Home Azam FC KWA CV HII YA KOCHA MPYA WA AZAM FC….MSIMU UJAO WASIPOBEBA KOMBE...

KWA CV HII YA KOCHA MPYA WA AZAM FC….MSIMU UJAO WASIPOBEBA KOMBE ‘HAWATUSUI TENA’..

Kocha Mpya Azam FC

AZAM FC imemtangaza Kocha wao mpya, Youssouph Dabo raia wa Senegal kwa ajili ya kukifundisha kikosi hicho kwa msimu ujao akichukua nafasi ya Kally Ongala.

Dabo anatua kwenye timu hiyo baada ya kuachana na ASC Jaraaf de Dakar huku akikumbukwa zaidi baada ya kuifundisha Teungueth iliyokuwa na staa wa Simba, Pape Sakho na Malikcou Ndoye wa Azam.

Dabo mwaka 2016, akiwa na Teungueth alitwaa ubingwa wa Kombe la Ligi na 2017 akiwa Kocha wa Teungueth alifika fainali ya Kombe la Senegal (sawa na Kombe la Shirikisho la Azam hapa nchini).

Desemba 2018, alitwaa ubingwa wa vijana chini ya miaka 20 kwa timu za taifa ukanda B wa Afrika Magharibi (Wafu B) katika mashindano yaliyofanyika nchini Togo na Februari 2019 alichaguliwa kocha bora wa AFCON chini ya miaka 20 huko Niger alipoiwezesha Senegal kufika hatua ya fainali.

Juni 2019 aliiongoza Senegal kufika robo fainali ya Kombe la Dunia chini ya miaka 20 kule Poland na Julai 2019 alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya Senegal iliyofika fainali ya AFCON Misri.

Agosti 2019, akiwa kocha wa timu ya taifa ya Senegal chini ya miaka 23, aliiongoza kushika nafasi ya tatu hivyo kushinda medali ya shaba kwenye michezo ya Afrika iliyofanyika jijini Rabat, Morocco.

Desemba 2019, Dabo aliiongoza Senegal kushinda ubingwa wa Kanda ya Wafu mashindano yaliyofanyika Guinea na Machi 2020 aliiongoza Senegal kushinda ubingwa wa vijana chini ya miaka 20 katika mashindano ya mataifa ya Kiarabu ikishiriki kama wageni waalikwa yaliyofanyika Saudi Arabia.

Novemba 2020, akiwa kocha wa timu ya taifa ya Senegal chini ya miaka 20 alifika fainali kuwania ubingwa wa kanda A ya Afrika Magharibi na msimu wa 2020/21 alishinda ubingwa wa Ligi ya Senegal akiwa na Teungueth.

Msimu wa 2020/21, Dabo akiwa na Teungueth iliiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuishangaza Raja Casablanca ya Morocco kwenye mchezo wa raundi ya kwanza.

Mchezo wa kwanza uliofanyika Senegal ulimalizika kwa 0-0 sawa na mechi ya marudiano iliyopigwa pale nchini Casablanca kisha kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ndipo Teungueth ikashinda 3-1.

Kuteuliwa kwa Dabo hakuwezi kuathiri nafasi ya Ongala kwani huenda akarejea nafasi yake ya mwanzo aliyokuwa anaitumikia ya kuendelea kuwa kocha wa washambuliaji ndani ya kikosi hicho.

Kally alipewa kibarua hicho baada ya Klabu hiyo kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu Mfaransa, Denis Lavagne aliyetimuliwa Oktoba 22 mwaka jana kutokana na matokeo mabovu yaliyokuwa yanaiandama.

SOMA NA HII  MABOSI SIMBA NI NOMAA....WAWAPA MASTAA WAPYA MIKATABA YA KIMAFIA MWANZO MWISHO...