Home Habari za michezo HUYU HAPA MCHEZAJI WA KWANZA…KUTOKA YANGA KWENDA SIMBA…OKWI,TAMBWE,MORRISON WANASUBIRI

HUYU HAPA MCHEZAJI WA KWANZA…KUTOKA YANGA KWENDA SIMBA…OKWI,TAMBWE,MORRISON WANASUBIRI

HUYU HAPA MCHEZAJI WA KWANZA...KUTOKA YANGA KWENDA SIMBA...OKWI,TAMBWE,MORRISON WANASUBIRI

JANA Aprili 16, 2023 ilikuwa dabi ya Kariakoo. Miaka 40 iliyopita tarehe kama hiyo, Simba ilikubali kichapo cha mabao 3-1.

Ndio ilikuwa ni Aprili 16, 1983. Simba ilikuwa imetoka kujiandaa na Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) katika nchi ya Brazil.

Katika mchezo huo, uliopigwa katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru), Simba ndio ilianza kuandika bao la kwanza lililofungwa na Kihwelo Mussa ‘Super’ marehemu, huyu ni kaka mkubwa wa Kocha wa KMC, Jamhuri, Mtwa, Mhehe (marehemu), Mwesa na Mwavanga Kihwelo.

Twende kwenye pointi, wachezaji wengi wamecheza dabi ya Kariakoo na wanaijua vizuri sana lakini wapo ambao wamecheza pande zote mbili.

WA KWANZA YANGA KWENDA SIMBA

Siyo wengi ambao wanalijua hili, yupo mchezaji mmoja wa kwanza kabisa kutoka Yanga na kujiunga na Simba.

Alikuwa ni straika mmoja hatari sana, Mambo Mzinga miaka ya mwanzoni ya 1960.

Mambo Mzinga alikorofishana na viongozi wa Yanga na kujiunga na Simba. Nchi ilitikisika kwa kweli.

Lakini viongozi wa Yanga, walitulia na kuamini ni jambo la kawaida baada ya kuamini straika wao, Mambo Mzinga alikuwa amekwisha na nguvu zake zote alikuwa amezimaliza Yanga.

Kweli Mambo Mzinga hakuwa na nguvu tena na alienda Simba kwa hasira tu.

WALIOPO LEO HII

Hawa hapa wachezaji ambao leo hii wanaweza kucheza dhidi ya Simba au Yanga wakiwa tayari wameshavaa jezi ya timu mpinzani.

Kipa Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Saido Ntibanzokiza na Bernard Morrison.

KUMBE NI HASIRA TU

Wachezaji wengi walifuata mkondo wa Mzinga Mambo. Sio kama walizihama Simba na Yanga kwa sababu walikuwa na mapenzi na timu ya pili, la hasha.

Wapo walihama Simba na kujiunga na Yanga wakiwa bado na mapenzi na timu hiyo na wapo waliohama Yanga na kwenda Simba lakini bado walikuwa na mapenzi na timu hiyo.

Wachezaji hao walihama kwa sababu ya kukosana na baadhi ya viongozi wa klabu hizo.

SIO WENGI LAKINI WAPO

Mmoja kati ya wachezaji hao ni Mambo Mzinga, hasira zilimfanya akaihama Yanga na kwasababu hakukuwa na timu nyingine kubwa ya kwenda akaona bora aende Simba.

Mchezaji anapoenda kujiunga na timu pinzani kama Simba au Yanga anaamini anawakomoa viongozi aliovurugana nao katika timu yake ya awali. Hasira zake zote anaamua kuzimalizia kwa kuhamia timu pinzani.

MOGELLA NA MMACHINGA

Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ mwaka 1992 alihama Simba na kujiunga na Yanga na kwenda kuitwa DHL.

Kitendo chake kilishtua sana na kilitingisha nchi lakini baadaye Mogella alijutia uamuzi wake huo. Kwani alipoteza mtandao wote wa Simba ambao aliutengeneza kwa miaka takribani 10.

Captain Morgan alipoteza hata marafiki kwa kitendo chake cha kuikacha Simba.

Hata hivyo, baadhi ya watu wa Yanga waliokuwa wakimjua Mogella hawakumwamini kama kweli alikuwa amejiunga nao kwa mapenzi.

Hata marehemu Abbas Gulamali aliyemchukua Mogella hakuamini kama kweli angeweza kufanya vizuri Yanga.

MMACHINGA NAYE YALIMKUTA

Straika hatari wa Yanga, Mohammed Hussein mwite Mmachinga naye yalimkuta kama haya ya Mogella.

Ingawaje ya Mmachinga yalikuwa mazito zaidi, aliamua kuitosa timu aliyoipenda na kujiunga na Simba.

Lakini leo hii Mmachinga ni Yanga wa kulia na hata Yanga wenyewe wanalijua hilo, ndio maana yuko kwenye benchi la ufundi la timu hiyo.

