Home Habari za michezo BAADA YA KUPONDWA SANA…MWANYETO AANZA KUKIWASHA YANGA…NABI AFUNGUKA ALICHOMFANYIA…

BAADA YA KUPONDWA SANA…MWANYETO AANZA KUKIWASHA YANGA…NABI AFUNGUKA ALICHOMFANYIA…

Habari za Yanga

Baada ya kusemwa kwa kushuka kiwango, beki Bakari Mwamnyeto wa Yanga ni kama amewaziba midomo waliokuwa wanambeza kwa kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe.

Katika mchezo huo Yanga ilishinda kwa mabao 3-1, huku Mwamnyeto akionyesha uwezo wa hali ya juu kwenye mchezo huo.

Hivi karibuni kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema anamuweka nje Mwamnyeto kwa kuwa ana matatizo binafsi na atakapomaliza atarejea kwenye ubora wake na juzi alithibitisha hilo.

Kiwango cha Mwamnyeto kimewaibua mastaa wa zamani wa soka nchini waliosema beki huyo ataendelea kuwa kwenye ubora kwa sababu anajitambua vya kutosha.

Mshambuliaji wa zamani Yanga na timu ya Taifa, Herry Morris alisema Mwamnyeto ni beki mwenye uzoefu kwa sasa na ndio maana anapopata nafasi huitumia vizuri.

Akizungumzia kitendo cha mchezaji huyo awali kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza, alisema hutokea kwa sababu muda mwingine kucheza mfululizo ni changamoto.

“Mwamnyeto alikuja Yanga akitokea Coastal akiwa anacheza kikosi cha kwanza. Alipokuja aliendelea kucheza kikosi cha kwanza na kiubinadamu inabidi mwili upumzike.

“Kapumzika na ndiyo maana kwa sasa amerejea na anafanya vizuri kwenye kikosi cha Yanga. Nadhani akiendelea hapa alipo anaweza kurudi katika timu ya Taifa Tanzania,” alisema.Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema hana shida na beki huyo kwa sababu ni mchezaji mzuri na mkubwa kwenye soka la Tanzania.

“Wewe ukitaka uone ana kitu cha tofauti inabidi ujiulize kwanini kocha amempanga kwenye mechi kubwa. Maana yake anajua ubora wake na hajamuangusha kwenye mchezo.

“Ni tegemeo kwenye kikosi chao na hata timu ya Taifa Tanzania. Aendelee kupambana nafikiri atafika mbali sana,” alisema.

Alipotafutwa kuzungumzia ubora wake, Mwamnyeto alishukuru kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuitumikia timu hiyo huku akisisitiza kuwa mipango ya benchi la ufundi imemsaidia kurejea vizuri uwanjani.

“Mchezo ulikuwa mgumu na wa ushindani. Mipango mizuri kabla ya mchezo ilitekelezwa kwa usahihi kwa kila mchezaji, siyo mimi pekee ukiangalia timu yote kila mmoja alifanya majukumu yake kwa usahihi,” alisema.

Awali, Mwamnyeto alipoteza namba kwenye kikosi cha kwanza na nafasi yake akawa akicheza Dickson Job sambamba na Yanick Bangala na anapokosekana mmojawapo anacheza Ibrahim Abdallah ‘Bacca’.

Kwenye mchezo wa wikiendi iliyopita Mwamnyeto alicheza na Job kisha Bangala alicheza eneo la kiungo cha ukabaji akiwa pamoja na Khalid Aucho.

Mwamnyeto alisajiliwa Yanga 2020 akitokea Coastal Union na mkataba unamalizika mwisho wa msimu huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here