Home Habari za michezo WAKATI LEO NI SIKU YA HISTORIA KWA YANGA…JIWE LA NABI HILI HAPA...

WAKATI LEO NI SIKU YA HISTORIA KWA YANGA…JIWE LA NABI HILI HAPA DHIDI YA WAARABU…HAWATOKI…!!!

Habari za Yanga SC

YANGA ina dakika 90 za kupindua meza dhidi ya USM Algers na kuishtua Afrika kwa kuandika rekodi mpya.
Iko ugenini kwenye Uwanja wa Julai 5, Algiers, Algeria ikihitajika ushindi wa kuanzia mabao 2-0 baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa mabao 2-1. Mechi ya leo itapigwa saa 4 usiku.

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa licha ya kutokuwa na matokeo mazuri kwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mashindano hayo, uliipa Yanga mwanga wa namna inavyoweza kujipanga katika mechi ya leo hasa katika upangaji wa kikosi na wachezaji wa kuwatumia ili iweze kupata ushindi ambao utawafanya warudi na taji la Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Ingawa benchi la ufundi la Yanga linaweza kuwa na mpango wake wa mchezaji yupi wa kuanza, wa kukaa benchi na nani wa kukaa jukwaani, kutokana na hitajio la mchezo huo kuwa ni ushindi tu na hapana shaka inahitajika kushambulia kwa muda mrefu wa mchezo, kikosi kifuatacho kinaweza kuwashangaza USM Alger.

UKUTA
Yanga inaweza kuufanyia kazi kwa ufanisi mkubwa mpango wa kushambulia ikiwa safu yake ya ulinzi itaundwa na Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘Bacca’.

Kipa Djigui Diarra, kiufundi uwezo wake wa kucheza mipira kwa miguu ambao umekuwa ukimuwezesha kushiriki katika ujenzi wa mashambulizi, unamhakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha Yanga leo.

Djuma na Kibwana wakianza katika nafasi za mabeki wa pembeni wanaweza kuchangia kuipa Yanga kile ambacho inakihitaji katika mchezo huo ambacho ni uwiano mzuri katika kushambulia na kuzuia.

Upande wa beki wa kulia, Djuma anaweza kuwa chaguo sahihi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushambulia hasa katika kutengeneza nafasi na kupiga krosi ingawa anahitaji kuwa na winga wa kumzibia vyema nafasi pindi akipanda mbele wakati kushoto Kibwana atasaidia vilivyo katika ulinzi kwani ndio upande ambao USM Alger wamekuwa wakiutumia zaidi katika kushambulia.

Katika nafasi ya mabeki wa kati, Mwamnyeto na Bacca wanaweza kuendelea kuaminiwa na kocha Nasreddine Nabi.

KWENYE KIUNGO
Kocha Nabi atamkosa kiungo wake Khalid Aucho ambaye anatumikia adhabu ya kukosa michezo miwili kutokana na kupata idadi ya kadi sita za njano katika mashindano hayo.

Yanga inawahitaji wachezaji wepesi wa kufanya uamuzi pindi wawapo na mpira, kuichezesha timu kwa haraka na kutopoteza sana muda pindi wanapomiliki mpira na kupelekea kuwapa nafasi wapinzani kujipanga.

Yannick Bangala na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye aliingia kutokea benchi katika mchezo uliopita wanaonekana wanaweza kuwa chaguo sahihi kucheza kama viungo wa ulinzi na juu yao anaweza kupanga Mudathir Yahya ambaye ana uwezo mkubwa wa kusaidia mashambulizi na kukaba kuanzia mbele.

PALE MBELE SASA
Fiston Mayele atabaki kuwa chaguo la kwanza la Yanga katika nafasi ya mshambuliaji wa kati kutokana na kasi, uwezo mkubwa wa kufumania nyavu na hata kuichezesha timu na kupiga pasi za mwisho.

Wachezaji wengine wawili ambao wanaonekana wataipa mchango mkubwa Yanga katika kikosi cha kwanza leo ni Jesus Moloko na Bernard Morrison.

USM Alger ni timu ambayo imekuwa na nidhamu kubwa ya kujilinda ikifanya hivyo kwa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji pindi inaposhambuliwa.

Mbinu bora ya kuvuruga muundo wa kiulinzi wa USM Alger ni kuwa na washambuliaji wabunifu ambao wanaweza kuifungua safu ya ulinzi ya timu pinzani.

Moloko ni chaguo sahihi upande wa winga ya kulia kwa sababu amekuwa vyema katika kutengeneza nafasi na kufunga mabao na amekuwa akitoa msaada mkubwa katika ulinzi hivyo atakuwa anaziba nafasi itakayoachwa na Djuma Shaban pindi anapokwenda kusaidia mashambulizi.

Bernard Morrison sio mzuri sana katika kusaidia kulinda pindi wanaposhambuliwa lakini ana ubunifu na ujanja wa kuwatoka mabeki wa timu pinzani akitegemea zaidi chenga na umiliki wake wa mpira.

Uwepo wa Kibwana upande huo utampa eneo kubwa la kucheza Morrison ambaye amekuwa akifanya vyema zaidi pale anapopata fursa hiyo, jambo litakalokuwa na faida kubwa kwa Yanga.

KWENYE BENCHI
Yanga ikitokea imeanzisha kikosi hicho, kiufundi itabakiwa na benchi lenye idadi ya kutosha ya wachezaji ambao wataingia na kutoa msaada ikiwa wanahitajika kufanya mabadiliko ya kimbinu.

Golini watakuwa na Metacha Mnata, mabeki ni Dickson Job, Joyce Lomalisa na viungo wakiwa ni Farid Musa, Zawadi Mauya, Aziz Ki na washambuliaji ni Kennedy Musonda, Tuisila Kisinda na Clement Mzize.

NABI ATUMIA AKILI
Kocha Nabi alisema kuwa licha ya wengi kuamini kuwa USM Alger itatwaa ubingwa, anaamini wana uwezo wa kupata ushindi mnono ugenini na kutwaa ubingwa. Alichofanya ni kutanguliza watu mapema Algeria lakini anapata pia mbinu kutoka kwa wenzie kutoka mataifa mbalimbali wenye uwezo wa kusoma mchezo ndani na nje ya uwanja.

“Itakuwa ngumu lakini haishindikani kubadili mawimbi. Siwezi kuahidi kwamba taji litakuja Tanzania. Ninaweza kuahidi kwamba kwa vile kuna tumaini, tutapambana. Tunatakiwa kufunga mabao mawili ili tuwe na nafasi na tunapata utulivu kutokana na tulichokipata ugenini katika robo fainali na nusu fainali.

“Vijana walitengeneza nafasi nyingi wikiendi iliyopita dhidi ya timu yenye ukuta mgumu. Hii inatupa matumaini na matokeo ya fainali bado sana kukamilika,” alisema Nabi ambaye mashabiki wanaamini uwezo wake mkubwa wa kubadili mchezo haswa kipindi cha pili anapofanya mabadiliko yoyote.

SOMA NA HII  MIQUISSONE KUTOKA SIMBA HADI KMC TENA KWA MKOPO