Home Habari za michezo ROBERTINHO:- KUNA SIKU TUTAMFUNGA MTU GOLI 10-0…MASHABIKI SIMBA WANANIFUATA SANA…

ROBERTINHO:- KUNA SIKU TUTAMFUNGA MTU GOLI 10-0…MASHABIKI SIMBA WANANIFUATA SANA…

Tetesi za Usajili Simba

Kocha Mkuu wa Simba Robert Oliveira ‘Robertinho’ ametamba kwamba endapo Simba itafanya usajili ambao amezungumza na mabosi wake Kuna uwezekano mkubwa wekundu hao wakampiga mtu hata 10 -0 msimu ujao.

Kauli hiyo ya Robertinho inakuja kufuatia juzi kuichapa Polisi Tanzania kwa mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, matokeo yaliyoishusha rasmi maafande hao kwenda Ligi ya Championship kwa msimu ujao.

Katika mchezo huo uliopigwa Azam Complex, Chamazi, kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza alifunga mabao matano pekee yake, huku jingine likiwekwa kimiani na Israel Mwenda na kumfanya nyota huyo wa Burundi kuifikia rekodi ya Nsa Job na Edibily Lunyamila walioiweka 1998 na 2009 walipofunga mabao matano kwenye mchezo mmoja dhidi ya Kagera Stars na Villa Squard.

Akizungumza Robertinho alisema hashangazwi na matokeo hayo kwa timu yake na kwamba falsafa wanayoitumia ni rahisi kutengeneza mabao mengi endapo watakutana na timu isiyojua kucheza kwa nidhamu.

Robertinho alisema endapo kikosi chake kitapata mastaa wakubwa zaidi mithili ya Said Ntibazonkiza ‘Saido’aliyefunga mara tano katika ushindi huo wa juzi Simba itakuja kumfunga mtu mabao 10 msimu ujao.

“Wala sio kitu cha kunishtua ni vile bado tuna wachezaji ambao wanakosa utulivu lakini falsafa yetu inaturuhusu kushinda zaidi ya mabao haya ambayo tumeyapata kwa Polisi,” alisema Robertinho

“Mara ya kwanza tulishinda mabao Saba dhidi ya Horoya watu waliona kama tumebahatisha, Horoya hawakuwa timu mbovu lakini ubora wa soka letu uliwaadhibu, Saido ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa alitulia akatumia nafasi nyingi.

Alisema msimu ujao anawasubiri mastaa wapya ambao endapo watawapata wachezaji wanaowataka basi Simba itacheza mpira mkubwa zaidi ya huu unaocheza sasa. Alisema anahitaji mastaa ambao watakuja kuwapa changamoto kubwa hawa ambao wanawakuta ili watengeneze timu ngumu ambayo itarudisha heshima ya Simba

“Nawaza sana kuhusu msimu ujao, nasubiri kuona wachezaji tuliozungumza na uongozi wanaletwa, hiyo itakuwa ni heshima kubwa kwa mashabiki wetu ambao kwangu mimi wanastahili kikubwa kuliko hiki cha msimu huu.

“Kila ukitembea barabarani unakutana na shabiki wa Simba anakuomba kutengeneza timu bora kwa msimu ujao, hii ni klabu kubwa inastahili matokeo bora na mataji mengi.”

SOMA NA HII  ALICHOSEMA GOMES BAADA YA KAIZER CHIEFS KUTOKA SARE JANA