Home Habari za michezo KUELEKEA FAINAL CAF…MASHABIKI YANGA WAANZA KUWAPULIZA WAARABU MAPEMA…

KUELEKEA FAINAL CAF…MASHABIKI YANGA WAANZA KUWAPULIZA WAARABU MAPEMA…

Habari za Yanga SC

Mashabiki na wanachama wa Yanga mkoani Mbeya wamesema watatumia gharama yoyote kuhakikisha mchezo wao wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Algers wanamalizia Dar es Salaam kwa kupata idadi kubwa ya mabao.

Pia wamesema watajitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Mkapa kuishangilia timu hiyo ambapo zaidi ya mabasi 10 yanatarajia kutumika kusafirisha mashabiki hao kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kushangilia timu hiyo.

Wakizungumza baada ya kikao cha maandalizi ya mechi hiyo kilichofanyika jijini hapa kwa kushirikisha viongozi wa matawi yote mkoani humo wamesema wanahitaji kuona Yanga ikiweka rekodi, historia na heshima kwa Taifa kuleta taji hilo la Afrika nchini.

Mwenyekiti wa matawi hayo mkoani Mbeya, Said Suleiman ‘Kastela’ amesema matarajio yao ni kuona Yanga inashinda mechi hiyo itakayopigwa Mei 28 na kuleta ubingwa.

Amesema kutokana na mchezo huo kuwa muhimu kila mmoja anatamani kushuhudia mechi hiyo na kwamba wanatarajia mabasi 10 makubwa yakiwabeba mashabiki.

“Nani hataki kuona fainali ya Afrika, wote tunayo shauku ya kutazama mchezo huo ndio maana tumekubaliana viongozi wa matawi Wilaya waorodheshe mapema majina ili Juamatatu (kesho) tujue idadi rasmi” amesema Kastela.

Kwa upande wake Katibu na Msemaji wa timu hiyo mkoani humo, Rajabu Mrisho amesema kwa umri wao hii ni historia kushuhudia fainali hiyo, hivyo wanaenda kwa lengo la kuhakikisha Yanga inashinda fainali hiyo.

“Tutatumia gharama yoyote kumaliza mchezo huo pale Dar es Salaam ili mechi ya marudiano iwe ni kukamilisha ratiba, tunataka kushinda mabao yasiyopungua matatu na kuendelea,”

“Tunao makocha bora, wachezaji imara na sisi tunaenda kitofauti kwa mikakati mizuri ya kuipa timu ushindi, kwa umri wetu hii ni historia kubwa kuwahi kutokea hivyo lazima tufanye kitu msimu huu” ametamba Mrisho.

SOMA NA HII  BEKI SIMBA ASHONWA NYUZI SITA,MACHOZI NA MAUMIVU YAKUTOSHA