Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU…..SIMBA ISIBEZWE KWA NUSU FAINAL YA YANGA CAF…

UKWELI MCHUNGU…..SIMBA ISIBEZWE KWA NUSU FAINAL YA YANGA CAF…

Habari za Simba SC

Yanga imefuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni mafanikio makubwa na historia kwa timu na nchi kwa ujumla. Huwa inatokea mara chache.

Hakuna mtu aliyeipa Yanga nafasi ya kufanya makubwa katika mashindano hayo msimu huu. Unajua kwanini? Nitakueleza.

Yanga haikuanza vizuri mashindano. Baada ya mechi mbili dhidi ya vibonde Zalan, hawakuwa na jipya mbele ya Al Hilal ya Sudan. Walipata sare Dar es Salaam kisha wakafungwa pale Khartoum. Wakaondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa.

Huku kwenye Shirikisho pia wakaanza kwa kuchechemea. Wakapata sare nyumbani dhidi ya Club Africain. Hivyo Yanga walifika hatua ya makundi katika nyakati ambazo watu waliamini kuwa haiwezekani tena.

Hata hivyo mambo yalibadilika Yanga walipofuzu hatua ya makundi. Wakaanza kucheza soka la kuvutia. Wakamaliza kama vinara wa Kundi ambalo lilikua na timu za TP Mazembe, US Monastir na Real Bamako. Ni mafanikio makubwa sana.

Ubabe wao dhidi ya Rivers United pale Nigeria ukawafikisha hatua ya nusu fainali. Ni rekodi kubwa sana kwa Yanga. Haikuwahi kufika hatua kama hiyo kwa miaka zaidi ya 40. Unaachaje kuwapa sifa zao?

Mafanikio makubwa zaidi kwa Yanga katika mashindano ya Afrika yalikuwa kufika hatua ya makundi. Walifika hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa mwaka 1998. Hata hivyo walimaliza mkiani.

Wakafika tena hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho mwaka 2017 na kumaliza mkiani mwa kundi tena. Ni TP Mazembe na MO Bejaia waliofanikiwa kusonga mbele.

Baada ya hapo wakarejea hatua ya Makundi tena mwaka 2018 ambapo pia walimaliza kwa aibu. Licha ya kundi lao kuwa na timu za Rayon Sports, Gor Mahia na USM Alger bado Yanga hawakuwa na jipya.

Hivyo baada ya muda mrefu Yanga imepata mafanikio makubwa CAF. Walisubiri kwa hamu na sasa wanafurahia. Inapendeza sana.

Hata hivyo mafanikio haya ya Yanga yasitufanye tusahau kile walichofanya Simba katika mashindano haya ya CAF kwa miaka ya karibuni.

Simba ilionyesha njia mwaka 2019 ilipofika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa. Ilikuwa imepita miaka 26 tangu timu ya Tanzania ifike hatua za juu zaidi kwenye mashindano ya Afrika.

Historia kubwa ilikuwa kwa Simba kufika Kombe la CAF mwaka 1993. Baada ya hapo hakukua na timu ya Tanzania iliyoweza kufika hatua za juu zaidi. Lakini unadhani kwa Simba kufika robo fainali mwaka 2019 ilikuwa jambo kubwa? Hapana.

Simba imefanya jambo kubwa kwa kuweza kufika robo fainali tatu katika miaka mitatu iliyopita. Si jambo jepesi hata kidogo.

Imefuzu robo fainali mbili za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho. Inasisimua sana.

Changamoto kubwa katika mashindano ya Afrika si kupata mafanikio ya msimu mmoja. Changamoto ni kurudia mafanikio yako kwa miaka na miaka. Hapa ndipo Simba walipofanikiwa.

Ni kweli Yanga mwaka huu wanaweza kufika hata fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini mbeleni wana mtihani mzito wa kurudia mafanikio yao. Hapa ndipo Simba wamefanikiwa zaidi.

Unapoweza kurudia mafanikio kila baada ya mwaka ni ishara kuwa umekuwa timu kubwa na siyo kwamba unabahatisha. Ndio njia wanayopitia Simba. Mwaka jana waliondoshwa kwenye Robo Fainali ya Shirikisho na Orlando Pirates kwa mikwaju ya penalti. Ndivyo ambavyo wameondoshwa na Wydad kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka huu.

Ni wazi kuwa Simba inazidi kupata uzoefu na kuimarika katika mashindano haya makubwa. Sitashangaa kuwaona wakifika nusu fainali mfululizo ndani ya miaka michache ijayo. Kumbuka kuwa uzoefu hauna mwalimu.

Hivyo wakati tunaendelea kufurahia mafanikio ya Yanga, tukumbuke kuwa wana mtihani mkubwa mbele ambao Simba alishafanikiwa kuuvuka. Wanatakiwa kuyafanya mafanikio yao kuwa kitu cha kawaida.

Wafuzu hatua ya makundi CAF mara kwa mara. Wafanye vizuri katika hatua ya makundi na kuweka rekodi. Bila hivyo, mafanikio ya mwaka huu yataonekana kama walibahatisha tu.

SOMA NA HII  VIDEO: SIMBA YAFUNGUKIA ISHU YA MECHI YA WATANI ZAO WA JADI