Home Habari za michezo KIBADENI ASHINDWA KUJIZUIA KOCHA MZUNGU KUPEWA SIMBA SC..AMTAJA MGUNDA…

KIBADENI ASHINDWA KUJIZUIA KOCHA MZUNGU KUPEWA SIMBA SC..AMTAJA MGUNDA…

Kocha Mkuu Simba SC

Kocha mkuu mpya wa Simba SC, Robertinho Oliviera, atakutana na rekodi ya heshima ya mzawa Juma Mgunda ambayo atatakiwa kuiendeleza, kuhakikisha timu inamaliza kwa kishindo mechi 11 zilizosalia za Ligi Kuu Bara.

Rekodi hii, inaweza kumfanya Oliviera afanye kazi kwa presha zaidi, kwa kuwa anaingia wakati ambao timu inafanya vizuri kwelikweli tofauti na makocha wengine wanavyoingiaga kwenye timu.

Katika mechi 16 za Ligi Kuu ambazo Mgunda ameifundisha Simba SC, ameshinda 11, sare nne na alifungwa mchezo mmoja tu dhidi ya Azam FC, jumla ya pointi alizokusanya ni 34, huku tisa zikiwa za Zoran Maki na moja ya Seleman Matola, dhidi ya KMC zikitoka kwa sare ya mabao 2-2, hivyo timu hiyo ina jumla ya pointi 44.

Nje na mechi za Ligi Kuu Bara za Ligi ya Mabingwa Afrika alizozisimamia ameshinda zote na moja ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Rekodi hizi zimekuwa zikiwagawa mashabiki huku wengine wakiamini Simba SC inahitaji kocha mpya na wengine wakiona kuwa Mgunda anatosha kuipa mafanikio msimu huu.

Simba SC imemalizana na Oliviera raia wa Brazil ambaye alikuwa anaitumikia Vipers ya nchini Uganda, akiwa anatajwa kuwa kati ya makocha wenye uwezo wa juu wa kufundisha soka la kuvutia.

Kutokana na rekodi hiyo, wataalamu wa soka wametoa mtazamo wao na kuutaka uongozi wa Simba SC kuthamini mchango wa Mgunda ndani ya timu hiyo.

Kocha wa zamani wa timu hiyo, Abdallah Kibadeni, alisema Mgunda aliichukua Simba na kuwakuta wachezaji wana morali ya chini, alifanikiwa kuwarejesha mchezoni na sasa wana ushindani mkali dhidi ya wapinzani wao.

“Wakati msimu unaanza mashabiki walionekana kuikatia tamaa timu yao, walianza kucheza wakiwa wazito, lakini kwa sasa wapo vizuri hiyo ni kazi ya Mgunda akisaidiana na Seleman Matola, ninachoshauri uongozi wa Simba usiwatupe mbali makocha hao ndiyo watampa muongozo mgeni,” alisema.

Hoja yake ilikwenda sambamba na straika wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma aliyesema alichokifanya Mgunda na Matola kipewe heshima na wasitupwe mbali, badala yake wamsaidie kocha mgeni kwa ukaribu.

“Chini ya Zoran, Clatous Chama alionekana hana kitu ila kwa sasa ndiye anaongoza kwa asisti, ukiondoka hilo Moses Phiri alionekana butu ndiye kinara wa mabao 10 kwenye timu yao, hiyo ni kazi ya makocha Mgunda na Matola kuvipa thamani vipaji vya wachezaji,”alisema.

SOMA NA HII  PAMOJA NA USHINDI WA JUZI....MAKI KATAZAMA MASTAA WAKE WEEH....KISHA AKATIKISA KICHWA KUKATAA UWEZO WAO...