Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU…KWA YANGA HII YA LEO..SIMBA WAPEWE MAUA YAKE TU MAPEMA…

UKWELI MCHUNGU…KWA YANGA HII YA LEO..SIMBA WAPEWE MAUA YAKE TU MAPEMA…

Habari za Simba SC

WAKATI leo Yanga wakilitia Taifa wasiwasi wa kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa magoli 2-1 dhidi ya USM Alger ,awali baada  Yanga kufuzu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Jumatano iliyopita kumekuwa na tambo nyingi kutoka kwa mashabiki wa Simba na Yanga.

Shida ilianza baada ya Yanga kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo, pale ilipoitoa Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0.

Vita ya maneno imekuja baada ya mashabiki wa Simba kudai timu yao ilifika hatua ya fainali mwaka 1993, huku wale wa Yanga wakisisitiza Simba haikuwahi kufikia hatua kama hiyo kwenye taji hilo.

Kuna wadau wa soka walijaribu kuchambua kuhusu ushiriki wa klabu hizo lakini baadhi walizungumzia kwa kuegemea upande mmoja, hususan wa timu wanazoshabikia.

Bahati mbaya kati yao wapo wadau wanaoaminiwa katika medani ya michezo nchini lakini wameamua kupotosha kwa makusudi historia kwa sababu ya maslahi binafsi. Wamekuwa wakiidisi Simba kana kwamba haikuwahi kufanya kitu katika soka la Tanzania kwenye fainali hizo za CAF. Inapondwa eti, taji ililoshiriki lilikuwa kama bonanza na kejeli nyingine, ila ukweli ni kwamba Simba wanastahili maua yao kwa kuwa klabu ya kwanza Tanzania kufika fainali za CAF miaka 30 iliyopita kabla ya Yanga kurejea rekodi hiyo msimu huu lakini kupitia Kombe la Shirikisho. Tiririka nayo…!

TATIZO HILI HAPA

Ubaya wa hiki wanachokifanya (kwa kuwa wanaaminiwa na wengi) kinaweza kuwapotosha wale wasiojua ambao ndio wengi. Ni kweli kuna utani wa jadi kati ya Simba na Yanga, lakini historia inapaswa kuheshimiwa.

Ni vizuri utani wa jadi ukabaki kuwa utani na historia ikaaelezwa kwa ukweli wake hata kama inakuumiza.

Kuna madai yametolewa kwamba, Kombe la Caf ambalo Simba ilishiriki na kufika fainali mwaka 1993 lilianzishwa na kabaila mmoja aliyeitwa Mashood Abiola raia wa Nigeria.

Pia, ilidaiwa na mmoja wa wadau wa soka, shindano hilo halikuwahi kutambuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa madai lilikuwa sawa na Kombe la Jengo au CCM ambayo yalikuwapo hapa nchini zamani kama sio Ndondo Cup.

UKWELI UKOJE?

Ni kweli michuano hiyo ya Kombe la CAF ilianza baada ya aliyekuwa mfanyabiashara na mwanasiasa mashuhuri nchini Nigeria, Mashood Abiola mwaka 1992, lakini lilipata baraka ya CAF kwa kulitambua ni kwa kulipa jina hilo la Kombe la CAF mwaka 1993 Simba ikafanya kweli.

Kombe la CAF lilikuwa ni shindano la kila mwaka linaloandaliwa na CAF kwa washindi wa pili wa ligi za ndani za vyama wanachama ambao hawajafuzu kwa mashindano ya awali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Washindi lililoasisiwa mwaka 1975 yaliyokuwa yakitambuliwa zaidi.

Ndipo michuano hiyo ilianzishwa 1992 kwa mtindo wa Kombe la UEFA la Ulaya. Taji lililopewa jina la Moshood Abiola, mfanyabiashara wa Nigeria, mchapishaji na mwanasiasa na pia Mkurugenzi wa kwanza wa Michezo katika Nigeria huru.

Kuanzishwa kwa Kombe la CAF lilikuwa ni wazo la Rais wa zamani wa Shirikisho hilo Issa Hayatou ambaye aliufanya mwaka 1992 kuwa mwaka wa michezo Afrika.

Mashindano hayo yalianzishwa mara baada ya kufanikiwa kwa Kombe la Mataifa ya Afrika la 1992 ambapo washindi 12 walishiriki katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya Afrika. Timu 31 zilishiriki katika Kombe la Caf na timu kutoka Nigeria Shooting Stars ilikuwa ya kwanza kubeba taji hilo baada ya kuifunga SC Villa ya Uganda katika mchezo wa fainali.

Taji hilo lilikuwa mali ya JS Kabylie ilililolibeba mara tatu mfululizo mwaka 2002.

RAJA NDIO WA MWISHO

Raja Casablanca ilikuwa timu ya mwisho kubeba taji hilo mwaka 2003 baada ya kuifunga timu kutoka Cameroon, Cotonsport de Garoua katika fainali.

Lilipoanzishwa Kombe la CAF, ikafanya Shirikisho la Afrika kuwa na mashindano matatu ya Klabu Bingwa Afrika (mshiriki bingwa wa nchi), Kombe la Washindi (Mshindi wa pili na Kombe la CAF.

