Home Habari za michezo SAMATTA AACHIWA MSALA GENK…AKISHINDWA HAPO NDIO BASI TENA…

SAMATTA AACHIWA MSALA GENK…AKISHINDWA HAPO NDIO BASI TENA…

Habari za Michezo

MCHECHETO kwa mashabiki wa KRC Genk huko Ubelgiji ni mkubwa huku presha ikipanda na kushuka, macho yao yanasubiri kuona chama lao lililoongoza msimamo Jupiler Pro kwa kipindi kirefu likitwaa ubingwa huo kwa mara wa tano.

Ni jino kwa jino, KRC Genk ambayo anaichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta imetinga hatua ya mchujo ya kuwania ubingwa huo ambayo ilianza juzi, Jumapili huku wakibeba matumaini ya mashabiki wao.

Kawaida huko Ubelgiji mara baada ya kila timu kucheza michezo yake yote, wababe wanne ambao wamemaliza nafasi za juu ‘top four’ hupambanishwa huku pointi zao za awali zikigawanywa mara mbili kuwania ubingwa huo na hapo ndipo utamu ulipo.

Samatta ambaye anaonekana kurejea kwenye makali yake huku akifunga mabao matano kwenye michezo saba iliyopita ni kati ya wachezaji wa chama hilo ambao wamebeba matumaini kwenye vita ya ubingwa ambayo mbali na KRC Genk timu nyingine ni Union SG, Antwerp na Club Brugge.

Kabla ya pazia kufunguliwa juzi, Jumapili ambapo KRC Genk walicheza dhidi ya Club Brugge, chama la Samatta lilikuwa likiongoza msimamo wa hatua hiyo ikiwa na pointi 38 sawa na Union SG huku Antwerp ikishinda nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36, wanaoshika nafasi ya mwisho ni Brugge (30).

Kocha wa KRC Genk, Wouter Vrancken yupo na matumaini ya kutwaa ubingwa huo, “Tunatakiwa kujitoa hii ni hatua muhimu ambayo kila mmoja wetu karibu kwenye kila msimu amekuwa akitamani kucheza, tutapambana kwa ajili ya timu na mashabiki zetu ambao wamekuwa nyuma yetu.”

“Nimekuwa nikiongea na wachezaji wangu kwa sababu najua kwa pamoja tunaweza kufanikisha hili, namna pekee ya kumaliza vizuri msimu ni kuwapa zawadi mashabiki wetu ambayo si nyingine bali ni kutwaa ubingwa.”

Katika ligi ya kawaida kabla ya mchujo wa ubingwa, KRC Genk ilikuwa na pointi 75 sawa na Union SG, wababe hao walikusanya pointi hizo baada ya kushinda michezo 23, walipoteza na kutoka sare mara sita.

Takwimu zinaonyesha KRC Genk ndio timu yenye safu kali zaidi ya ushambuliaji kwani hakuna timu iliyofunga mabao mengi zaidi kuliko wao (78), ni wazi hilo litakuwa imani Vrancken ya kufanya vizuri.

Vrancken anafaida ya safu yake ya ushambuliaji kuwa na Samatta ambaye ni mzoefu na ameonakana kushirikiana vyema na damu changa kama vile Mike Tresor, Joseph Paintsil na Bilal El Khannouss

Samatta bado yupo midomoni mwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na kile ambacho alifanya msimu wa 2018–19 ambao aliweka kambani mabao 32 kwenye michuano yote na kuliwezesha chama hilo kutwaa ubingwa huo kabla ya kujiunga na Aston Villa ya Ligi Kuu England msimu uliofuata.

Akiongelea mwenendo wa KRC Genk, Jeff Megan ambaye rafiki wa Samatta anayeishi nchini humo, alisema licha ya ushindani uliopo inawezekana kwa wababe hao kutwaa ubingwa huo, “Naona kabisa Genk ikichukua tena ubingwa,”

“Siwezi kuficha wamekuwa na msimu mzuri, wamekuuwa kwenye kiwango bora kwa muda mrefu, zaidi, kikosi chao kinaundwa na wachezaji wengi vijana hivyo naamini wananjaa ya kuchukua ubingwa huo.”

Jeff ambaye ni raia wa Tanzania anayeishi Ubelgiji, aliongeza kwa kumtakia kila la kheri mshikaji wake, Samatta kwenye hatua hii huku akiamini anaweza kuendelea kufanya makubwa akiwa na chama hilo.

“Hapa ni nyumbani (Genk) anajua namna gani anatakiwa kufanya na kwa bahati nzuri sote tumeona vile ambavyo yupo kwenye kiwango chake, sina shaka kabisa na uwezo wake kwenye kufunga, mchezaji mkubwa huwepo kwa matukio makubwa.”

Kutokana na kile ambacho Samatta anakionyesha kwa sasa akiwa na Genk ni wazi mabosi wa chama hilo watataka kumsajili jumla baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika mwishoni mwa msimu, ikumbukwe nahodha huyo wa Taifa Stars ni mchezaji wa miamba ya soka la Uturuki, Fenerbahce.

Samatta anaweza kukubali ofa ya Genk kutokana na chama hilo kuwa na nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

MAFANIKIO YA GENK
Jupiler Pro:
Ubingwa: 1998–99, 2001–02, 2010–11, 2018–19
Nafasi ya Pili: 1997–98, 2006–07, 2020–21

Daraja la Kwanza:
Ubingwa: 1975–76
Nafasi ya Pili: 1986–87, 1995–96

Kombe la Ligi:
Ubingwa: 1997–98, 1999–2000, 2008–09, 2012–13, 2020–21
Nafasi ya Pili: 2017–18

Super Cup:
Ubingwa: 2011, 2019
Nafasi ya Pili: 1998, 1999, 2000, 2002, 2009, 2013, 2021

SOMA NA HII  WAKATI MAMBO YAKIZIDI KUNOGA SIMBA....LWANGA..MUGALU WAMTIBUA PABLO....UONGOZI WATOA TAMKO...