HAYA ndio maajabu ya Stephane Aziz KI. Wakati ambao wadau na mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiona kiwango chake kimeshuka kwa vipindi tofauti, nyota huyo wa Kimataifa kutoka Burkina Faso amekuwa akiibuka na kuwashangaza kwa kufanya makubwa.
Ni nani ambaye alijua atauwasha vile kwenye mchezo uliopita wa Yanga wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar? Unakumbuka kilichotokea dhidi ya Club Africain kule Tunisia wakati wakipigania nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na vipi kuhusu mchezo wa kwanza wa dabi msimu huu kwenye Ligi.
Wakati ambao Aziz Ki anajitafuta amekuwa na maajabu yake na kile kilichotokea dhidi ya Kagera kwa kufunga hat trick ya kwanza akiwa na Yanga ilikuwa ni muendelezo tu wa kile ambacho amefanya kwa nyakati tofauti, jambo lililomfanya Kocha Nasreddine Nabi kuchekelea.
Akizungumzia kurejea kwa kiwango cha Aziz KI, kocha Nabi alisema kikao ambacho walifanya na mshambuliaji hiyo kimechangia juhudi kubwa za kutaka kukuona anarudi katika kiwango chake.
Nabi alisema Aziz KI anatakiwa sasa kuendeleza moto wa kufunga na kucheza vizuri.
“Tulifanya juhudi kubwa ya kuongea naye na kumuelewesha jinsi anavyotakiwa kurudi kati11ka kiwango chake, mimi binafsi niliongea naye lakini pia wasaidizi wangu na hata viongozi nao walikuwa wakifanya hizi juhudi,” alisema Nabi.
“Tulikuwa tunaumia mioyo yetu kumuona anakuwa katika wakati mgumu licha ya jina lake kubwa, nafikiri sasa amepata sehemu ya kuanzia na kuendeleza makali yake ili azidi kufanya makubwa zaidi.”