Beki wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara Yanga, Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ (24) licha ya jina lake kupata umaarufu haumfanyi atoke kwenye misingi ya dini ya Kiislamu kwani anajifunza kuishi vyema zaidi ya alivyokuwa awali.
Bacca ni mchezaji mtulivu anajipambanua ajibu jambo gani na aache lipi wakati wa mahojiano na Mwanaspoti yaliyofanyika hivi karibuni Dar es Salaam akifunguka mengi ya fani yake.
Haijawa ghafla kuibuka na kuwa kipenzi cha mashabiki, lakini beki huyo alikubali kuumia wakati anasota kupata namba kwenye kikosi cha kwanza Jangwani akijipa muda akiamini ingetokea siku Watanzania kujua kipaji chake.
Nyota huyo anajua kuyapambania maisha akisimulia namna ambavyo mila za Kizanzibari, wazazi wanavyokata huduma kwa vijana wa kiume ili kuwafunza kujitegemea, ilipofika wakati huo alipiga mishe za biashara hadi kufanya kibarua cha kumenya viazi maarufu chipsi.
“Zanzibar kuna umri ukifika, wazazi wanaanza kupunguza huduma kama chai, chakula cha mchana kisha watataka ujitegemee kila kitu. Ilipofika hatua hiyo nilitafuta muuza chipsi nikawa namenya viazi kwa siku nilikuwa napata Sh3,000 na kupewa chipsi za kula.
“Nilifanya mishe mbalimbali na mimi nikaanza kuonyesha umwamba wa kumpa mama Sh5,000 ili aamini nimekua na kumuondoa hofu ya kuwategemea muda wote,” anasema.
Jambo lingine lililokuwa linamfanya apambane anasema baba yake alikuwa anapenda kumnunulia viatu vya moka, hivyo alikuwa hapendi akawa anapambana kujitafutia pesa za kununua raba za kisasa.
“Hizo moka zilizochongoka mbele sipendi kabisa hadi leo, labda itokee Yanga watake tuvae kwenye sherehe za ubingwa nitakuwa sina namna na nikavaa siwezi kuvirudia tena,” anasema.
UVUMILIVU WAKE
Kauli za makocha wa Yanga, Nasreddine Nabi na Msaidizi Cedrick Kaze, walipomwambia ni fundi ukifika muda wa kucheza Watanzania wataona kipaji chake, ilimpa moyo wa kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii bila kujali atapata nafasi lini.
“Kocha Nabi mara kwa mara alikuwa ananiambia nina kipaji kikubwa sana, nakumbuka mechi yangu ya kwanza kucheza ni dhidi ya KMC, alinifuata kocha Kaze akaniambia kesho unaanza tunatarajia kuona utulivu wako, kisha nikaingia ndani na kutafakari na kumuomba Mungu anisimamie,” anasema.
Nje na makocha, wazazi wake ambao wote ni askari wa Jeshi la Magereza baba yake Abdallah Hamad Bakari na mama yake Mwajina Makame, walimwambia avumilie, aongezee bidii, ajifunze kila wakati na kuwasikiliza makocha kwake.
“Kwa mara ya kwanza wakati najiunga Yanga baba aliniambia, nizingatie uvumilivu na nidhamu, hilo lilikuwa linaishi sana moyoni mwangu, ila mama yangu muda mwingi anapiga simu kuniuliza afya, utamsikia upo salama si unajua kina mama na watoto wao,”anasema.
USHINDANI WA NAMBA
Baada ya kocha kuanza kumwamini kikosi cha kwanza anakiri bado ushindani ni mkali, unaomfanya asivimbe kichwa badala yake unamtengeneza ubora wa kiwango chake na kutamani kufanya makubwa kila anapopata nafasi ya kucheza.
“Bado nina safari ndefu, ndani ya kikosi cha Yanga wapo mastaa waliofanya makubwa sana, hivyo napaswa kuongeza bidii ili kuisaidia timu na kiwango changu kizidi kukua siku hadi siku,”anasema.
Anakiri yapo mambo anayojifunza kwa mabeki wengine, ili kumuongezea ubunifu zaidi, kubwa zaidi anapendelea kurudia mechi alizocheza kujua makosa aliyoyafanya kisha anayafanyia kazi.
