BAADA ya misimu miwili wazawa kuwapiku wageni kunyakua tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, awamu hii ni kama nyota njema inachomoza kwa mapro.
Ipo hivi: Kabla ya wazawa hao kunyakua tuzo hiyo, msimu wa 2017/18 alichukua Emmanuel Okwi (20), akafuatia Meddie Kagere 2018/19 mabao 23, 2019/20 mabao 22 wote walikuwa Simba.
Kabla ya hapo 2016/17, mzawa Simon Msuva alichukua akiwa Yanga akimaliza na mabao 14 yalikuwa sawa na Abduralhman Mussa wa Ruvu Shooting.
SOKA LA BONGO linakuchambulia kwa njia ya data namna ambavyo maproo msimu huu wanaonyesha taswira ya kuwapindua wazawa ambao miaka miwili nyuma ndio walichukua tuzo ya ufungaji bora.
Misimu miwili ya wazawa 2020/21, John Bocco alimaliza na mabao 16 nyuma yake alikuwepo Cris Mugalu na mabao 15 na wote walitoka Simba.
Msimu wa 2021/22, George Mpole akiwa Geita Gold alimaliza na mabao 17 nyuma yake alikuwepo Fiston Mayele wa Yanga aliyekuwa na 16 na Ligi Kuu inayoendelea ni kinara wa mabao 15.
Wakati Mayele anaongoza kwa mabao 15 na Moses Phiri wa Simba akiwa na 10, kuna maproo nje ya Simba na Yanga ambao wanamiliki mabao mengi ambao wakipambana wanaweza wakapindua ufalme wa wazawa.
Zikiwa zimebaki mechi tano kwa kila timu ukiondoa Simba na Yanga ambazo zina mechi sita vita ya mapro kuwinda tuzo ya TPL ili kurejesha heshima baada ya misimu miwili kukosa iko juu sana.
Hadi sasa wachezaji wa kigeni 53, wamefunga mabao 156 wakichuana na wachezaji 124 wazawa wenye jumla ya mabao 275 huku Mayele akiongoza kwa kupachika mabao 15 kwa upande wa wageni na kwa upande wa wazawa John Bocco amepachika mabao 10 akiachwa mabao matano tu na mgeni.
KAULI YA WAZAWA
Kinara wa mabao msimu uliopita ambaye anakipiga FC Lupopo, George Mpole amesema ushindani msimu huu ni mkali huku akilia na wazawa kushindwa kuendeleza rekodi aliyoiacha.
“Namwona Mayele akifikia malengo aliyoshindwa msimu uliopita kutokana na ushindani uliokuwepo baina yetu kutokana na wazawa kukosa mfululizo wa kufunga kila mchezo kama ilivyo kwa upande wake na amekuwa akitumia kila nafasi anayoitengeneza;
“Reliants Lusajo, Sixtus Sabilo walianza vizuri wakakwama, mkongwe John Bocco katumia dakika chache kafunga mabao 10 hadi sasa akipata nafasi ya kucheza dakika zote kwenye mechi zilizobaki anaweza kumpa presha Mayele ambaye amekuwa kinara kwa mabao 15,” alisema Mpole.