Home Habari za michezo BARUA HII YA FEI TOTO YAZUA MAZITO MAPYA…”UONGOZI WA YANGA ULINITESA SANA

BARUA HII YA FEI TOTO YAZUA MAZITO MAPYA…”UONGOZI WA YANGA ULINITESA SANA

BARUA HII YA FEI TOTO YAZUA MAZITO MAPYA...

Sakata la kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum ‘Fei Toto’ dhidi ya Yanga limeingia sura nyingine baada ya upande wa mchezaji huyo kuwasilisha barua ya kuvunja mkataba, huku mabosi wa klabu hiyo wakiweka vipengele wanavyotaka vitekelezwe kabla ya kurudiwa kwa shauri, Aprili 25.

Kesi hiyo mpya iliitishwa jana na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambayo ilikuwa ikisikilizwa sambamba na kesi nyingine, huku upande wa Fei uliwakilishwa na yeye mwenyewe pamoja na wasimamizi wake akiwamo Wakili maarufu nchini, Fatma Karume na Jasmine Razack huku upande wa Yanga uliongozwa na Mwanasheria wa klabu hiyo, Simon Patrick.

Kwa mujibu wa chanzo makini kutokana ndani ya kamati hiyo ni kwamba barua ya Fei ilijadiliwa na Yanga kuwasilisha vipengele vya kutaka kiungo auvunje mkataba huo na kutaka wautekeleze kabla ya kuitwa tena kwa shauri hilo, Aprili 25.

Hakuna upande uliokuwa tayari kuzungumzia suala hilo, lakini hii ni kesi ya pili kati ya Fei na Yanga tangu alipotagaza kuvunja mkataba mwishoni mwa mwaka jana na kuilipa klabu hiyo Sh 112 Milioni zikiwamo za mishahara ya miezi mitatu, lakini akagomewa kabla ya kuburuzwa katika kamatai hiyo iliyoa uamuzi wa kuendelea kumtambua kuwa mali ya Yanga.

Hata hivyo, Fei aliamua kuomba marejeo ya hukumu hiyo ya kwanza kesi iliyosikilizwa mwezi uliopita na kuamuliwa kurejea Yanga kwani alivunja mkataba kienyeji na hivyo anaendelea kuhesabika kuwa ni mali ya Yanga na mabosi wa klabu hiyo kuiwacha milango wazi kwa kiungo huyo kurejea klabuni.

Lakini Fei aliamua kuandika barua kwa TFF kuomba kuvunja mkataba na Yanga kwa kufuata taratibu baada ya mipango ya kwanza kukwama na ndipo jana kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 8 mchana yakatolewa maamuzi hayo baada ya pande hizo mbili kusikilizwa na kukubaliana kukutana Aprili 25.

Wakati kamati hiyo ikikutana jana kujadili barua ya Fei iliyoandikwa Machi 6 ikiwa na kurasa moja, alichokiandika kwenye barua hiyo kumeibua maswali kwa walioiona kwani kuna mistari iliyozaa maswali matano matata.

Katika barua hiyo Fei ameandika ombi la kuvunja mkataba na Yanga akieleza uamuzi huo unatokana na kutoelewana kwa muda mrefu pamoja na kupitia manyanyaso ya mbalimbali na uongozi wa klabu hiyo ya Yanga na kuitaka kamati kushughulikia jambo hilo, kwa vile anataka kucheza timu inayompa ushirikiano na inayothamini na kujali masilahi yake.

Vipengele hivyo vya barua hiyo ndivyo vilivyozaa utata na maswali matano ambayo Mwanaspoti imekuainisha hapo chini;

MASWALI MATANO
1. Ni klabu gani ambayo Fei anasema inampa ushirikiano na kujali maslahi yake tofauti na Yanga ambao ni waajiri wake?
2. Kama amekiri kimaandishi kuwa, kuna klabu inampa ushirikiano na kujali maslahi yake, kamati itambana aitaje na ikishaijua itachukua hatua gani, kwa vile kikanuni ndio iko nyuma ya uamuzi wa Fei kuikacha Yanga?
3. Fei kama alikuwa haelewani na Yanga kwa muda mrefu kama alivyoandika kuwa, amepitia manyanyaso, kwa nini alikubali kusaini mkataba mrefu wa kuitumikia timu hiyo huku akijua hana mahusiano nayo mazuri?
4. Je, kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji inayo mamlaka kuvunja mkataba halali wa mchezaji kwa sababu nyingine tofauti na zile zinazoainishwa katika muongozo wa hadhi za wachezaji wa kimataifa?
5. Iwapo Fei alikuwa ananyanyaswa kwa muda mrefu, amewahi kuwasilisha malalamiko kwa kamati hiyo au vyombo vingine vya soka vinavyowezakutumika kama uthibitisho wa ombi lake ya kuvunja mkataba na Yanga?
Bila ya shaka ni suala la kusubiri hiyo Aprili 25 kuona kama Yanga itatekelezewa vipengele na Fei atakubaliwa kuvunja mkataba huo na klabu hiyo unaotarajia kufikia tamati mwakani.

SOMA NA HII  SIO AL AHLY MLETENI YEYOTE, SIMBA WATAMBA