jana ilifanya mkutano mkuu wa kawaida wa mwaka uliofuatiwa na uchaguzi mkuu ambapo walichagua mwenyekiti wa wanachama pamoja na wajumbe watano wa bodi ya wakurugenzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema kwa sasa kila mchezaji mkubwa Afrika anataka kuja kuichezea klabu hiyo huku akiwahakikishia Simba kuwa furaha waliyoipoteza sasa itarudi na hawatakuwa wanyonge tena.

“Simba hii ni ya kimataifa, nimepokea mwaliko mwingine wa kwenda kwenye Semina ya Fifa kule Morocco, hii ni kwa ajili ya Simba, katika watu watatu kwa Afrika mimi ni mmoja wao kwenda kuwakilisha.

Alisema kwa sasa Simba ni namba 10 kwa ubora Afrika kwa ngazi ya klabu na kwamba wamejipanga kutetea ubingwa wao wa ligi licha ya kwamba ni ngumu kutokana na ushindani ulioko, lakini wao kama viongozi wamejipanga.

“Hivi karibuni tutapokea ujumbe kutoka FIFA na CAF kuja kukagua kama mnavyojua Simba ndio timu pekee kutoka Ukanda wa CECAFA ambayo itashiriki Africa Super League,” alisema.

Aidha, Try Again aliwashukuru wanachama na mashabiki wao kutokana na klabu hiyo kupitia kipindi kigumu, lakini wameendelea kuwa nao wakati wote.

Kuhusu mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, alisema licha ya kuzidiwa pointi sita na anayeongoza msimamo (Yanga), bado hawajatoka katika kinyang’anyiro hicho na wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanafanikiwa kufikia malengo yao.

“Mwaka huu tutachukuwa ubingwa kwa uwezo wa Mungu tutafanikiwa katika malengo yetu, kikubwa wanachama na mashabiki wa Simba ni kuendelea kuwaamini viongozi na kuwapa ushirikiano mkubwa.

Alisema hawana budi kumshukuru Mwekezaji Mkuu wa klabu hiyo, Mohamed ‘Mo’ Dewji kwa upendo wake, kwa kutumia pesa zake, muda wake na nguvu zake kuhakikisha wanayafikia mafanikio haya, hivyo wanapaswa kuendelea kumtia moyo kwa kufanya kazi kubwa.

“Sina budi pia kumshukuru Mtendaji Mkuu aliyepita, Barbara Gonzalez, amefanya kazi kubwa, nachukua nafasi hii kumshukuru namwombea dua katika changamoto yake mpya,” alisema Try Again.

WAVUNJA REKODI

Uchaguzi huo wa Simba jana ulivunja rekodi ya wanachama kuhudhuria baada ya ukumbi kufurika kupita kiasi hali iliyosababisha wengine kukosa sehemu ya kukaa na kulazimika kukaa chini sakafuni.

Kwa ujumla uchanguzi ulienda kwa utulivu huku mwitikio wa wanachama kuwa ni mkubwa tofauti na uchangu uliopita.

Zoezi la kuhakiki wanachama lilikuwa gumu kutokana na msururu mrefu ulioanza kuingia ukumbini kuanzia asubuhi na kumaliza saa 8: 17 mchana ambapo ulinzi uliimarika.

Mgeni rasmi arusha dongo

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo mkuu, yeye amewataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutosikiliza maneno ya watu wa pembeni na badala yake kuimarisha kaulimbiu yao ya “Simba Nguvu Moja”.

Alisema Simba imetoka katika hali ngumu kabla ya sasa kuwapo kwa uhakika wa timu kuingia kambini, kusafiri sehemu mbalimbali, na hiyo yote ni kutokana na kuwapo kwa Mwekezaji, Mo Dewji na wadhamini wengine ndani ya klabu hiyo.

“Tusirudi nyuma kwa maneno ya watu ambao hawaitakii mema Simba, kuna mtu katika haya makundi yetu ya mitandao ya kijamii anauliza Sh. bilioni 20 za Mo Dewji ilihali hakuwahi kuchangia hata 5,000 wala kupeleka maji kambini au mazoezini, huyo sio mtu mwema,” alisema Makala.

Alisema baada ya uchaguzi huo kupita Wanasimba wote wanatakiwa kusimama pamoja na kuendelea pale walipoishia na kusonga mbele kucheza nusu fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bajeti ya Mabilioni

Ofisa Fedha Mkuu wa Simba, Suleiman Kahumbu, aliweka wazi bajeti yao ya mwaka 2022-2023 kuwa ni Sh. bilioni 13.7 na matumizi yake ya ni bilioni 13.5, ambazo zitatumika kwa kulipa mishahara, fedha za usajili, posho za wachezaji na wafanyakazi na masuala muhimu ya klabu hiyo.

