Home Habari za michezo KWA SIMBA HII…MTENDAJI MKUU MPYA ATATOBOA KWELI…?…BARBARA KAMWACHIA SWALI ZITO…

KWA SIMBA HII…MTENDAJI MKUU MPYA ATATOBOA KWELI…?…BARBARA KAMWACHIA SWALI ZITO…

Mtendaji Mkuu wa Simba Iman Kajula kwenye Mkutano Mkuu leo

Karibu kila kitu unachokiona kwenye mtazamo wa kidijitali pale kwenye Klabu ya Simba muasisi wake ni Imani Kajula. Huyu mwamba ni mtaalamu wa masoko kwelikweli. Ni mtu wa soka haswa na kubwa zaidi ni mwana Simba kindakindaki.

Wiki iliyopita Klabu ya Simba ilimtambulisha Imani kuwa mtendaji mkuu. Ni mtu sahihi ambaye amekuja wakati sahihi. Mbona amepewa mkataba wa muda mfupi? Jibu la swali hilo majibu yake yako kwa Imani mwenyewe na klabu yake.

Imani sio mgeni pale Simba. Ni kama kusema mtoto amerudi nyumbani ingawa nyumba imebadilika kidogo. Klabu ya Simba pamoja na changamoto zake, lakini kuna hatua nyingi za maendeleo imezipiga ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni.

Simba ya mwaka 2023 sio ile tena ya 2015. Simba wamekua kibiashara. Simba wamekua kwenye matokeo uwanjani. Kuna kazi kubwa ilianzishwa na ofisa mtendaji wa kwanza, Crescentius Magori. Kuna kazi kubwa ilifanywa na ofisa mtendaji wa pili, Senzo Mazingiza. Kubwa zaidi. Ni kazi iliyotukuka ya Barbara Gonzalez. Huyu mwanadada ndiye mtendaji mkuu wa Simba mwenye mafanikio makubwa katika historia ya Simba na klabu zote hapa Tanzania.

Mikataba mikubwa yote ya Klabu ya Simba imepatikana chini ya uongozi wa Barbara. Mwendelezo wa kutinga robo fainali ya michuano mikubwa Afrika yote imekuja chini ya Barbara. Hakuna kazi ngumu kama kwenda kuvaa kiatu cha mtu aliyefanikiwa.

Imani ana kazi kubwa sana ya kuwafanyia wana Simba. Sina shaka na uwezo wake wa kibiashara. Ni mtaalamu haswa. Taasisi nyingi za fedha hapa nchini zimenufaika na taaluma yake. Wasiwasi wangu mkubwa upo kwenye kusaka makombe uwanjani.

Kizazi cha ìdhahabuì cha Simba ni kama kinaenda machweo. Jua taratibu limeanza kuzama. Hakuna tena LuÌs Miquissone, hakuna tena Larry Bwalya. Ni zama mpya. Ni mambo mapya. Pamoja na kuwa bado John Bocco anafunga lakini sio kwa uwezo ule.

Pamoja na kuwa Erasto Nyoni bado anacheza, lakini sio kwa uwezo ule. Ni kweli Jonas Mkude bado anacheza lakini na yeye ni binadamu. Kuna muda akili inachoka. Kuna muda mwili nao unachoka. Kifupi pale Simba panahitaji utulivu sana kujitafuta upya.

Niliposikia Imani ametangazwa nilijua Simba wamelamba dume, lakini niliposikia kuwa mkataba aliopewa ni wa muda wa miezi sita tu nikapata wasiwasi. Mpira ni mchezo wa muda. Mchezaji anahitaji wakati mwingine muda wa kutosha kuzoea timu mpya. Kuzoea mfumo mpya.

Makocha wakati mwingine wanahitaji muda wa kutosha kutengeneza timu za ushindi. Ni sawa na kwa watawala. Ni sawa na kwa viongozi. Kwa nini ofisa mtendaji mkuu apewa mkataba wa miezi sita? Jibu lipo kwa Imani mwenyewe na klabu yake. Miezi sita ni muda mdogo sana.

Ni vigumu kupata mafanikio kwa muda kwenye mchezo wa soka japo wachache wametoboa. Unamuona Imani akitoboa? Nitumie ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Changamoto kubwa kwa Imani, ni kuyafikia mafanikio ya ofisa mtendaji mkuu aliyeondoka hivi karibuni.

Barbara ameacha alama kubwa sana pale Msimbazi. Hata kwenye masoko pia kunahitaji muda wa kutosha. Nadhani ulikuwa wakati muafaka kwa Klabu ya Simba kumpa Imani mkataba wa miaka miwili au mitatu. Ni mwamba sana huyu mtu sema muda mfupi unaweza usimpe nafasi ya kuleta makuu.

Kwenye Soka letu, watu wanataka sana kuona matokeo mazuri Uwanjani kuliko hata Miundombinu. Kwenye mpira wetu watu wanafurahia zaidi kumfunga mtani kuliko kutwaa kombe. Hapa ndipo Imani anapaswa kuketa Imani kwa wana Simba. Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika imekaribia. Watu wanataka kuona Mnyama anamtafuna mtu hapa kwa Mkapa. Watu wanataka kuona timu inavuka robo fainali.

Pamoja na mtani wao kuimarika, bado Simba wanataka ubingwa wa FA na Ligi Kuu Bara. Hakuna kulala. Pamoja na kutinga hataua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika wana Simba wanataka kuona mtani safari hii hachomoki kwa Mkapa. Wanasimba wanataka kuona mtu anafungwa nyingi siku hiyo. Yanawezekana haya yote ndani ya miezi sita? Labda majibu mazuri anayo Imani Kajula.

Sina shaka na uwezo wa Imani, lakini amekuja wakati mgumu kwa sababu amekuta mafanikio makubwa klabuni. Amekuta Barbara amekichafua sana. Chochote atakachochemka, watu watarudi kwa Barbara kutazama mafanikio. Naheshimu makubaliano ya klabu ya Simba na Imani, lakini mkataba wa miezi sita ni masihara makubwa.

SOMA NA HII  SIMBA YAMALIZANA NA NYOTA HAWA WATATU WA KAZI, YANGA WAJIPANGE