Home Habari za michezo VITA HII KUBWA YAIBUKA…BALEKE ACHARUKA ILE MBAYA…SIMBA KULIPA KISASI

VITA HII KUBWA YAIBUKA…BALEKE ACHARUKA ILE MBAYA…SIMBA KULIPA KISASI

VITA HII KUBWA YAIBUKA...BALEKE ACHARUKA ILE MBAYA...SIMBA KULIPA KISASI

WAKATI Ihefu ikiwakaribisha leo Simba, mechi hiyo itakuwa ni vita kati ya mastaa wawili, Yacouba Sogne na Jean Baleke ambao wamekuwa moto kwa timu hizo huku rekodi na visasi vikitawala kwenye mpambano huo.

Iko hivi. Katika mechi 12 nyuma ilizocheza Simba, straika Baleke amefunga jumla ya mabao 11 ikiwamo hatitriki mbili za ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar na kombe la shirikisho (ASFC) mbele ya Ihefu.

Staa huyo alianza kuwaka kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji alipoifungia Simba bao la ushindi (1-0), akafunga tena dhidi ya Singida BS (3-1), akatupia tena moja dhidi ya African Sports kombe la shirikisho (4-0) na akafunga matatu dhidi ya Mtibwa (3-0).

Nyota huyo raia wa DR Congo aliendelea kutakata dhidi ya Horoya akifunga bao moja wakati Simba ikishinda 7-0, akatupia tena moja wakifa ugenini 3-1 dhidi ya Raja Casablanca na juzi akaweka matatu dhidi ya Ihefu kombe la FA, Simba ikishinda 5-1.

Hata hivyo naye straika wa Ihefu, Yacouba amekuwa na kiwango bora haswa anapokuwa uwanja wa Highland Estate kwani katika michezo minne amefunga mabao mawili na asisti mbili na kuwa tegemeo kikosini.

Timu hizo zinakutana tena ikiwa ni baada ya siku tatu tu tangu mara ya mwisho zilipokutana katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya robo fainali na Simba kushinda 5-1.

Kuhusu rekodi, Ihefu inajivunia matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu kwani katika mechi tano za nyuma haijapoteza wakiwachapa pia vigogo wa soka, Yanga 2-1 na Azam FC 1-0 na leo ina kazi nyingine kubwa dhidi ya Wekundu hao.

Hata hivyo vijana hao wa Mbogo maji, katika michezo mitano kukutana na Simba haijawahi kushinda wala kutoa sare wakichezea vipigo na kuruhusu mabao 12 kwa mawili tu.

Mchezo huo unazifanya timu hizo kucheza kwa rekodi au kisasi ambapo Ihefu inasaka ushindi wa kwanza dhidi ya wapinzani hao, huku Simba ikihitaji kuendeleza heshima na ubabe.

Ihefu imeonyesha upinzani mkali hasa inapokuwa kwenye uwanja wa Highland Estate na kuthibitisha hilo katika michezo yake minane iliyopita imeshinda sita, sare mmoja na kupoteza pia mmoja tu.

Mchezo iliopoteza ni ule wa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania Novemba 17, mwaka jana hii ikiwa na maana kwamba tangu mwaka huu umeanza miamba hiyo ya Mbarali haijapoteza mechi.

Tangu mara ya mwisho Ihefu ifungwe na Yanga kwa bao 1-0 Januari 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa imecheza michezo mitano bila ya kupoteza ambapo kati yake imeshinda minne na sare mmoja.

Kwa upande wa Simba nao inaingia katika michezo huu ikiwa na rekodi nzuri kwani kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu iliyopita imeshinda minne na sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC Februari 21, mwaka huu.

Kocha msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema baada ya kupoteza mchezo wao wa kombe la shirikisho na kutolewa kwenye michuano hiyo wanaenda kuwasubiri wapinzani hao nyumbani.

β€œTulihitaji kufika mbali lakini haikuwezekana ndio hali ya mpira ila niwapongeze vijana walipambana na sasa tunaenda nyumbani kwenye mechi ya ligi kuu kuhakikisha tunashinda,” alisema Katwila.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema matokeo waliyoyapata baina ya wapinzani wao katika mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho la Azam yamewaongezea morali.

“Timu ni ile ile ila tofauti ni mashindano tu, tunatambua hauwezi kuwa mchezo mwepesi kama ule uliopita hivyo tutacheza kwa kuwaheshimu lakini tukiishi katika malengo ya kupata pointi tatu.”

SOMA NA HII  ISHU YA BARBARA KUPIGWA VITA...KIGOGO SIMBA AIBUKA NA KUANIKA MAPYA..." HAFANYI KWA MAAMUZI YAKE"....