Baada ya TFF kutupilia mbali mapitio ya hukumu ya Mchezaji wa Yanga Feisal Salum “Fei Toto” na maamuzi ya awali kubaki na uhalali wa kuwa mchezaji huyo ni mali ya Yanga kwa kuwa bado ana mkataba na Yanga.
Wadau wengi wa masuala ya michezo na hasa kandanda wameonekana kumuhurumia mchezaji huyo huku ikionekana kuwa yeye hayuko tayari kurejea Yanga.
Ni takribani miezi mitatu sasa Feisal hajacheza mchezo wowote wa Kimashindano na kuendelea kupingana na maamuzi ya Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF ni kuendelea kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu zaidi.
Sasa mchambuzi nguli wa michezo nchini, Edo Kumwembe kupitia kipindi cha Sports Arena amefunguka ushauri ambao anaona kwa upande wake utakuwa na faida kwa pande zote mbili zinazovutana yani Yanga na Feisal.
Edo anasema;
“Kama ningekuwa kiongozi wa Yanga mara baada ya majibu ya rufaa ya Fei kutoka, ningejitokeza hadharani na kutangaza kabisa thamani ya Fei Toto hivyo kwa timu inayomtaka ije itoe kiasi hicho cha pesa maisha yaendelee.
“Kuliko mvutano uliopo hivi sasa baina yao maana mawazo ya kwenda CAS kama fei atakuwa nayo ni kujiweka nje ya uwanja kwa kipindi kingine kirefu zaidi”.
Mwishoni mwa mwaka jana (2022) Feisal aliomba kuvunja Mkataba na Klabu ya Yanga huku Timu ya Azam FC ikihusishwa kumuhitaji ndani ya kikosi chao.
Mkataba wa Feisal na Yanga umebakisha mwaka mmoja, na rasmi unaisha Mei 30, 2024.