Kahumbu alisema bajeti ya mwaka 2022-2023, vyanzo vyake vya mapato ni fedha za wadhamini Sh. bilioni 3.97 wakiwamo M-Bet na Vunjabei, Emirats, wadhamini wa Ligi Kuu NBC Bank. Haki za matangazo ya Azam TV Sh. bilioni 2.85 na haki ya matangazo Ligi ya Wanawake Sh. milioni 410.

“Mapato ya viingilio vya mlangoni Sh. milioni 961, kodi ya jengo la Msimbazi bilioni 1.1 na ada za wanachama Sh. milioni 17 huku Mo Dewji akiahidi Sh. bilioni 3.95 kwenye bajeti ya mwaka huu.

Alisema matumizi kwa upande wa usajili ni Sh. bilioni 2.45, mishahara ya wachezaji na wafanyakazi bilioni 4.8, bonasi milioni 840 kwa timu zote tatu, leseni na vibali vya makocha na wachezaji wa kigeni kuishi nchini Sh. milioni 189, kodi ya pango ofisi na hosteli Sh. milioni 578, hoteli ndani na nje ya nchi Sh. milioni 403, usafiri wa nje ya nchi Sh. milioni 102.

Aidha, alisema bajeti ya Simba kwa msimu wa 2021/22 ilikuwa ni Sh. bilioni 11.94 huku makusanyo yakiwa Sh. bilioni 12.73.

MANZOKI: NAKUJA SIMBA

Wakati huo huo katika mkutano huo ambao Mshambuliaji wa Klabu ya Dalian Professional, inayoshiriki Ligi Kuu nchini China, Cesar Lori Manzoki, amefunguka juu ya usajili wake na kuweka wazi kuwa siku moja atacheza na kuvaa jezi ya klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi.

Manzoki yuko nchini tangu juzi na jana alialikwa katika Mkutano Mkuu wa Simba ambao ulifanyika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Nyota huyo alisema yuko nchini kwa ajili ya kupata baraka za Wanasimba kwa kipindi hiki ambacho yuko katika klabu yake ya hiyo ya China, ila yeye ni Simba na ndoto yake kwa Afrika ni kuichezea Simba.

Alisema kutojiunga na Simba kwa msimu huu ni roho mbaya za baadhi ya watu ambao wamemkwamisha kucheza ndani ya kikosi cha Simba katika michuano mbalimbali.

“Nawashukuru Wanasimba wote kwa sababu wananipenda na mimi nawapenda, niwahakikishie kuwa mimi ni mtoto wao na kwa hapa Afrika timu ya kucheza si nyingine bali ni Simba pekee na muda wowote nitakuja kucheza ndani ya klabu hii.

“Kuna maneno mengi yalikuwapo hapa nchini na watu walijua nitacheza timu nyingine, ukweli wa nafsi yangu kama nilivyosema awali kuwa siwezi kuchezea timu yenye rangi ya kinyoka nyoka,” alisema Manzoki.

IBENGE AIMWAGIA SIFA

Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge, ambaye anatarajia kuiongoza timu yake Jumapili wiki hii dhidi ya Simba kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, alisema anajivunia kuwapo kwa ushirikiano kwa Klabu ya Simba na Al Hilal.

Alisema Simba inakuwa timu pekee Ukanda wa CECAFA kucheza kwa mara ya kwanza Africa Super League, inayotarajiwa kuanza Agosti mwaka huu.

“Hii inaonyesha ubora wa Simba kwa sababu ya kufanya kwao vizuri katika michuano ya kimataifa, niwatakie kheri katika ushiriki wao wa michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Ibenge.

MTENDAJI MKUU

Mtendaji Mkuu mpya wa Simba (CEO), Imani Kajula, aliweka wazi mipango yake kuwa kazi kubwa ni kuunganisha Wanasimba na kufanya maendeleo makubwa ikiwamo kuifanya Simba kuendelea kuwa kubwa.

“Kuna mambo mengi nitahakikisha Simba inafanikiwa ikiwamo suala la kuwapo kwa hosteli za kisasa zitakazokuwa mali ya klabu, kuzifanya timu zetu zote tishio ndani na nje ya Bara la Afrika ikiwamo Simba Queens kama msimu uliopita iliishia nafasi ya nne basi msimu huu ichukue ubingwa,” alisema Kajula.

By Saada Akida

SOMA NA HII  SAKATA LA KUSIMAMISHWA MENEJA UWANJA WA MKAPA....MASHABIKI SIMBA NA YANGA WATAJWA KUWA SABABU...