Home Habari za michezo SAA KADHAA KABLA YA KUKIPIGA NA MAZEMBE….FEI TOTO NA MORRISON WAACHA MSALA...

SAA KADHAA KABLA YA KUKIPIGA NA MAZEMBE….FEI TOTO NA MORRISON WAACHA MSALA YANGA..

Habari za Yanga

YANGA itashuka uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa leo Jumapili kucheza mchezo wa pili wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya vinara wa Kundi D, TP Mazembe ya DR Congo.

Kumbuka mchezo wa kwanza wa Yanga, ikiwa ugenini ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir ya Tunisia katika ushindi ambao uliamuliwa kwa mashambulizi ya mipira iliyokufa, wakitangulia kuruhusu bao kwa njia ya adhabu ndogo na baadaye shambulizi la kona.

Ndani ya dakika 15 tu za mchezo huo wa Tunis, Yanga ilishakufa na mchezo kuishia hapo, licha ya kuchakarika kwa dakika zilizosalia ili kurejesha mabao hayo bila mafanikio.

Kikosi hicho cha Kocha Nasreddine Nabi kilipambana kusawazisha mabao hayo na licha ya kutawala vipindi vyote vya mchezo huo lakini kuna ubora ulikosekana katika kikosi chao.

PENGO LA FEI TOTO

Yanga ilicheza mchezo wa kwanza wa CAF msimu huu bila ya kiungo wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kuwa pigo kubwa kwao mbele ya Monastir, Jumapili iliyopita.

Iko hivi. Yanga ilimtumia kiungo Stephane Aziz KI kucheza nafasi anayotumika sana kuicheza Fei Toto na ukweli ni kwamba Mbukinabe huyo aliipambania sana timu, japo mambo yalienda harijojo.

Kuna kitu ambacho Aziz KI anatofautiana na Fei Toto hasa kasi ya kupandisha mbele mashambulizi kwa haraka ambacho Fei Toto anamzidi KI.

Ukimuangalia Aziz KI anacheza soka la kiufundi zaidi, lakini Fei Toto akiwa na maamuzi ya haraka anapokuwa karibu na uso wa goli la wapinzani, hapo anaweza kupiga shuti na lolote linaweza kutokea kama sio kufunga yeye basi anaweza kufunga mwingine.

Utakumbuka katika mchezo wa mwisho ambao Yanga iliutumia kutinga hatua ya makundi dhidi ya Club Africain, Nabi alichukua uamuzi mgumu wa kumweka nje asubiri Aziz KI na kuanza na Fei toto ingawa bao la ushindi lilikuja kufungwa na raia huyo wa Burkina Faso alipoingia.

Aziz KI anatakiwa kusukwa zaidi kuongeza ubora ambao unaweza kuipa Yanga wepesi wa kupasua katika eneo lao la kati akiunganisha na safu ya ushambuliaji.

MORRISON NALO TATIZO

Ukiangalia Yanga lazima wakubali kwamba kwa sasa hawana winga hatari ambaye anaweza kuwabeba kwa akutumia ubora wake wa kufungua ngome ya wapinzani.

Yanga sasa inalazimika kuwatumia kwa nyakati tofauti mawinga Jesus Moloko, Twisila Kisinda, Farid Mussa na wakati mwingine Dickson Ambundo.

Ukiwatazama mawinga hawa wanapocheza mechi kubwa utagundua kocha wa Yanga anakuwa na kazi nzito kuweza kuwa na kikosi bora, kama sio wachezaji kubadilika kama itawezekana, basi Yanga ianze kujipanga upya kwani hapo sio uhakika kwamba wanaweza kusumbua kwa mawinga kama hao.

Wangeweza kuwa na mtu bora kama winga Bernard Morrison, ambaye bado ameendelea kuwa na filamu yake akiwa anatumika kukaa nje zaidi kuliko uwanjani.

Morrison ni usajili ‘kichaa’ ambao Yanga iliufanya kwani ameshindwa kukidhi kiu ya waliomsajili wakiamini kazi ambayo aliifanya akiwa na Simba katika mechi za CAF ndio usajili ambao ungewabeba katika mechi hizi kubwa lakini imekuwa tofauti.

Morrison ana ubora wa kujua mbinu za kuufungua ukuta wa wapinzani na akasababisha hatari kubwa, ubora ambao Yanga walilazimika kuvunja benki kumrudisha lakini mambo yamekuwa kinyume chake.

Inawezekana Yanga isionyeshe lakini uhakika itakuwa lazima haimuangalii Morrison kwa jicho zuri sitashangaa kusikia lolote gumu mkataba wake utakapoisha kwa jinsi alivyochangia kumuachia msala Nabi katika mechi hizi za CAF.

MIPANGO TU

Licha ya mapengo ya nyota hao wawili, bado Yanga inaweza kutoboa leo Jumapili kama Kocha Nabi atakisuka kikosi chake vyema tofauti na mechi ya ugenini waliyopoteza 2-0 kwa US Monastir ya Tunisia.

Yanga bado ina kikosi kipana cha kupambana na timu yoyote, ilimradi tu benchi liamue lianze na nani na pale mambo yanapoenda kombo kufanya mabadiliko ya haraka yanayoweza kuibeba.

Katika mechi iliyopita ya kundi hilo, Kocha Nabi na wenzake walichelewa kuwatoa Tuisila Kisinda, Kibwana Shomary na Khalid Aucho na kuwaingia Mudathir Yahya na Kennedy Musonda na Joyce Lomalisa ambao waliichangamsha timu wakati muda ukiwa umeyoyoma.

Mechi za kimataifa wakati mwingine zinahitaji maamuzi magumu yenye lengo la kupata matokeo chanya, kitu ambacho Nabi na jopo lake wanatakiwa kufanya kama wanataka kutoboa mbele ya TP Mazembe yenye rekodi nzuri kwenye michuano ya CAF na hata mbele yao kwani katika mechi mbili za awali walizokutana shirikisho makundi mwaka 2016, Wakongo walishinda zote nje ndani.

SOMA NA HII  FT: SIMBA SC 5 - 0 MTIBWA SUGAR ....SAKHO AIBUKA NA STAILI MPYA...AKPAN AKUMBUKWA...

2 COMMENTS