Home Habari za michezo WAKATI YANGA WAKITAMBA NA MZINZE ….MBRAZILI SIMBA AMSUBIRISHA MUSSA…MSIMAMO WAKE HUU HAPA…

WAKATI YANGA WAKITAMBA NA MZINZE ….MBRAZILI SIMBA AMSUBIRISHA MUSSA…MSIMAMO WAKE HUU HAPA…

Habari za Michezo

Simba hakuna kulala, baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuita mastaa wake kambini ikiwa ni muda mchache tangu awape mapumziko mafupi tangu ilipocheza na Ruvu Shooting na kuishusha daraja kwa kuichapa mabao 3-0, Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam.

Mbrazili huyo ameita wachezaji hao kambi ya mazoezi iliyopo Uwanja wa Mo Simba Arena ili kujiandaa na mechi mbili za kufungia msimu za Ligi Kuu Bara akisema anazitaka pointi zote sita.

Simba itamalizana na Polisi Tanzania na Coastal Union, huku ikiwa tayari imeshapoteza tumaini ya ubingwa baada ya Yanga kutetea kwa msimu wa pili mfululizo kabla ya ligi kufikia tamati kwa kufikisha pointi 74, wakati Wekundu hao hata ikishinda mechi hizo za mwisho itafikisha alama 73 tu.

Akizungumza Robertinho alisema licha ya mastaa hao kupewa mapumziko hayo ila aliwapa programu binafsi za kuzifanyia kazi kwa lengo la kutaka kuona wakirudi wakiwa wapo fiti ili kumaliza msimu kwa heshima licha ya kulikosa taji.

Hadi sasa Simba ndio timu pekee iliyopoteza mechi chache zaidi ikifungwa mara moja, lakini ikifunga mabao 66, ikiwa ni 10 zaidi na iliyonayo Yanga japo zinalingana kwa mabao ya kufungwa kila mmoja kuruhusu 15.

“Programu niliyowapa ni kuzingatia jinsi ya kuhimili miili yao kwa maana ya vyakula mbalimbali wanavyokula wakiwa nje ya kambi, lengo ni kuona hakuna mabadiliko pindi wanaporudi kwa sababu bado tuna michezo miwili ya kumalizia msimu ambayo nahitaji kuimaliza kwa heshima,” alisema.

Aidha Robertinho alisema amefarijika kuona mastaa wa timu hiyo wamerejea kwenye hali zuri za utimamu wa mwili huku akisisitiza licha ya kutopata taji lolote msimu huu ila amewataka kutobweteka na badala yake kuendelea kuonyesha kiwango kizuri ili kutoa imani kwa mashabiki zao msimu ujao.

“Kila mmoja wetu anatambua tulipokosea msimu huu ndio maana tumeanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao sasa licha ya changamoto ya yote ambayo tumepitia ila tunahitaji kuhakikisha tunashinda michezo yote miwili iliyobakia ingawa tunacheza na timu ambazo haziko sehemu salama,” alisema.

Kuhusu kiwango cha mshambuliaji wa timu hiyo, Mohamed Mussa tangu ajiunge nao Januari mwaka huu akitokea Malindi ya visiwani Zanzibar, Robertinho amewataka mashabiki kuendeleza imani kubwa kwa nyota huyo huku akiweka wazi sababu za kushindwa kutamba ni kutokana na ushindani wa namba uliopo.

“Mohamed ni mchezaji mzuri na kijana wenye shauku ya mafanikio isipokuwa kama unavyojua tulikuwa tuna presha kubwa ya matokeo hivyo isingekuwa rahisi kumtumia, pia majeraha ya mara kwa mara yalimfanya kushindwa hata kufanya mazoezi na wenzake ingawa kwa sasa amerudi vizuri,” alisema.

Mussa aliyeonyesha kiwango kizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu amefunga bao moja tu tangu ajiunge na Simba katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya African Sports katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 16 bora uliopigwa Machi 2, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

SOMA NA HII  WAKATI SIMBA WAKITAMBA KWA UBORA...YANGA WAIFUNIKA KWA JEZI BORA AFRIKA NZIMA...