Home Habari za michezo HIVI NDIVYO BOCCO ANAVYOWACHANGA SIMBA NA UZEE WAKE WA ‘MCHONGO’….

HIVI NDIVYO BOCCO ANAVYOWACHANGA SIMBA NA UZEE WAKE WA ‘MCHONGO’….

Habari za Simba

Jina? John Bocco. Umri? Miaka 33. Mahala pakuzaliwa? Dar es salaam. ndivyo mtandao wa Wikipedia unavyoeleza pindi linapokuja suala la wasifu wa John Bocco. Katika soka letu huwa tunaamini kwamba John Bocco ni mzee.

Nasikia hata mwenyewe anaamini hivyo. Vyanzo ambavyo sina uhakika navyo viliniambia kwamba Bocco anasomea ukocha na kwamba mwanzoni mwa msimu huu aliwaambia watu wa Simba watafute mshambuliaji mwingine wa uhakika kwa sababu yeye anajihisi kupitwa na wakati.

Sina uhakika na habari hii lakini nusura iwe ya kweli kwa namna ambavyo Bocco aliuanza msimu. Aliuanza kwa kusuasua huku akionekana kuwa chaguo la tatu au la nne katika orodha ya washambuliaji wa Simba.

Lakini ghafla John Bocco ana mabao tisa katika msimamo wa wafungaji bora wa msimu huu. Juu yake anasimama mshambuliaji mwenzake wa Simba, Moses Phiri. Juu yao anasimama mshambuliaji wa Yanga, Fiston Kalala Mayele.

Nyuma ya Bocco kuna washambuliaji wa Kitanzania. Ukitazama msimamo wa wafungaji mpaka sasa inaonekana Bocco ana ushindani na mshambuliaji mwenzake wa Simba, Phiri ambaye ni mshambuliaji nambari moja klabuni hapo.

Lakini hapo hapo msimamo haumuweki mbali na kinara wa mabao, Mayele ambaye ana mabao 14. Hii ina maana kuna tofauti ya mabao matano tu kati ya Bocco na Mayele. Sio mabao mengi. Tatizo kwa Bocco ni kwamba Mayele naye hawezi kubaki hapo hapo kiurahisi na siku hizi amekuwa akifunga mabao mengi ndani ya mechi moja tofauti na msimu uliopita.

Bocco ameanza kutuchanganya. Tulishaanza kupiga hesabu zetu kwamba Bocco amekwisha lakini kuna mambo kadhaa ametukumbusha msimu huu. Hata watu wenyewe wa Simba si ajabu wakawa wamechanganywa zaidi na Bocco kwa sababu mbalimbali.

Kwanza kabisa kuna pengo kubwa kati ya Bocco na washambuliaji wetu wa ndani wazawa. Hawa ni wale wanaopatikana katika klabu yake na pia wanaopatikana katika klabu nyingine. Mabao ambayo Bocco amefunga msimu huu ilitegemewa yafungwe na mshambuliaji kama Habib Kyombo.

Hata hivyo Bocco ametukumbusha pengo lililopo kati yake na akina Habib Kyombo, Anwar Jabir, Crispian Ngushi, Ayoub Lyanga,Reliant Lusajo, Sixtus Sabilo na wengineo wengi. Bado kuna pengo. George Mpole alijaribu msimu uliopita lakini pengo kati ya Bocco na wengineo bado lipo na ni kubwa.

Nimewahi kuongea na mabosi wa Simba, Yanga na Azam wakaniambia bado kuna ugumu mkubwa wa kupata vipaji vya ndani. Naamini leo hata watu wa Simba hawatajiamini sana na maamuzi yao ya kuachana na Bocco. Watahisi tu kwamba ataweza kwenda Yanga au Azam na bado akawasumbua.

