NYOTA wa zamani wa Simba, Eric Sagala amwemwagia sifa straika mpya wa timu hiyo, Jean Baleke kwa kufunga bao zuri katika mchezo wa mwisho wa Kundi C katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Athletic, uliopigwa jijinio Casablanca, nchini Morocco.
Sagala alisema kwa namna mfungaji huyo alivyotulia mbele ya mabeki wa Raja baada ya kupewa pande na kiungo Mzamiru Yasini inaonyesha wazi Baleke analijua goli kwani ufungaji ule sio wa kubahatisha ni wa hesabu nyingi za mchezaji.
Katika mchezo huo Simba ilikubali kichapo cha 3-1, huku Beleke akifunga dakika ya 75 kwa kuubetua mpira uliompita kwa juu kipa wa Raja, Anas Zniti aliyekuwa ametoka kukabiliana naye.
Mara alipopokea pasi ya kupenyeza kutoka kwa Mzamiru aliutuliza mpira kwa mguu wa kushoto na kuuchopu kwa mguu wa kulia na kumshinda kipa wa Raja.
Sagala aliyeichezea Simba kati ya 1987-1990 kabla ya kujiunga na Township Rollers na BDF 1X za Botswana, alisema Baleke analijua goli na atakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo akiendelea kuaminiwa.
“Achana na matokeo, mimi nazungumzia ule ufungaji sisi tuliocheza mpira tunajua na ndio maana nakwambia soka ni ufundi, mjinga mjinga hawezi kufunga vile zile ni hesabu nyingi sana,” alisema nyota huyo aliyewahi pia kupita CDA Dodoma na kuongeza;
“Kwamba kipa kaja niubetua juu kwa kiwango hichi ili ukaingie kwa juu ile ni hatari sana nasema hivi Simba wamepata mtu sasa wamlishe mipira sahihi sio tena aanze kuhangaika mara kutuliza kuweka sawa pasi mbovu.”
Hata hivyo, Sigala aliishauri timu hiyo kuongeza umakini katika mchezo wa robo fainali kwani ina changamoto ya mawasiliano kwa mabeki wa kati.
“Kuna shida hata magoli waliyofungwa unaona, sasa hili kocha aliangalie kwa umakini,watu wakijua udhaifu wako ndio wanautumia,” alisema Sagala.






