Home Habari za michezo A-Z JINSI WAMOROCCO WALIVYOIYEYUSHA SIMBA KWA MKAPA JANA…MBRAZILI AKALIA KUTI KAVU…

A-Z JINSI WAMOROCCO WALIVYOIYEYUSHA SIMBA KWA MKAPA JANA…MBRAZILI AKALIA KUTI KAVU…

Simba vs Raja

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Klabu ya Simba imeshindwa kutamba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca katika mchezo wa pili hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao ya wenyeji yamefungwa na Hamza Khabba dakika ya 30 kwa shuti kali lililomshinda kipa Aishi Manula huku Soufiane Benjdida akiiandika Raja Casablanca bao la pili dakika ya 83 wakati Ismail Mokadem akafunga la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 85.

Hii ni mechi ya kwanza kwa Simba kukutana na Raja Casablanca lakini ni ya nne kwao kukutana na timu kutoka nchini Morocco.

Mara ya kwanza kwa Simba kukutana na timu kutoka Morocco ilikuwa ni Mei 28, 2011 ilipokutana na Wydad Casablanca katika mchezo wa mchujo kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ambapo katika mchezo huo ilipoteza kwa mabao 3-0, mechi iliyopigwa Uwanja wa Petro Sport uliopo huko jijini Cairo.

Shirikisho la Soka Afrika liliamua timu hizo kukutana baaada ya Simba kushinda rufaa yake iliyoiwasilisha kwa Klabu ya TP Mazembe ambayo ilimtumia kimakosa mchezaji wake, Besala Bokungu.

Mchezo wa pili kwa Simba kukutana na timu ya Morocco ulipigwa Februari 27 mwaka jana ambapo ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika mechi ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika ingawa marudiano yaliyopigwa jijini Dar es Salaam Machi 13 mwaka jana ilishinda bao 1-0.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa Simba kupoteza hatua ya makundi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye michuano ya Afrika kwani baada ya hapo imecheza mechi 10, ikishinda minane na sare mmoja.

Hiki ni kipigo cha pili mfululizo kwa Simba katika hatua hii ya makundi baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Guinea kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Horoya ambayo leo hii pia imelazimishwa suluhu ya 0-0 na Vipers kutoka Uganda.

Kwa matokeo haya yanaifanya Simba kuburuza mkiani mwa msimamo wa kundi C huku Raja Casablanca ikiendelea kushika usukani na pointi sita.

Nafasi ya pili inashikiliwa na Horoya ambayo imejikusanyia pointi nne huku Vipers ikishika ya tatu na pointi moja baada ya timu zote kucheza michezo miwili.

Endapo Simba itashindwa kufuzu kuingia hatua ya robo fainali, ni wazi mkataba wa Mbrazili Robertinho utasitishwa kwani moja ya kipengele kwenye mkataba wake ni kuivusha timu hiyo kwenda Robo Fainali.

SOMA NA HII  BREAKING: SIMBA YATINGA CAF KUOMBA UCHUNGUZI