Home Habari za michezo KISA MAFANIKO YA YANGA CAF…WAKUU WA MIKOA WANYUKANA UKUMBINI…UBISHI ULIANZA HIVI…

KISA MAFANIKO YA YANGA CAF…WAKUU WA MIKOA WANYUKANA UKUMBINI…UBISHI ULIANZA HIVI…

Habari za Yanga SC

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amekubali yaishe kwa kuitakia Yanga ushindi katika mchezo wake wa fainali ya kombe la shirikisho Afrika baada ya kubanwa na mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.

Wakuu hao leo waliuteka ukumbi kwa muda wakati wa kikao cha kujadili maandalizi ya sherehe za wakulima ‘Nanenane’ kilichofanyika jijini Mbeya kwa kuwashirikisha viongozi mbalimbali kutoka Nyanda za Juu Kusini.

Kanal Thomas ndiye alianza kuwasalimia washiriki wa kikao hicho akielezea kwa mafumbo mafanikio ya Simba kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika akiwapiga kijembe Yanga kuwa ni kama mwanafunzi aliyeshindwa akieleza kuwa ili kujua mwano ana akili lazima ashindane na shule 10 bora.

“Kama mwanao anashinda shule za St Kayumba utatambaje ana uwezo? Lazima umpeleke shule 10 bora kitaifa ili umpime akili zake nadhani waliosoma kule Quba mmeelewa” amesema Kanal Thomas na kuamsha shangwe kwa baadhi ya viongozi ukumbini humo.

Hata hivyo Kanal huyo wakati akifunga kikao hicho, aliiombea Yanga ushindi akiwahamasisha wananchi pia kuiunga mkono ili timu hiyo iweze kutwaa ubingwa wa michuano hiyo akieleza kuwa wamekuwa na mafanikio.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Homera ambaye ni shabiki lialia wa Yanga amesema kufungwa ni kufungwa haijalishi ni michuano gani akisema Tanzania nzima itaishangilia Yanga.

Ameongeza kuwa Yanga imekuwa na uwakilishi mzuri akibainisha kuwa kwa sasa ni jukumu la kila mmoja aliye na uzalendo kuiombea katika mchezo wake wa fainali dhidi ya USM Algers ili kuweza kutwaa ubingwa huo.

“Ninaamini timu zangu za Mkoa, Tanzania Prisons, Ihefu na Mbeya City hazishuki daraja, kwa sasa tunajiandaa kuona kombe la shirikisho Afrika linakuja Tanzania, hivyo tuungane na Rais Samia Suluhu kuiombea Yanga kushinda mechi ya fainali, Simba ilifungwa na Orlando Pirates huko lakini Wananchi tumeshinda kwenye ardhi hiyo” ametamba Homera akishangiliwa na baadhi ya washiriki wa kikao hicho.

Simba ilikuwa ikishiriki michuano ya klabu bingwa Afrika na kuishia hatua ya robo fainali, huku Yanga wao wakisubiri fainali ya kombe la shirikisho Afrika.

Yanga tayari ametwaa ubingwa wa ligi kuu, huku akisubiri pia mechi ya nusu fainali ya kombe la shirikisho (ASFC) dhidi ya Singida Big Stars ambapo Wekundu wameshaondoshwa dhidi ya Azam walipolala mabao 2-1.

SOMA NA HII  NABI AWAFUNGIA KAZI WANIGERIA..DITRAM NCHIMBI 'DUMA' APEWA KAZI MAALUMU