YANGA SC imeeleza sababu ya winga wake Bernard Morrison ‘BM33’ kutotumika kwenye mchezo wa kwanza robo fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya Rivers United uliopigwa kwenye Uwanja wa Godswill Akpabi nchini Nigeria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Yanga SC kupitia kwa Kocha msaidizi Cedric Kaze amefichua kuwa sababu iliyofanya benchi la ufundi kutomtumia winga Morrison kwenye mchezo huo ni kupata majeraha.
“Morrison alipata shida kidogo ya msuli kwenye mazoezi ya mwisho hapa Nigeria, kama benchi la ufundi tukaona sio sawa kumlazimisha acheze kwani anaweza kuumia zaidi” amesema Kaze na kuongeza;
“Tuliamua kumuondoa kwenye mpango wa mechi ili kumpa nafasi ya kuwa sawa kabisa kwaajili ya mechi zinazofuata,”
Nyota huyo ambaye amerudi Yanga SC msimu huu akitokea Simba amekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali, Kaze amesema bado watamtumia kwenye mechi zijazo.
“Kila mtu anajua ubora wa Morrison akuiwa na mpira na kwa mechi zilizobaki tunahitaji sana awe kwenye utimamu wake kwa asilimia 100 ili awe na faida kwa timu” amesema Kaze
Yanga ilianza vyema hatua ya robo fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Rivers United katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Godswill Akpabio.
Timu hizi zinakutana tena kumalizia mkondo wa pili Jumapili hii katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.