Licha ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga, Kocha Mkuu wa US Monastir, Nivic Darko, ameonyesha kuvutiwa na kiwango walichoonyesha wapinzani wao, akisema ni timu nzuri na huenda ikawa ni ngumu zaidi kwenye kundi lao,lakini akionyesha kushangazwa kufungwa kirahisi mabao ya ‘mipira iliyokufa’
Akizungumza nchini Tunisia baada ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Olympique Hamadi Agrebi Rades, kocha huyo pia amewasifu wachezaji wake kwa kupata ushindi kwenye mechi ya kwanza ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika katika historia ya klabu hiyo.
“Yanga ni timu nzuri, inaweza kuwa ni timu ngumu zaidi kwenye kundi hili, wana wachezaji wenye uzoefu, nawapongeza, lakini wamenishangazwa kufungwa mabao mawili ya mipira ya kutengwa. Lakini nawapongeza vijana wangu kwa sababu ilikuwa ni mechi yetu ya kwanza kucheza kwenye makundi tangu timu hii ianzishwe, tunakwenda hatua kwa hatua mpaka tuone mwisho wake,” alisema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema wamepoteza mechi hiyo, hivyo wanaachana nayo, badala yake wanaangalia mechi ijayo Jumapili dhidi ya TP Mazembe inatakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Yalikuwa ni mabao ya Mohamed Saghafaoui dakika ya 10 na Boubacar Traore dakika ya 16.
Juzi pia kwenye mechi ya Kundi D, TP Mazembe ilianza vema michuano hiyo baada ya kuichapa Real Bamako ya Mali mabao 3-1 kwenye Uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mabao ya washindi yalifungwa na Jephte Kitambala dakika ya 24, Alex Ngonga dakika ya 38 na Patient Mwamba dakika za majeruhi, huku bao la kufutia machozi la wageni likifungwa na Souleymane Coulibaly dakika ya 32.
Baada ya mechi hizo za kwanza, TP Mazembe imekaa kileleni ikiwa na pointi tatu mabao matatu, Monastir ikishika nafasi ya pili kwa pointi tatu na mabao mawili, Yanga ikiwa nafasi ya tatu bila pointi lakini mabao mawili ya kufungwa huku Real Bamako ikishika mkia ikiwa haina pointi, bao moja la kufunga na kuruhusu matatu.