Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddin Nabi amesisitiza jambo zito kwenye kikosi chake, kuelekea mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, dhidi ya AS Real Bamako.
Yanga itacheza ugenini mjini Bamako keshokutwa Jumapili (Februari 26), ikiwa na morari ya hali ya juu baada ya kuibamiza 3-1 TP Mazembe, kwenye mchezo wa Mzunguuko wapili uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa mwishoni mwa juma lililopita.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesisitiza kutoa nafasi kwa wachezaji wenye umuhimu na wanaojituma mazoezini katika kikosi chake cha kwanza, ambacho kitakuwa na jukumu la kusaka alama tatu dhidi ya AS Real Bamako.
Nabi amesema kwa sasa kuna ushindani mkubwa katika kikosi chake cha kwanza, lakini bado kuna baadhi yao wamekuwa wanahisi kama wameshafanikiwa, jambo ambalo analipinga vita kila kukicha.
“Kila mchezaji anatakiwa kupata nafasi ndiyo maana ya timu, niliona kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi kulingana na ratiba tuliyonayo mbele yetu, lakini nimesikitishwa na viwango vya baadhi ya wachezaji ambao hawaonekani kubadilika.”
“Kuna wachezaji ambao wameridhika, hawaonyeshi kuwa na shauku ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza, hiyo ni mbaya na ni kitu ambacho hakitakiwi kuwa kwenye klabu kama hii yenye malengo makubwa,” amesema Nabi.
Tayari kikosi cha Yangakimeshawasili mjini Bamako tangu jana Alhamis (Februari 23), na leo kimeanza mazoezi mjini humo kuelekea mchezo wa Jumapili.