“Napata muda wa kuangalia mechi za marudio, nikiona yapo maeneo sikufanya vizuri naenda kuyarekebisha mazoezini, niliyofanya vizuri naboresha zaidi,” anasema.
Pia anapenda kuangalia mastaa mbalimbali wa Ulaya wanaocheza nafasi yake, ili kupata ufundi zaidi, huku miongoni mwa mabeki wanaocheza Ligi Kuu Bara anamtaja Yakubu Mohamed anamuona fundi sana.
NINJA, FEI WALIMSAIDIA
Anasema kwa mara ya kwanza wakati anatua kambini wachezaji ambao walikuwa wanamsaidia kumwelekeza mazingira ya timu ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ walikuwa wanamsisitiza kutunza blandi ya Yanga popote anapokuwepo.
“Maisha ya timu niliyotoka na Yanga ni vitu viwili tofauti, ingawa maisha yangu hayakuwa ya kujisahau, lakini Ninja na Fei waliniambia nilinde sana blandi ya Yanga, kwani chochote nitakachokifanya watasema mchezaji wa Yanga, hivyo walinipa mwanga mkubwa pia wakinipa moyo nisikate tamaa,” anasema.
DIARRA ASHANGAZWA NAYE
Aina ya uchezaji wake unamchanganya kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra kwani Bacca anatumia miguu miwili kucheza; “Kuna siku Diarra aliniita akaniuliza dogo mguu gani ni halisi kuutumia zaidi.
“Nikacheka nikamwambia halisi ni wa kulia, akauliza tena mbona naona yote inafanya kazi sawa, huwa naangalia unachokifanya na lazima nifuatilie kwani tunasaidiana kazi, mwisho akasema utafika mbali, anapenda ninachofanya kwa sababu anaona idadi ya mabeki wanaotumia miguu miwili ni wachache.”
Mchezaji mwingine aliyependa aina ya uchezaji wake ni aliyewahi kuichezea klabu hiyo, Chicco Ushindi; “Ushindi aliwahi kuniambia utafika mbali, usiangalie leo, ipiganie kesho maneno hayo yakawa yananipa moyo sana.”
Anazungumzia usajili wake kuwa anakumbuka KMKM ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga, kuna shabiki wa Mlandege anamtaja kwa jina moja analojulikana Mbamba, kwamba aliiona kipande cha video yupo na rais wa Yanga, Injinia Hersi Said akimwambia msajili dogo anajua na hawatajutia kuwepo kwenye kikosi chao.
“Huyo alitia nguvu kwa Injinia kunifuatilia zaidi hadi usajili wangu ulipokamilika, maana siku hiyo nilifuatwa na mashabiki wengi wakiniambia nimecheza vizuri wanatamani kuniona mbali,” anasema.
BADO NI ASKARI
Ingawa hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusiana na ajira yake ya askari wa KMKM, msichokijua mkataba wowote anaoingia na klabu waajiri wake hao wanahusika.
“Nawashukuru sana waajiri wangu wa KMKM kukubali kipaji changu kijulikane kwa ukubwa, lakini bado naheshimu mipaka ya kazi yangu, mkataba nikitaka kuongeza lazima wajulishwe, hiyo ni taasisi siwezi kuzungumza zaidi ya hapo na hapa naona navuka mipaka ni vile unavyong’ang’ania kujua hilo,”anasema.
Anazungumzia picha inayotembea mitandaoni inayomuonyesha kavaa nguo za kiaskari hata yeye anajiuliza hajui wameipataje; “Kiukweli hata mimi nilishangazwa kuiona mtandaoni, kwani ni picha ambazo si rahisi kuniona naziposti.”
MAISHA YA UMARUFU
Anasema hana mambo mengi yakumfanya akumbane na matukio nje ya kazi yake, ila changamoto inakuja anapoposti picha zake kwenye mtandao wa kijamii (Instagram), anakutana na ujumbe mbalimbali DM, ambazo zipo pande mbili za mashabiki anazozifurahia na mbaya.
