MABAO ya Boubacar Traore na Mohamed Saghraoui wa Monastir yameifanya Yanga kuanza vibaya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kama ambavyo ilikuwa kwa Simba juzi, Jumamosi huko Guinea, jana wawakilishi wengine wa Tanzania wamepoteza kwa mabao 2-0 wakiwa nchini Tunisia.
Hizi ni dondoo muhimu kuhusiana na mchezo huo
Hii ni mara ya pili kwa Yanga kucheza kwenye uwanja wa Olympique de Radès, awamu ya kwanza waliifunga Club Africain bao 1-0 ambalo liliwafanya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mwaka 2018 ambapo Yanga ilitinga hatua ya makundi kwa mara ya mwisho kabla ya msimu huu, napo ilianza vibaya michano hiyo kwa kufungwa mabao 4-0 huko Algeria dhidi ya USM Alger kwenye uwanja wa 5-Juillet-1962, Algiers.
Hii ni mara ya sita kwa Yanga kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika na ya tatu kutinga hatua ya makundi, ikumbukwe kuwa 2016 walitinga hatua hiyo.
Ni wachezaji watatu tu wazawa ambao walianza kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwenye mchezo dhidi ya Monastir ambao ni Kibwana Shomary, Dickson Job na Abubakari Salum ‘Sure Boy’.
Ndani ya dakika sita, Yanga iliruhusu mabao mawili, hii ni mara ya kwanza kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kwenye mchezo wa mashindano.
Azizi KI ambaye alipiga mashuti matatu kwenye mchezo huo, ndiye mchezaji pekee ambaye alionyeshwa kadi ya njano kwa upande wa Yanga.
Yanga ilifanya mabadiliko manne kwenye mchezo huo kwa kuwatoa Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, Kibwana Shomary na Khalid Aucho.
Huku wakiingia , Joyce Lomalisa, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Kennedy Musonda ambaye alienda kushirikiana na Fiston Mayele.
Katika mashuti 15 yaliyopigwa kwenye mchezo huo, Yanga ilipiga saba huku matatu yakilenga lango.