Mwaka 2004, Kombe la CAF liliunganishwa na Kombe la Washindi Afrika na kubadilishwa jina na kuitwa Kombe la Shirikisho la CAF, kwa mara nyingine kwa kuiga Kombe la Ulaya UEFA Cup.

Kwa rekodi ni kwamba tangu kuasisiwa kwa Kombe la Shirikisho ni kweli Yanga ndio timu pekee ya Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki iliyovuka hadi nusu fainali na hatimaye fainali na sasa inasubiri kuona kama itaandika historia nyingine ya kubeba taji hilo mbele ya USM Alger ya Algeria ambapo katika mchezo wa leo USM wamepata ushindi wa goli 2-1.

MAUA YA SIMBA

Mwaka 1992 Tanzania iliwakilishwa na Small Simba ya Zanzibar ambayo ilitolewa raundi ya awali tu na Kisumu Postal ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kulala ugenini 2-1 na nyumbani 2-0, lakini katika msimu huo kwa ligi ya ndani Simba ilimaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga iliyotetea taji kwa msimu wa pili mfululizo kisha kulitetea tena 1993 kwa mara ya tatu.

Pia, ilikuwa ya pili kwenye Ligi ya Muungano ambayo kwa msimu huo bingwa alikuwa ni Malindi ya Zanzibar ilipangwa kushiriki Klabu Bingwa Afrika, huku Pamba iliyokuwa bingwa wa Kombe la Nyerere ikapangwa Kombe la Washindi na Yanga ikashiriki Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) michuano iliyofanyika Kampala Uganda, huku Simba ikienda kama watetezi kwani ilitwaa 1992 kwa kuifunga Yanga katika fainali kali iliyopigwa visiwani Zanzibar.

Katika ushiriki wa michuano hiyo, Malindi ilitolewa raundi ya kwanza na Zamalek kwa jumla ya mabao 5-0, huku Pamba nayo ikitolewa pia raundi ya kwanza na Al Ahly kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya raundi ya awali kupenya kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya Mukura Victory ya Rwanda iliyotoka sare ya 2-2, ikilala nyumbani 1-0 na kwenda kushinda ugenini kwa mabao 2-1.

Kwa upande wa Simba ikicheza kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya CAF ilifanya kweli kwa kuanzia raundi ya kwanza na kuifunga Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini kwani ilianza kwa suluhu nyumbani na kupata sare ya 1-1 ugenini na kuvuka hatua hiyo.

Raundi ya pili Simba ilikuitana na Manzini Wanderers ya Swaziland (sasa Eswatini) na kuifunga jumla ya mabao 2-0 ikishinda 1-0 nyumbani na ugenini na kutinga robo fainali na kuvaana na USM El Harrach ya Algeria. Simba ilishinda nyumbani 3-0 na kulala ugenini 2-0 na hivyo kuvuka nusu fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2 na kutinga nusu fainali.

Katika hatua hiyo walipangwa na Atletico Sportivo Aviacao ya Angola na mechi ya kwanza nyumbani Simba ilishinda mabao 3-1 na ilipoenda ugenini ikalazimisha suluhu kwenye pambano lililojaa vimbwanga kwa mashabiki wa ASA kuwasumbua mastaa wa Simba wa enzi hizo.

Klabu hiyo ikaandika historia ya kutinga fainali ikifuata nyazo za SC Villa ya Uganda kwa timu za Afrika Mashariki ikikutana na Stella Club d’Adjamé maarufu kama Stella Abidjan ya Ivory Coast na mechi ya kwanza iliisha kwa suluhu ugenini na kukubali kipigo cha mabao 2-0 nyumbani na kuliacha taji likirudi tena Afrika Magharibi.

UKWELI MCHUNGU

Mwaka 1979, Gor Mahia ya Kenya ilifika fainali ya Kombe la Washindi na mwaka 1987 ilishinda taji hilo la Afrika.

Ni taji pekee lililokuja Afrika Mashariki kabla ya michuano hiyo kufutwa kwa kuunganishwa na Kombe la CAF kuwa Kombe la Shirikisho Afrika ambalo kwa msimu huu Yanga imetinga fainali na kusubiri kuandika historia ya kulibeba kama itaifunga USM Alger.

Je ni kweli K’Ogalo leo hii haipaswi kujivunia taji hilo la Washindi ililotwaa mwaka 1987 kwa sababu michuano hiyo ilifutwa? SC Villa haiwezi kuijivunia kufika fainali ya Kombe la CAF 1992 kwa sababu michuano hiyo haipo tena? Hii si kweli! Ndio maana hata Simba na Tanzania bado zinapaswa kujivunia kwa kufika fainali za michuano ya Kombe la CAF 1993.

Yanga imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu, ikiwa ni timu ya kwanza kufanya hivyo Afrika Mashariki baada ya mabadiliko ya mwaka 2004.

Hakuna timu iliyofanya hivyo kabla yake, lakini ukweli ni kwamba Simba ilitinga fainali wakati taji hilo likiwa halijaunganishwa na hivyo wanastahili maua kwa heshima iliyowekwa badala ya kupuuzwa!

SOMA NA HII  KWA MARA YA KWANZA NABI AFUNGUKA ISHU YA KUWATIMUA SAIDO NA AMBUNDO....KASEKE AKOLEZA NDIMU...