“Nawapenda mashabiki wa Yanga sana, ambao mara zote wananipa nguvu ya kupambania kutokana na maneno ya kunijenga wanayoniambia, ila nashangawazwa na watu wanaonitumia ujumbe DM usiofaa, mimi ni Muislamu siwezi kuyafanya watakayo, iwe wanawake ama wanaume ambao hawataki kukaa kwenye nafasi zao, nawaomba tu wamuogope Mwenyenzi Mungu.
“Kuna wakati mwingine nazisoma, najiuliza hivi binadamu mbona wanakosa hofu ya Mungu, mfano wanaume wanapataje nguvu ya kunitumia ujumbe usio sahihi, natumia chombo hiki kuwaomba kwamba tupunguze maasi Mungu hapendezwi nayo.
“Pia niwaahidi mashabiki, vipenzi wa Yanga nitapambana siwezi kulewa sifa, najua wanapenda nifanye vizuri siyo nje ya hapo.”
TUKIO BAYA
2011 akiwa darasa la sita alipoteza rafiki yake wa karibu Hamad, alikuwa miongoni mwa waliozama na meli ya MV Spice, anasimulia kwa uchungu alivyopokea taarifa hiyo.
“Mungu kama hajakupangia kufa basi utaishi, asilimia kubwa wanafunzi tulikuwa tukifunga shule tulikuwa tunapanda meli hiyo kwenda Ugunja, wazazi wangu hawakuwa tayari nisafiri, basi nikawa na huzuni kuona marafiki zangu wanaondoka mimi nabaki.
“Mimi ni Mpemba kwetu ni Pemba, nilikuwa chumbani nikawa nasikia kelele za watu ambazo zilifanya nikae kitandani badala ya kulala, baba akawa anafungua milango, moyo wangu ukawa mzito sana, baada ya muda ndipo nikasikia taarifa za kifo cha rafiki yangu kuanzia shule hadi mtaani, pia walikufa wanafunzi wengi niliyokuwa nasoma nao,” anaema.
SOKA LA ZANZIBAR
Anasema soka la Zanzibar kuna misingi ambayo mchezaji anapaswa kuanza nayo, anaitaja ni Juvanali ni vijana kuanzia miaka 10 hadi 11, Junior kuanzia miaka 11-13 na Central kuanzia miaka 13 hadi 18 ambayo Bacca ameipitia.
Anamtaja aliyeona kipaji chake akiwa nyumbani kwao Pemba, mkoa wa Wete ni Abdallah Mohamed ‘Ukocha’ kocha wa timu ya Young Stars inayoshiriki Ligi Daraja la pili.
“Nikiwa nacheza mtaani, kocha huyo ambaye ni kama kaka yangu, aliniambia una kipaji kikubwa njoo kwenye timu yangu alinisimamia hadi nilipopata timu za kuonekana zaidi,” anasema.
KIKOSI WANZANZIBARI WANAOCHEZA BARA
Kipa ni Isihaka Hakimu (Ruvu), Mohamed Othuman (Polisi Tz), Abdul Malki (Namungo), Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (Yanga), Abdallah Sebo (Azam FC), Mudathir Yahya (Yanga), Aban Kassim (Ruvu), Hassan Maulid (Mbeya City), Maabad Maulid (Coastal Union), Fei Toto (Yanga) na Ibrahim Mkoko (Namungo), Bacca amejiweka upande wa kocha.
“Zanzibar kuna vipaji vikubwa sana vya makocha na viungo, ila utofauti wa soka la Bara lina wadhamini wengi na sasa naona wana vituo vingi vya soka ambavyo miaka ya baadaye watakuwa na wachezaji tishio, kwa sasa hicho ndicho kikosi changu,” anasema.
MSIMU 2021/22
Bacca anasema msimu uliopita alicheza dakika 270 dhidi ya Mbeya City, Mtibwa Sugar na Polisi Tanzania na pamoja na hilo hakuwahi kukata tamaa na wenzake ambao walikuwa wanapata nafasi alikuwa anawahamasisha wapambane kupata matokeo ya ushindi.
“Yanga kwanza mengine yanafuata, mchezaji yoyote anapopata nafasi ni kuipigania timu na sasa tuna raha baada ya kunyakua taji hilo tena,” anasema.