KIKOSI cha TP Mazembe kimewasili juzi jioni nchini tayari kwa mchezo dhidi ya Yanga, lakini kabla hawaondoka nchini kwao kuna kasheshe moja walipambana nalo ndani ya kikosi chao.
Iko hivi. Katika msafara wa wachezaji 25 uliotua hakuna jina la kipa namba moja, Siadi Baggio na sababu ni moja tu kipa huyo alijiondoa kikosini akidai amekuwa anashutumiwa mambo mbalimbali na mashabiki wa timu hiyo.
Lawama za Baggio zilianza mara baada ya kipa huyo kufanya makosa msimu uliopita wakati wakiondolewa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane msimu uliopita.
Mara baada ya kurejea kwenye Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) Baggio aligoma kurejea klabuni hapo na kuukosa mchezo wa timu hiyo uliopita dhidi ya Real Bamako.
Mabosi wa Mazembe licha ya juzi kumuita Baggio kumsikiliza kipa huyo aligoma kurejea na kulazimika kuja nchini na kipa wao aliyedaka mechi iliyopita Mcameroon Narcisse Nlend.
Nlend ndiye aliyedaka mechi ya Real Bamako wakishinda kwa mabao 3-1 huku Mazembe wakiona kwamba kuna ulazima wa haraka kumaliza sakata la Baggio ili arejee katika nafasi yake.