Home Simba SC GOMES WA SIMBA BADO ANAIFIKIRIA YANGA

GOMES WA SIMBA BADO ANAIFIKIRIA YANGA


 KOCHA Mkuu wa Simba raia wa Ufaransa, Didier Gomes, amesema anafahamu ugumu umeongezeka wa Ligi Kuu Bara, lakini hataki iwe sababu ya kupata matokeo mabaya na badala yake wachezaji wanatakiwa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ili wawaondoe Yanga kileleni.

 

Kikosi cha Simba kipo nafasi ya pili na pointi 46, kililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Mkapa.

Prisons walimtungua Aishi Manula kupitia kwa Salum Kimenya kwa mpira wa faulo nje kidogo ya 18 na Simba walimtungua Jeremiah Kisubi kwa kichwa cha Luis Miquissone.

 

 Gomes amesema matokeo ya ushindi katika kila mchezo kwao ni muhimu, hivyo ni lazima vijana wake wapambane kuhakikisha wanatimiza malengo ya kubeba ubingwa wa ligi na Kombe la FA.

 

Gomes amesema kuwa ana imani kubwa na ubora wa kikosi chake ambacho kinaundwa na wachezaji wengi wenye viwango bora.


“Mchezo wetu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh washambuliaji wangu walikosa umakini uliosababisha tutoke suluhu.

 

“Sitaki kuona makosa yakijirudia, tayari nimekaa na wachezaji wangu na kuwaambia nafasi moja haiwezi kujirudia mara mbili, hivyo kila nafasi tutakayoipata lazima tuitumie vizuri kwa kufunga mabao.

 

“Nafahamu ugumu wa ligi umeongezeka katika mzunguko wa pili, lakini hiyo haiwezi kutufanya tupoteze michezo yetu, kikubwa ninahitaji ushindi pekee ili tuwaondoe walio juu yetu katika msimamo,” amesema Gomes.

SOMA NA HII  SABABU ZA SIMBA KUMRUDISHA CHIKWENDE ZIMBABWE ZATAJWA