Home Habari za michezo YANGA BADO TATU TU….

YANGA BADO TATU TU….

Singida vs Yanga SC

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga imeondoka na alama tatu ugenini baada ya kuwachapa wenyeji wao Singida Big Stars kwa mabao 2-0 kwenye mchezo uliomalizika katika Uwanja wa CCM Liti Mkoani Singida.

Ushindi huo unaifanya Yanga sasa kuhitaji alama Tatu pekee kwenye mechi zake tatu zilozobaki kujihakikishia ubingwa wa pili mfululizo wa Ligi Kuu Bara huku mechi yao ijayo wakirudi nyumbani kupambana dhidi ya Dodoma Jiji .

Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huo.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuendelea kujikita kileleni wakifikisha alama 71 huku Singida wao wakibaki na alama zao 51 katika nafasi ya nne wakiendelea kupambana na Azam kuwania nafasi ya tatu.

Yanga imemalizana na Singida Big Stars msimu huu kwenye ligi wakifanikiwa kuondoka na alama zote 6 kufuatia kuwafunga nyumbani na ugenini huku wakiwafunga jumla ya mabao 6-1.

Mchezo wa kwanza Yanga ikiwa nyumbani ilifanikiwa kushinda kwa mabao 4-1 huku Leo ikishinda kwa mabao 2-0 ugenini.

Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga alikuwa ni Stephanie Aziz akifunga bao hilo dakika ya 15 kwa shuti kali, likiwa ni bao la tisa msimu huu kwake kwenye ligi huku mshambuliaji Clement Mzize aliyefunga bao la pili likiwa ni bao la tano kwake msimu huu.

Aziz KI pia amekuwa kinara wa wachezaji waliofunga kwa mguu wa kushoto akiwa na mabao hayo 9 akifuatiwa na Mosses Phiri wa Simba aliyefunga mabao mabao 5.

Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi aliendelea na ukuta wake wa wazawa ukiwa na mabeki Dickson Job,Kibwana Shomari Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘ Bacca katika mechi ya pili mfululizo ukiwa haujaruhusu bao.

Hata hivyo Nabi alimpumzisha Job kipindi cha pili akimrudisha Mkongomani Djuma Shaban kucheza beki ya kulia katika mchezo huo.

Hiyo inakuwa ni mechi ya 27 msimu huu kwa Yanga wakiwa wameshinda jumla ya michezo 23 huku wakitoa sare mbili na kupoteza mbili huku mabao hayo mawili yakiwafanya kufikisha mabao 52 ikiwa ni timu ya pili kufunga mabao mengi wakiwa nyuma ya watani wao Simba wenye mabao 63 ya kufunga.

Singida wao huo unakuwa ni mchezo wa 6 kupoteza msimu huu huku mabao hayo mawili waliyoruhusu yakiwafanya kufikisha mabao 22 ya kufungwa.

Yanga imeendelea kuwa kinara ya timu iliyoshinda mechi nyingi ugenini ambapo katika mechi zao 13 wakishinda michezo 11 wakifuatiwa na Simba ambao kwenye mechi 15 wakishinda 9.

SOMA NA HII  SIMBA TENA....CAF WAIBEBA MBELE YA HOROYA...WAFUNGIWA KUTUMIA UWANJA WAO....