Rais wa Klabu ya AS Real Bamako ya Mali Famakan Dembélé amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo wa Mzunguko wa tatu wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika 2022/23, dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Bara Yanga.
Miamba hiyo itamenyana Jumapili (Februari 25) katika Uwanja wa Machi 26 mjini Bamako, huku wenyeji Real Bamako wakiweka dhamira ya kushinda mchezo huo, ili kujiongezea alama, baada ya kuambulia alama moja dhidi ya US Monastir kufuatia sare ya 1-1 mwishoni mwa juma lililopita.
Dembélé amesema kikosi chao kimekua na maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo, ambao wanaamini utakua na upinzani mkubwa kutokana na uimara wa Yanga, lakini amesisitiza jukumu lao kuu ni kupata alama tatu.
“Sisi ni timu kubwa Afrika na tunacheza nyumbani kutokana na ubora wetu na jinsi tunavyowafahamu Yanga, tunawaheshimu kwa sababu wana kikosi bora na imara, lakini kwetu lazima tutashinda.”
“Tunazihitaji sana alama tatu za mchezo wetu ujao hapa nyumbani, kila mmoja alifadhaika na matokeo yetu dhidi ya US Monastir Jumapili, hatutaki kurudia kosa la kushindwa kupata matokeo mazuri hapa, naamini tutashinda dhidi ya wageni wetu kutoka Tanzania,” amesema Famakan Dembélé.
Hadi sasa msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, US Monastir inaongoza ikiwa na alama nne, ikifuatiwa na Yanga yenye alama tatu, sawa na TP Mazembe inayoshika nafasi ya tatu, huku Real Bamako ikiburuza mkia kwa kuwa na alama moja.