Home Habari za michezo BAADA YA KUTINGA ROBO FAINAL KIBABE…MBRAZILI SIMBA AAPA KUIVIMBIA YANGA…APELEKA FAILI ‘KWA...

BAADA YA KUTINGA ROBO FAINAL KIBABE…MBRAZILI SIMBA AAPA KUIVIMBIA YANGA…APELEKA FAILI ‘KWA MABOSI KAZI’…

Habari za Simba SC

Mashabiki wa Yanga wanatamba mtaani kutokana na timu hiyo kuongoza Ligi Kuu Bara kwa tofauti na pointi nane, lakini wakiamini watani wao wa jadi Simba watawapa taji kwa msimu wa pili mfululizo watakapovaana nao Aprili 16 timu hizo zitakapokutana kwenye Kariakoo Derby.

Hata hivyo, kocha mkuu wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameshajipanga mapema na kulikabidhi faili ya Yanga kwa mabosi wa klabu hiyo ya Msimbazi, huku akisisitiza hayupo tayari kuwa daraja la kuwapa vinara hao taji mgongoni mwake watakapovaana Kwa Mkapa.

Yanga inaongoza msimamo kwa sasa na pointi 65, huku Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na alama 57 na vinara wao wa Ligi Kuu na Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika inahitaji ushindi wa mechi tatu zijazo ikiwamo dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa Aprili 11, Simba ya Aprili 16 na ile ya Singida Big Stars itakayochezwa Aprili 25 mjini Singida.

Yanga ikishinda mechi hizo itafikisha pointi 74 ambazo hazitaweza kufikiwa hata na Simba ambayo ikishinda mechi zote tano zitakazosalia baada ya kuumana na Yanga itafikisha alama 72 tu, na hilo ndilo asilotaka Robertinho aliyewasilisha ripoti ya ubabe wa wapinzani hao ili lifanyiwe kazi mapema.

Akizungumza Robertinho amekiri kuna changamoto kubwa ya kuizuia Yanga kubeba ubingwa kutokana na pengo la ponti, lakini amewasilisha projekti kabambe kwa mabosi wa timu hiyo itakayokwenda kupindua ufalme wa wababe hao wenye mataji 28 ya Ligi Kuu tangu 1965.

Robertinho alisema kama mabosi wa Simba wataifanyia kazi projekti hiyo kwa usahihi anaamini Simba itapindua meza kwa kurejesha heshima kwa kuwa na kikosi imara lakini itarudisha utawala wake, huku akisisitiza msimu huu hataki awe daraja la kuipa Yanga taji mapema.

“Nimeandaa projekti yangu ambayo ni siri yangu na viongozi wa klabu wanayo tayari, nikiri kuwa sio rahisi kuwakamata Yanga licha ya kwamba tutaendelea kukimbizana nao hadi tuone mwisho kipi kitatokea,” alisema kocha huyo na kuongeza;

“Hii projekti nimeweka kila kitu ambacho naweza kusema viongozi kama wataitekeleza nina imani Simba ambayo wanaitaka ya kuwa na kikosi imara lakini pia kutamba hapa Tanzania itarejea kwa kishindo.

“Humo ndani kwa ujumla wake nimegusia benchi langu, kikosi chetu, hizi ni idara ambazo lazima tuziboreshe ili turudishe heshima yetu kama Simba, Simba haitakiwi kumilikishwa nafasi ya pili au kuwa na pengo kubwa la pointi kama hili ambalo tunalo sasa.”

Robertinho aliongeza anajua wapi kikosi chake kina changamoto na kwamba ni aina gani ya mastaa wanaohitajika katika kuboresha kwanza timu yake.

“Furaha yangu sasa kikosi tulichonacho kimeanza kujua kitu gani tunachotakiwa kushika jinsi ya kucheza soka la kisasa, wachezaji wengi wameshika mbinu tunazotaka.

“Yapo maeneo lazima tuyaboreshe kwa kuleta watu sahihi, hii ni klabu kubwa ukiwasikiliza viongozi wa klabu na malengo yao nadhani utapata picha ni watu aina gani ambao tutalazimika kuwaongeza.”

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATANO