Katika mechi mbili iliyobakiza Simba kufunga msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union, licha ya kutopigania taji hilo, bado straika wa timu hiyo Jean Baleke amesema haiondoi thamani ya kiwango chao uwanjani.
Baleke alisema timu yake kutokuchukua mataji yoyote, siyo sababu ya kucheza chini ya kiwango badala yake, wanatakiwa kumaliza kwa kishindo kwa ajili ya kulinda heshima ya kazi yao na klabu.
“Kutokuchukua mataji haimanishi ni mwisho kwa mchezaji kucheza kwa kiwango kinachotakiwa, kazi yetu ni kama wanajeshi hatuwezi kunyosha mikono juu hadi tuone tumefika mwisho wa Ligi Kuu kabisa.
“Tulitamani sana kuona tunasherekea mataji mbalimbali lakini imeshindika, kikubwa ni kujipanga upya na tusimalize kinyonge michezo iliyosalia mbele yetu.”
Baleke anayemiliki mabao manane kwenye Ligi Kuu na manne Ligi ya Mabingwa Afrika, alisisitiza anaipenda kazi yake anapopata nafasi ya kucheza anatamani kufanya vizuri kila wakati, bila kujali mazingira ya aina yoyote kama wanavyocheza mechi za kumaliza msimu.
“Soka linachezwa sehemu ya wazi, kuna mashabiki ambao kwenye mazingira yoyote watatazama mechi, ndio maana nasema hatuna budi kucheza kwa viwango vya juu kwa heshima ya klabu na sisi bifasi,” alisema Baleke aliyesajiliwa Simba kupitia dirisha dogo.
Simba itacheza na Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya pili kutoka mwisho, hivyo ikitokea ikashinda mechi zake mbili na timu nyingine itakayocheza nayo ni Azam FC ambao nao hawana cha kupoteza zaidi ya kumaliza nafasi ya tatu iliopo, pamoja na hilo Baleke alisema kila mchezaji atapambana na hali yake.
“Kila mmoja atavuna atakachokipanda ndani ya dakika 90, tutaipambania Simba yetu na wao wataipambania timu yao kuhusu kushuka ama kutokushuka hiyo siyo ishu yetu, kila mmoja yupo kazini kwake,”alisema.