Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa nchini Nigeria Rivers United, Stanley Eguma, amekiri kuifuatilia Yanga SC ilipokuwa ikicheza dhidi ya Simba SC juzi Jumapili (April 16), katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga SC inayoongoza Msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa, ilikubali kupoteza mchezo huo kwa kufungwa 2-0, mabao ya Simba SC yakifungwa na Beki kutoka DR Congo Henock Inonga na Mshambuliaji wa Tanzania Kibu Denis.
Kocha Eguma amesema matokeo ya mchezo huo yatawasaidia kuwavusha katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kwa kuwa walitumia muda mzuri kufuatilia udhaifu na ubora wa kikosi cha Yanga.
Kocha Eguma amesema mchezo huo umeweza kutoa muelekeo wa matokeo yao katika mchezo wao wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ambao wanahitaji kupata matokeo ya ushindi kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Dar es salaam.
“Nimeweza kupata nafasi ya kuangalia mchezo wao, Yanga siyo wa baya isipokuwa walizidiwa katika mbinu hasa kipindi cha kwanza, kipindi cha pili walikuwa bora katika kutengeneza nafasi lakini hawakuweza kufanikiwa kupata matokeo mazuri.
“Matokeo waliyoyapata nadhani kwa upande wetu ni mazuri kwa sababu yameweza kunisaidia kupata mapungufu yao ambayo naamini nitaweza kuyatumia ili kuhakikisha napata matokeo makubwa hapa kwetu kabla ya kuja Tanzania kwa sababu malengo yetu ni kuona tunaenda nusu fainali,” amesema Eguma.
Rivers United itaanzia nyumbani Nigeria kucheza dhidi ya Young Africans April 23, kisha itaelekea jijini Dar es salaam-Tanzania kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili, April 30