SIMBA imeanza hesabu kali sana ikitaka kuangusha mbuyu wa Wydad Casablanca na kocha wa timu hiyo Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ametamka kwamba anakiamini kikosi chake na kitashtua kwa kile watakachokifanya kwenye robo.
Na Robertinho amewaambia mashabiki na wadau wa soka nchini, wafute matokeo ya awali Simba dhidi ya Wydad ilipochapwa mabao 3-0 iliyopigwa Mei 28, 2011.
Simba inaumizwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo huo ndani ya dakika sita za mwisho, ikiwa ni mechi ya play-off kusaka timu ya kwenda makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika kikosi cha Simba kipindi hicho dhidi ya Wydad ina wachezaji wanne tu ambao bado wanacheza soka hadi sasa akiwamo Haruna Shamte na Kelvin Yondani waliopo na Geita Gold, Juma Nyosso aliyepo Ihefu na Emmanuel Okwi anayecheza soka la kulipwa nchini Iraq.
Wengine waliocheza mechi hiyo iliyopigwa Cairo, Misri na wameshastaafu ni soka la ushindani ni; kipa Juma Kaseja, Amir Maftah, Jerry Santo, Shija Mkina, Mohamed Banka, Amri Kiemba na Hillary Echesa huku kocha wao akiwa Mganda Moses Basena.
Simba kujiandaa na mchezo huu walikusanyika kwa wiki moja tu baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwajulisha kuwa watatakiwa kucheza dhidi ya Wydad baada ya TP Mazembe iliyokuwa imezifunga timu hizo hatua za awali kukutwa na hatia ya kumtumia kimakosa Janvier Besala Bokungu.
Kikosi hicho kuingia kambini kwa siku tatu wakitokea majumbani baada ya msimu kumalizika na baada ya siku hizo walisafiri kwenda Misri na kuweka kambi ya siku chache na kuingia kwenye mechi hiyo na kufungwa mabao dakika za jioni kabisa baada ya baadhi ya wachezaji kuamini wanaenda kwenye penalti na kufungwa mabao matatu kwenye dakika nane tu.
NGOME YA SIMBA TUNISIA
Robertinho ameliambia SOKA LA BONGO kuwa ameshaanza hesabu ndefu kuelekea mchezo huo na kwamba ngome yake ya kubwa ameiweka Tunisia.
Kuna wataalam wa soka nchini humo ambao ni marafiki amewapa kazi ya kuisoka Wydad na kuicheza mechi hiyo kumpa taarifa za kutosha wakisaidiana na msaidizi wake Ouanane Sellami ambaye pia ni Mtunisia.
“Tulichoanza sasa ni kukusanya taarifa za Wydad kuna namna ambavyo wanacheza nyumbani na ugenini, kitu bora kwetu ni kuwa tutaanzia hapa mbele ya mashabiki wetu ambao ni kati ya mashabiki bora Afrika,”alisema Robertinho.
“Hata wao wanajua ubora wa Simba inavyocheza nyumbani, nataka kusema kuwa Simba itakayocheza mechi hizi mbili itakuwa na utofauti mkubwa wa ubora tofauti tulivyocheza mechi za makundi.”
Winga huyo wa zamani wa Brazil ambaye katika mechi 6 za CAF alizoiongoza Simba ameshinda tatu na kupoteza tatu alisema hata mfumo wa uchezaji utakuwa tofauti na ule wa 4-3-3 ambao waliutumia katika mechi mbili dhidi ya wapinzani wa Wydad nchini kwao Raja Athletic Club.
“Wakati tulipoanza dhidi ya Horoya na tukapoteza hakuna ambaye alijua leo tutakuwa hapa, Simba ni klabu kubwa haiwezi kumuogopa mpinzani yoyote Afrika, tutabadili mpaka mifumo ya uchezaji wetu, tutakapoona mbinu sahihi za kushindana na wapinzani wetu.
“Jambo zuri hata wachezaji wangu wanajua kubadilika na kucheza kwa nidhamu kubwa katika mechi kama hizi, mimi napenda mechi ngumu kama hizi unaposhinda thamani yako kama mchezaji inaongezeka zaidi na hiki ndicho nimewaambia wajiandae na hili, tunatakiwa kucheza kwa ubora na kuondoa makosa naamini tukicheza kama timu kwa kutekeleza majukumu yetu kwa umoja itakuwa ni mechi rahisi.”
NYUMBANI NA UGENINI
Simba faida kubwa ya mechi hizi mbili tofauti na mwaka 2011 ilipokutana na Wydad watacheza mechi mbili za nyumbani na ugenini ambazo watatakiwa kujipanga kwanza kushinda wakiwa nyumbani utakaochezwa kati ya Aprili 21 na 22 kisha kujipanga na mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki moja baadaye.
Simba ukiondoa kupoteza dhidi ya Raja msimu huu nyumbani rekodi zinaonyesha Waarabu hao wanatakiwa kjjipanga vizuri wakati wakitua Uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana ndio jeuri kubwa wa wekundu hao.
Tayari kiungo Clatous Chama anayeongoza kwa ufungaji katika kikosi hicho akiwa na mabao manne ameshawatumia salamu Wydad akiandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa ” Kwenu Wydad tuko zaidi ya tayari kuliko wakati wowote kabla, walete..”aliandika Chama, kauli ambayo itawashtua Waarabu hao lakini ikisapotiwa kwa ukubwa na Simba.