Klabu ya Yanga imekata rufaa hivi punde kupinga adhabu ambayo walipewa na Shirikisho la Mpira Afrika CAF hivi karibuni.
Yanga ilipigwa faini ya dola 35,000 (zaidi ya Tsh milioni 80) na CAF kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na makosa ya kuwasha mafataki na moshi pamoja na kuweka vitu vinavyodhaniwa kuwa ni kemikali na kuiba pesa kiasi cha dola 5,200 kwenye gari la Rivers United wakiwa mazoezini.
Klabu ya Yanga imewasilisha barua CAF kupinga adhabu waliyopewa kuwa hakuna fataki zilizopigwa katika dimba la Mkapa kwenye mchezo dhidi ya Rivers United.
Klabu imeandika kuwa haiusiki na pesa zilizoibiwa ndani ya bus la wageni wao ambao walikuwa ni Rivers United, kama CAF walivyodai kwenye barua.
Aidha, jana Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe alisema; ” Adhabu tuliopigwa sio uvumi, ni taarifa rasmi ya CAF na Yanga tumeiona tumepigwa adhabu ya faini dola 35,000.
“Jambo la kwanza ni mashabiki kuwasha mafataki na moshi uwanjani kisha madai ya basi la Rivers kuvunjwa na kuibiwa kiasi cha dola 5,200, harufu mbaya na sumu.
“Baada ya kuipokea taarifa hiyo wala hatukupaniki, tuna uongozi bora wenye akili kuliko kawaida, tulipoiangalia tukasema leo management itakaa na kujadili namna ya kuliendea suala hili.
“Ukishapigwa faini kama hivi kuna nafasi ya kukata rufaa kama unaona hujatendewa haki. Sisi sio wa kwanza kupiga mafataki, wapo masters wa hayo mambo, waarabu tumeona wamefanya na hawajapigwa faini, sisi tunaomba mtu asitutoeaa relini, tupo imara na tunafokasi na mchezo,” alisema Kamwe.