Home Habari za michezo UCHAGUZI MKUU SIMBA: KIGINGI CHA MANGUNGU HIKI HAPA…MATAJARI WAJIPANGA KUMTIKISA MO DEWJI…

UCHAGUZI MKUU SIMBA: KIGINGI CHA MANGUNGU HIKI HAPA…MATAJARI WAJIPANGA KUMTIKISA MO DEWJI…

Uchaguzi Mkuu Simba

ZIMESALIA saa chache  leo kufanyika kwa Uchaguzi wa uongozi wa juu wa klabu hiyo, huku jana Jumamosi Januari 28 ikiwa ni siku ya mwisho ya kampeni kwa wagiombea wote wa nafasi za Ujumbe na uenyekiti.

Itakumbukwa huu unakuwa ni uchaguzi wa pili kwa Simba tangu walipoingia katika mfumo mpya wa uendeshaji wa kisasa katika kuunda kampuni ambapo viongozi watakaopatikana wanakwenda kuunda bodi ya klabu hiyo wakiungana na wenzao wa upande wa mwekezaji.

Hata hivyo katika kampeni za uchaguzi lipo jambo kubwa lililoshtua kwa kampeni hizo kuwa kali kwa wagombea kutoleana siri zao mbalimbali za kuchafuana sambamba na vurugu katika mikutano hiyo.

Vita kubwa ipo kwa wagombea wa nafasi ya juu ya uenyekiti ambapo inagombewa na Murtaza mangungu na wakili Mosses Kaluwa.

Wagombea hawa wawili wamezusha kambi mbili tofauti ngumu ambazo zimekwenda kuligawa kundi moja klubwa na maarufu ndani ya Simba Friends of Simba (FOS) wakionekana kupigana vikummbo kila mmoja akichagua upande wake.

Huko nyuma

Miaka ya nyuma hali kama hii haikuwa rahisi kuonekana kwa kuwa FOS walikuwa ni kundi lenye nguvu ambapo ili utawale vizuri ulipaswa kuungwa mkono na familia hii ambayo ni kama iliukuwa inaiongoza Simba nyuma ya anayetawala.

Hata alipokuja mwekezaji Mohamed Dewji ‘MO’ bado aliishi na hawa hawa FOS katika kuiongoza Simba akiwachagua wachache kutoka katika familia hii kuungan nao katika bodi ya Simba na mambo yalikwenda.

Kundi hilo liliibuka mwaka 2001 likiwa na vichwa matata kama Dioniz Malinzi, Crescentius Magori, Geofrey ‘Kaburu’ Nyange, Evans Aveva, Mulamu Nghambi, Mohamed Nassor ‘Mkigoma’, Musley Ruwey, Harrison Mutembey, Kassim Dewji, Jerry Yambi na wengineo.

Kundi hilo kwa kiasi kikubwa ndilo iliwapa Simba jeuri ya kutengeneza kikosi chenye nyota wakali na waliowahi kuandika rekodi ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuivua ubingwa Zamalek mwaka 2003.

Ni kundi lililokuwa likikinzana na lile na wanachama wa Simba Taleban, lililokuwa likiamini FOS ndio kivuruge cha timu hiyo hasa enzi za uongozi wa Hassan Dalali, Mwina Kaduguda, Mohammed Mjengwa, Said Rubeya ‘Seydou’, Chano Almasi na wengine waliokuwa upande wa wanachama.

Kaburu aliamsha

Inatajwa hatua ya kwanza ya kutawanyika kwa kundi hili ni kukatwa kwa aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo Geofrey Iriki Nyange Kaburu, ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti na miaka ya nyuma.

Hatua ya kukatwa kwa jina la Kaburu kulizusha sintofahamu kwamba kuna baadhi ya wenzake ndani ya FOS walimzunguka na kugoma kurejea kwake ingawa kukatwa kwake sababu hazikuwekwa wazi kwa hadhara.

Inaelezwa Kaburu alikuwa na watu waliokuwa wanamuunga mkono ndani ya FOS ambao baadaye walikwenda kuunda umoja wa kumpa nguvu Kaluwa.

Hata hivyo mbali na watu hao wa FOS pia uwepo wa Mwenyekiti wa zamani wa Simba Hassan Dalali upande wa Kaluwa na baadhi ya viongozi wenye nguvu na ushawishi katika matawi ya Simba yaliongeza presha upande wa pili.

Mwanaspoti lilipofanya uchunguzi walitajwa vigogo wengi wa FOS kuwa upande wa Kaluwa wakiona klabu hiyo inahitaji kuwa na mtu ambaye atakuwa na nguvu ya kwenda kusimamia upande wa wanachama.

Kwa Mangungu nako

Mtu pekee wa FOS ambaye alionyesha kuwa upande wa Mangungu ni Hassan Othman ‘Hassanoo’ a.k.a Mpambanaji ambaye ndio alikuwa akizunguka na mgombea wake na kumpigania waziwazi na kutaja madhaifu ya mgombea wa upande wa pili.

Mbali na Hassanoo pia wanatajwa vigogo wengine wazito ambao walikuwa katika bodi iliyomaliza muda wake hasa upande wa mwekezaji wakimuunga mkono Mangungu ambaye ndiye mwenyekiti anayetea kiti hicho.

Vita kubwa aliyopigwa nayo Mangungu wakidai alikuwa ni mwenyekiti wa kufungua vikao na kufunga hakuwa na nguvu huku keshi ya mabasi ya klabu hiyo ikiteka katika kampeni zake sambamba na kutowahi kushinda dhidi ya Yanga katika kipindi alichokuwa madarakani ingawa amekuwa akielezea na kuyajibu hayo kwa ufasaha.

Madhara

Vidonda ambavyo vitaachwa baada ya uchaguzi huu vinaweza kuligawa zaidi kundi hilo kwa jinsi wajumbe wake walivyoshambuliana hadharani katika kampeni hizi ambazo zinafikia tamati leo endapo hawatasuluhishwa.

Kumong’onyoka kwa kundi hili kunaweza kuipunguzia Simba nguvu ambapo inawezekana wakaendelea kushambuliana na kupingana kwa siri baada ya uchaguzi huo kumalizika  leo Jumapili Januari 29.

Wenyeviti/Marais Simba tangu 2000-2022
2000-Abdallah Kipukuswa (Kaimu Mwenyekiti)
2001-2002- Kamnambeo
2004-2006- Ayoub Chamshama
2004-2005- Michael Wambura (Mwenyekiti Kamati ya Muda)
2006-2010- Hassan Dalali
2010-2014- Ismail Aden Rage
2014-2018-Evans Aveva
2018-2019- Swedi Mkwabi (alijiuzulu)
2019-2021- Mwina Kaduguda (Kaimu Mwenyekiti)
2021-2023- Murtaza Mangungu

Wagombea
Mwenyekiti
Murtaza Mangungu
Moses Kaluwa

Wajumbe
Dk. Seif Ramadhan Muba
Seleman Haroub
Idd Halifa Kitete
Issa Massoud Idd
Abubakari Zebo
Abdallah R. Mgomba
Injinia Elisony E. Mweladzi
Injinia Rashid M. Khamis
Rodney M. Chiduo
Aziz Mohamed
Asha Baraka
Pendo A. Mapugilo

SOMA NA HII  MAYELE, BANGALA WAMVUTA JANGWANI NAHODHA WA TP MAZEMBE..MWENYEWE AANIKA KILA KITU...