YANGA sasa imedhamiria kucheza fainali ya kombe la Shirikisho Afrika, ambapo kesho majira ya saa 10 jioni wanashuka dimbani kusaka ushundi mnono katika mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya Marumo Gallants F.C.
Mechi hiyo ni muhimu kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi kuhitaji matokeo mazuri kwa kumaliza mechi hiyo uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kwa kutafuta ushindi wa mabao mengi na kuzuia Marumo Gallants kutopata bao.
Kikosi cha Yanga kimejiweka sawa hasa safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Fiston Mayele na Kennedy Musonda wanatarajiwa kutumia vizuri nafasi watakazotengeneza kufikia malengo yao ya kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao.
Wakati Yanga ikimtegemea Mayele katika ufungaji, kocha Mkuu wa Marumo Gallants FC, Dylan Kerr amekiri ubora wa safu ya ushambuliaji ya wapinzani wao kwa kuhakikisha wanawachunga nyota wote hatari akiwemo mshambuliaji , Stephane Aziz Ki na wengine.
Kuelekea mchezo huo Kocha Nabi amesema maandalizi yameenda, kama walivyopanga na wamewasoma wapinzani wao baada ya kuona baadhi ya michezo waliyocheza ya ligi yao na kimataifa.
Amesema wachezaji wako na hali ya kupambana na kuwa tayari kwa ajili ya kutafuta ushindi mkubwa dhidi ya wapinzani wao Marumo Gallants FC,
“Niwapongeze Marumo Gallants, timu nzuri licha ya kwenye ligi yao hawafanyi vizuri lakini mashindano haya wamefanya Vizuri na wamewatoa timu kubwa hapa Afrika Pyramids.
Marumo Gallants F.C kufika hapa sio kwa bahati mbaya timu ambazo tunatakiwa kucheza nao kwa umakini mkubwa kwa sababu ya jinsi ya matokeo yao ya mechi za kimataifa kila mechi wamefanikiwa kufunga,”.
Mechi ni ngumu kwa sababu wapinzani wao ni timu bora, hawataibeza na sio kuifunga kwa urahisi, hatuwezi kumaliza kwa mkondo mmoja wa nyumbani na wa pili utakuwa ugenini.
“Hii timu unatakiwa kucheza nao kwa akili ya hali ya juu kwa kucheza kwa umakini na sio mechi ya kushambulia shambulia tu kwa sababu huwezi jua mpinzani wako anaingia kwa mfumo gani au mbinu ipi,” alisema Nabi.
Aidha katika hatua nyingine, Nabi amesema kuwa beki wake Shaban Djuma hakufanya mazoezi na timu kwa sababu ya kuungua mafua lakini waliobaki wote wako vizuri kwa ajili ya mchezo huo.
Nabi aliwashukuru mashabiki wa Yanga kwa sapoti yao na kuwaomba mechi ya kesho kuwa pamoja katika dakika zote 90.
“Mashabiki wanatakiwa kuiga mbele, hata kama mchezaji wetu akipoteza pasi basi asipigiewe kelele kwa sababu hii mechi sio rahisi kama wanavyofikiri tutapambana na kupata matokeo mazuri,” alisema Nabi.
Kwa upande wa mwakilishi wa wachezaji wa Yanga, Metacha Mnata alisema maandalizi yamekamilika na wanajiandaa kuhakikisha wanaweka historia kwa Tanzania kuvuka hatua ya nusu na kuwa sehemu ya historia ya kucheza fainali.
“Hii ni mechi ngumu na tunatakiwa kupata matokeo mazuri na tunahitaji kupata matokeo mazuri uwanja wa nyumbani ili mechi ijayo ya marudiano tusicheze kwa presha kubwa,” alisema Metacha.
Kocha Msaidizi Marumo Gallants FC, Raymond Mdaka alisema wamefanya maandalizi kulingana na mechi iliyopo mbele yao kuelekea mechi ya kesho wamejiandaa na wako tayari kwa kuwakabili Yanga.
“Hatuwezi kuwaongelea sana wapinzani wetu kwa sababu unaweza kusahau, ila tumefanya maandalizi mazuri dhidi ya Yanga kupata matokeo mazuri ugenini,” alisema Kocha huyo.
Nahodha wa Marumo Gallants FC,Washington Arubi alisema wamejianda na wanafahamu Yanga ni timu kubwa na watacheza kwa tahadhari kubwa.
“Hatutaangalia mchezaji mmoja labda Mayele (Fiston) au nani, bali tumekuja kucheza na Yanga, tumekuja kucheza mpira na sio kuangalia au kuwachunga baadhi ya wachezaji bali tunahitaji kufanya vizuri, ugenini,” alisema Arubi.