Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema sababu kubwa ya kutomfanyia mabadiliko ya mara kwa mara nyota wa timu hiyo, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ ni kutokana na faida mbili alizonazo akiwa uwanjani.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Robertinho alisema kuna muda baadhi ya mashabiki wamekuwa wanapiga kelele kuhusu kufanyiwa mabadiliko kwake akionekana kama kachoka licha ya yeye kuendelea kumuamini.
“Saido ni mchezaji mzuri sana na ana faida mbili, anaweza kufunga na kusaidia upatikanaji wa mabao kwa watu wengine jambo ambalo sio kila mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufanya hivyo uwanjani,” alisema na kuongeza;
“Muda mwingine huwezi kufanya mabadiliko kwa presha ya mashabiki tu ni lazima uamini katika falsafa zako na kile mchezaji anachokionyesha, Saido na wengine wanafanya vizuri ndio maana wanapata nafasi pia ya kucheza.”
Asisti mbili alizozitoa juzi kwa Pape Sakho katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting unamfanya Saido kuhusika kwenye jumla ya mabao 22 ya Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa ndiye kinara kwa wachezaji wote.
Saido aliyeanza msimu huu na Geita Gold baada ya kuachana na Yanga Mei 30, mwaka jana amekuwa kwenye kiwango kizuri tangu ajiunge na Simba dirisha dogo la Januari mwaka huu licha ya baadhi yao kuubeza usajili wake.
Msimu huu nyota huyo amefunga mabao 10 na kuchangia 12 ambapo akiwa na Geita Gold alifunga manne na kusaidia sita ila tangu ajiunge na Wekundu wa Msimbazi raia huyo wa Burundi tayari amefunga sita na kuchangia sita.
Ubora wa Saido umemfanya nyota huyo kuivunja rekodi yake aliyoiweka msimu uliopita wakati akiichezea Yanga kwani katika michezo 18 aliyocheza alihusika kwenye mabao 10 ambapo alifunga saba na kuchangia matatu tu.