Home Habari za michezo SAKATA LA CHAMA NA MBRAZILI…SIMBA WAIBUKA NA HOJA MPYA…KUMBE ISHU NZIMA IKO...

SAKATA LA CHAMA NA MBRAZILI…SIMBA WAIBUKA NA HOJA MPYA…KUMBE ISHU NZIMA IKO HIVI…

Habari za Simba

Benchi la ufundi la Simba limesema kiungo wa timu hiyo Clatous Chama ni mgonjwa ndiyo sababu alitolewa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City na kukosekana katika safari ya Dodoma.

Simba itacheza kesho saa 1 usiku dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu unaotarajiwa kupigwa katika Uwanja wa Jamhuri .

Mjadala mkubwa kwa mashabiki wa soka ni namna kocha mpya wa Simba, Oliveira Roberto ‘Robertinho’ alivyomfanyia mabadiliko ya mapema staa huyo dakika ya 33 katika mchezo dhidi ya Mbeya City na kuzua taharuki kwa mashabiki na wadau wa soka nchini.

Kitendo cha kumtoa Chama kilionekana kumshtua kila mmoja na kuzua mshangao mkubwa kwa mashabiki kwa kuwa yeye ndiye staa wa timu hiyo, kwani msimu huu ana asisti 12 na mabao matatu katika michezo 16.

Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda akizungumza jijini hapa, amesema mchezaji huyo ni mgonjwa na tangu wametoka naye Dubai alikuwa hajisikii vizuri na amegundulika ana malaria pamoja na mafua.

“Niwaambie na niliweke wazi hili na ndiyo maana Chama hatukuja naye, Chama anaumwa, tangu ametoka safari alikuwa na hajisikii vizuri baada ya kugundulika ana mafua na malaria.

Mgunda amesema wao ndiyo walimwambia acheze katika mchezo dhidi ya Mbeya City akiwa mgonjwa lakini baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ilibidi wamtoe akapumzike.

“Lazima tutambue kuna haki ya mtu, pia ni lazima kuheshimu maamuzi yake kama binadamu hakuja huku Dodoma kwa sababu ni mgonjwa,”amesema Mgunda.

Hata hivyo, Mgunda alisema hakuna kocha duniani ambaye anaweza kumweka benchi mchezaji mwenye kiwango kikubwa kwa kuwa anataka timu yake ipate ushindi.

SOMA NA HII  SENZO AUKATAA UBINGWA KWA YANGA....AWANYOOSHEA KIDOLE WACHEZAJI..NABI AKOLEZA 'PILIPILI'