Rais wa Klabu ya Young Africans Injinia Hersi Said amesema msimamo wa klabu dhidi ya Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ bado upo vilevile na hautabadilika.
Young Africans na Feisal Salum wapo katika mgogoro wa kimkataba, huku kiungo huyo akishinikiza mkataba wake kuvunjwa kupitia TFF, lakini Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamuru suala hilo haliwezekani, zaidi ya pande hizo mbili kukaa mezani na kumalizana.
Akizungumza mapema jana Jumatano (Mei 24) kupitia Clouds FM Injinia Hersi Said amesema, Young Africans ni Taasisi na haiwezi kuwa na huruma katika suala hilo, zaidi ya kusimamia misingi iliyojiwekea.
Hivi karibuni Fei Toto alijitokeza mbele ya Watanzania na kuomba kuchangia jumla ya mili 56 za kwenda kufungua kesi CAS huku akiamini kuwa huko haki yake ya kuuvunja mkataba kati yake na Yanga itapatikana.
Hii inakuja baada ya hivi karibuni Kamati ya hadhi za wachezaji na sheria ya TFF kumtaka arudi kwenye klabu yake ya Yanga.
Msimamo wa Fei Toto ni kuwa kwa sasa hataki kuichezea Yanga kwa kile alichodai kuwa hathaminiwe kulingana na mchango wake ndani ya klabu hiyo.
Sakata la Fei toto na Yanga lilianza mwishoni mwa mwaka jana, ambapo mchezaji huyo alipotangaza kusitisha kuichezea klabu hiyo kwa kudai kuwa mshahara anaolipwa ni mdogo tofauti na wachezaji wakigeni ambao aliamini hawana uwezo kama wake.