Aliyekuwa mfadhili wa Simba, Azim Dewji amempongeza beki Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa timu ya Taifa Tanzania.
Bacca alipewa nafasi ya kuanza katika mchezo wa kufuzu Afcon 2023 kati ya Tanzania dhidi ya Uganda iliyomalizika kwa Tanzania kushinda bao 1-0 likifungwa na Simon Msuva dakika ya 68.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dewji amesema mchezaji huyo alijituma ndani ya uwanja kuhakikisha lango linakuwa salama.
“Nawapongeza Yanga kwa kumuibua mchezaji huyu kwa sababu kama wao leo hii tusingemuona na asingeweza kuisaidia Taifa,”
“Waliomuona kwenye skauti yao wamefanya kitu kizuri na jambo bora kwa Taifa, kuna muda inabidi tuwaibue wachezaji wetu wenyewe kuliko kununua nje,”
Dewji ameongeza akisema; “Sio kwenye Taifa tu amefanya vizuri kwenye mchezo wake wa kwanza hata kule katika klabu yake alipopewa nafasi kimataifa alifanya vizuri,”
Bacca alisajiliwa na Yanga baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na kikosi cha KMKM katika kombe la Mapinduzi.
Tanzania itarudiana na Uganda Jumanne Machi 28 katika uwanja wa Mkapa.