Namna sahihi ya kumfuta mtu kama Bocco katika ramani ya soka ni kwa vijana kuonyesha uwezo mkubwa kuliko yeye. Bado tuna tatizo la vijana kuwafuta katika ramani wakongwe. Haikushangaza Juma Kaseja alikaa langoni kwa miaka mingi kuliko ilivyotakiwa.

Sijui msimu utakwendaje lakini kama Bocco akifikisha mabao 15 tu msimu huu itakuwa ni alama kwamba anastahili kucheza katika kikosi cha Taifa Stars na anastahili kuwa nyuma ya Mbwana Samatta na Simon Msuva katika suala la kuanza.

Lakini kama Bocco akifikisha mabao 15 tu msimu huu itakuwa alama kwamba anastahili mkataba mpya ndani ya klabu yake na anastahili kuwa msaidizi wa Phiri ingawa mpaka sasa bado anatuacha katika alama ya kujiuliza kama yeye na Phiri ndani atakuwa mfungaji bora ndani ya klabu.

Lakini hapo hapo anatuacha katika alama ya kuuliza kuhusu uwezo wa safu za ulinzi za klabu mbalimbali za Ligi Kuu. Huwa napinga suala la uzee katika soka letu kwa namba ambavyo hawa wachezaji tunaoita wazee wanavyoendelea kutamba kila siku.

Clatous Chotta Chama ana miaka 31 na bado anaonekana kuwa mchezaji mwenye madhara zaidi katika eneo la mwisho kuliko mchezaji mwingine yeyote katika Ligi yetu. Hapo hapo kumbuka kwamba Lucas Kikoti wa Namungo aliyekuwa anakuja kasi kwa sasa hakuna kikubwa anachoonyesha uwanjani na hana nafasi ya kudumu katika klabu yake.

Abdulaziz Makame ni mdogo kwa Khalid Aucho lakini unaweza kuona wazi kwamba Aucho ni bora zaidi kuliko yeye. Vipi kuhusu Saidoo Ntibanzokiza. Imekuaje amerudi katika timu kubwa.

Amekwenda kuonyesha uwezo wake Geita dhidi ya vijana wa pale, akajihakikishia namba, akaonyesha uwezo mkubwa dhidi ya vijana wa timu nyingine, leo amerudi timu kubwa. Hakukuwa na suala la umri.

Leo inawezekana Bocco akawa na misimu mingine mitatu au minne ndani ya Ligi Kuu akaondoka akiwa na umri wa miaka 37. Tazama washambuliaji wa kizawa ambao wameshindwa kumng’oa kwa umuhimu ndani ya kikosi cha Simba.

Kitu ambacho nimegundua kwamba tatizo kubwa mashabiki wetu wakati mwingine huwa wanawaharakisha wachezaji wetu kuvunjika moyo na kujiona wazee. Huwa wanapenda kuwaaambia hivyo badala ya kujadili namba zao uwanjani. Mara nyingi huwa wanajadili zaidi umri wao kuliko mchango wao.

Wachezaji wanaokumbana na hadha hii zaidi ni wale wachezaji wa timu kubwa ambao wana mashabiki wanaowapa presha zaidi. kwa timu ndogo kuna wachezaji wanaocheza kwa muda mrefu na hakuna presha kwao. Mfano mzuri ni staa wa zamani wa Kagera Sugar, George Kavilla ambaye alicheza kwa kiwango cha juu mpaka alipokaribia miaka 40. Kama angekuwa anacheza Simba au Yanga asingeweza kufikisha umri huo kutokana na presha ambayo angepewa.

Ndani ya presha hii hii, Bocco nadhani ameanza kuwafikirisha upya wale wote ambao wanaamini kwamba amekwisha. Ni kweli kwamba uwezo wake umepungua lakini vipi akiibuka kuwa mfungaji bora wa Simba au wa Ligi? Tutamfukuza tu kwa sababu ya umri wake au namba zake?

SOMA NA HII  CHAMA NA SIMBA SASA MAMBO NI BAMBAM....BENCHIKHA MENO YOTE NNJE....