BAADA ya kupoteza mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema nafasi tatu za wazi walizopoteza wachezaji wake wakiwa ndani ya eneo la hatari ndizo zilizowagharimu juzi nchini Guinea, wakichapwa bao 1-0 dhidi ya Horoya kwenye Uwanja wa Jenerali Lansana Conte jijini Conakry.
Akizungumza kutoka nchini humo baada ya kumalizika mechi hiyo Robertinho alisema kipindi cha pili waliwakamata kisawasawa wapinzani wao, na kama si wachezaji wake kukosa mabao matatu ya wazi wakiwa ndani ya eneo la hatari, basi wangetoka na ushindi.
Kwenye mechi hiyo, nahodha John Bocco alishindwa kuweka mpira wavuni akibaki na kipa Moussa Camara mara mbili, huku Clatous Chama naye akikosa bao la wazi baada ya kupiga mpira juu, akiwa ndani ya sita. Pia kipa Aishi Manula aliokoa mkwaju wa penalti kwenye mechi hiyo.
“Kipindi cha kwanza wapinzani wetu walicheza vizuri na wakapata bao moja, na wachezaji wangu walionekana kuwa na uchovu wa kusafiri kwa umbali mrefu, lakini kipindi cha pili nilibadilisha wachezaji wawili ambao walibadilisha mchezo.
“Tumepoteza nafasi tatu za wazi tukiwa ndani ya eneo la hatari, nafikiri nitoe pongezi kwa wachezaji wangu kwa kucheza vema kipindi cha pili na wapinzani kucheza vizuri kipindi cha kwanza,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, alisema Horoya pia walipata ushindi huo kwa kunufaika kucheza nyumbani, hivyo nao wanarejea nchini kukutana na mpinzani mwingine ambaye ni Raja Casablaca ya Morocco, ambayo Ijumaa iliyopita iliiangushia Vipers ya Uganda kipigo cha mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Mohamed wa Tano jijini Casablanca.
“Kwenye mechi hii Horoya walikuwa wanacheza nyumbani na wamenufaika na wenyeji na sisi tunarudi nyumbani. Tunarudi kuangalia mpinzani mwingine tutakayecheza naye kwenye mechi muhimu ambayo sasa nasi tutakuwa nyumbani, tutakuwa mbele ya mashabiki wetu wakitushangilia, kama Raja ni timu kubwa, na Simba nayo ni kubwa vile vile kwa nini tusishinde?” Alihoji kocha huyo.
Bao la wenyeji lilifungwa dakika ya 18 na Pape Abdou N’Diaye akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona ambayo mabeki wa Simba walimsahau mchezaji huyo.
Ni matokeo ambayo yaliweka Simba kwenye nafasi ya tatu ya msimamo, huku ikisubiri mechi yake ya Jumamosi dhidi ya vinara wa Kundi C, Raja Casablanca.
Naye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, aliwaambia waandishi wetu kuwa baada ya mchezo wa juzi na Horoya AC, jana jioni kikosi kilifanya mazoezi ya utimamu wa mwili kabla ya leo kuanza safari ya kurudi Dar es Salaam, Tanzania.
Alisema Kikosi kitapita Ethiopia na kupumzika kwa muda kabla ya kuendelea na safari ambapo wanatarajia kufika Dar es Salaam kesho (Jumanne) saa 9:00 alfajiri.
“Tutakaporejea Dar es Salaam, wachezaji wataingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Raja Casablanca katika uwanja wetu wa nyumbani, pia kuhusu mshambuliaji wetu, Saido Ntibazonkiza, sasa yuko fiti na tayari kwa ajili ya kuitumikia timu katika mchezo ujao,” alisema Ahmed.
Alisema Saido alikuwa na mazoezi maalum pindi timu ilipokuwa Guinea na sasa ataungana na wachezaji wenzake baada ya kupona majeraha.
“Saido tayari amerejea kwenye ubora wake baada ya kupona majeraha yaliyomweka nje siku chache na alikuwa na programu maalum kwa ajili ya kujiweka fiti kwa mechi ijayo dhidi ya Raja Casablanca na Azam FC, atakuwa miongoni mwa kikosi,” alisema Ahmed.
Saido aliumia katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars baada ya kuchezewa rafu na Hamis Ndemla, ambapo alilazimika kufanyiwa matibabu na kupewa mazoezi maalum wakati kikosi cha timu ya Simba kilipokuwa Guinea.
Tayari Simba imetangaza viingilio vya mchezo huo dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, ambapo cha chini ni Sh. 5,000 eneo la mzunguko, VIP B na C ni Sh. 20,000, VIP A Sh. 30,000 wakati Platinum ni Sh. 100,000 huku Platinum Plus ikiwa ni Sh. 150,000.
Kwa upande wa Platinum atakayenunua tiketi atanufaika na usafiri kutoka Hoteli ya Hyatt Regency mpaka uwanjani na kurudishwa hotelini hapo baada ya mechi huku gari likisindikizwa na polisi.
Lakini kwa mujibu wa Ahmed, watakaonunua tiketi hizo za Platinum watanufaika na kifurushi maalum kutoka Simba, chakula na vinywaji wakiwa uwanjani, ambapo alisema tayari tiketi zimeanza kuuzwa kwa njia ya mtandao na baadaye jana walitarajia kutangaza vituo mbalimbali vitakavyouza.