Kesi ya Mzinga Mambo, Mmachinga, Mogella na hata Ibrahim Ajibu Migomba zinaweza kufanana sana.

Mwingine kwenye mkondo huu ni Athumani Iddy ‘Chuji’ ugomvi mzito ndani ya Msimbazi ulimfanya kuhamia Yanga, alisema ni heri akauze ndimu kuliko kubaki Simba.

Kipa mahiri, Athuman Mambosasa, mwaka 1975 alihama Simba baada ya kuudhiwa na uongozi na kujiunga na Yanga. Lakini akakuta watu wanahama na kujiunga na Nyota Africa na baadaye Pan Africa, alienda nao ila baadaye alirudi Simba.

Chuji anaingia katika rekodi ya wachezaji walirudi tena kuzitimikia timu zao, alirudi Simba.

WAPO WENGINE WA MASLAHI

Wapo wachezaji wengine waliondoka kwasababu ya maslahi ya kufuata fedha.

Pia, Captain Morgan anaweza kuingia pia kwenye hili ambalo Juma Kaseja naye anaingia moja kwa moja.

Bernard Morisson ameweza kuondoka Yanga mwaka 2021na kujiunga na Simba na kama haitoshi mwaka 2022 akarudi tena Yanga.

Mtwa Kihwelo alijiunga na Simba kwa ajili ya maslahi, moyo wake na mapenzi yake yalikuwa Jangwani kama ilivyokuwa kwa Athuman Abdallah ‘China‘.

Pia, yumo mwinga mahiri, Mrisho Ngassa ‘Uncle‘ aliyeanzia Yanga kisha akaibukia Simba baada ya kuibua mzozo na klabu iliyomnunua, Azam kabla ya kurudi tena Jangwani.

Ngassa alipokuwa Simba, alipofunga goli alikuwa akishangilia kwa kuonyesha ishara ya nyoka aina ya cobra alikuwa akionyesha ishara ambao wengi hawakuielewa Nadhani unajua nyoka ni ‘mdudu’ wa aina gani.

Beki Kelvin Yondani aliwahi kuwaonyesha mashabiki wa Simba alama ya fedha wakati walipokuwa wakimzomea Ndio alitoka Simba kwenda Yanga kwa sababu ya maslahi.

Kwenye kundi hili pia yupo fundi mwingine wa mpira Haruna Niyonzima ‘Fabrigas’ alitoka Yanga kwenda Simba akamalizia mpira, Yanga.

HAWA HAPA WALE WA MAPENZI

Fundi wa Mpira, Method Mogella aliihama Simba na kujiunga na Yanga kutokana na kuwa na mapenzi na timu hiyo ya Jangwani.

Ni kama alivyofanya Ezekiel Grayson ‘Jujuman’ alihama Yanga mwaka 1977 na kutua katika timu ya moyoni mwake, Simba akitokea Yanga baada ya kukosea njia.

Hilo pia lilitokea kwa Said Maulid ‘SMG’ na Yusuf Ismail ‘Bana’ hawa walilazimisha uhamisho kutoka Simba kwenda kwenye mapenzi yao, Yanga.

Kiungo wa Mpira, Shaaban Ramadhani alipelekwa kwenda kuisaidia Yanga mwaka 1998 pamoja na Alphonce Modest na Monja Liseki wakitokea Simba, lakini kwa sababu mapenzi yake yalikuwa Jangwani, Shabaan hakurudi tena Msimbazi.

Mwingine ni Thomas Kipese ‘Uncle Thom’ alikuwa na mapenzi na Simba lakini alianza kuichezea Yanga na akaifunga Simba. Soka lake alilimalizia Msimbazi.

LISTI NDEFU SANA

Kuna wachezaji wengine wengi ambao wamecheza sehemu zote mbili, hawa hapa ni baadhi yao.
Said Mwamba ‘Kizota’, Akida Makunda, Ally Yusuf ‘Tigana’, Hamis Thobias ‘Gaga’, Willy Martin ‘Gari Kubwa’, Abubakar Kombo, Godwin Aswile ‘Scania’ na Suleiman Mathew Luwongo.

Wengine ni Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’, Steven Nemes, Doyi Moke, Emmanuel Okwi, Edibily Lunyamila, Said Mohammed ‘Nduda’, Nsa Job, Haruna Moshi ‘Boban’, Yew Berko, Ally Mustafa Barthez, Deo Munishi ‘Dida’, Rashid Gumbo, Nico Bambaga, Omar Hussein ‘Keegan’ na Moses Odhiambo.

Katika orodha hiyo wapo mastaa kibao, lakini huwezi kuwasahau makocha waliowahi kuzinoa timu hizo akiwamo Joel Bendera, Syllersaid Mziray ‘Super Coach’ na Tauzany Nzoysaba.

SOMA NA HII  KUMBE! UWEZO WA KABWILI NI MKUBWA KULIKO KIPYA MPYA