KOCHA Nasreddine Nabi amemalizana na Yanga baada ya kugoma kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kuifundisha timu hiyo aliyoifanya iwe tishio, huku akiwa ameipa kiasi cha Sh 4 Bilioni zilizotokana na mataji iliyoyapa sambamba na bonasi kutokana na mataji hayo.
Nabi aliyetua Jangwani Aprili, 2021 na kudumu Yanga kwa miaka miwili na nusu, huku hesabu zikionyesha chini ya kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Tunisia, klabu hiyo imevuna fedha ndefu kufuatia ubora na mafanikio ya kuchukua mataji na kuifikisha timu fainali za Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha huyo ambaye bado yupo jijini Dar es Salaam kwa muda, ametwaa mataji sita akiwa na Yanga yakiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili mengine ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na Ngao ya Jamii mara mbili na mafanikio yoye hayo yameiingizai Yanga fedha kutoka kwa wadhamini.
SH1 BILIONI AZAM
Kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu kwa misimu miwili mfululizo kwa Yanga ikiwa na Nabi imeiwezesha jklabu hiyo kuvuna kiasi cha Sh 1 Bilioni kutoka kwa wadhamini wa matangazo ya televisheni wa ligi hiyo, Azam Media inayotoa bonasi ya Sh 500 Milioni kwa bingwa kila msimu.
Yanga ilibeba taji msimu uliopita wakati mkataba huo wa Azam Media ukiwa umeshasainiwa tangu mwaka juzi na timu hiyo kulamba Sh 500 Milioni kabla ya msimu huu tena kulitetea na kukomba kiasi kama hicho na kuifanya kwa mataji ya Ligi Kuu kutoka kwa Azam TV ivune Sh 1 Bilioni.
SH200 MILIONI ZA NBC
Kama ilivyokuwa kwa Azam TV, Yanga pia imevuna Sh 200 Milioni kwa kubeba taji la Ligi Kuu mbali na kombe na medali.
Kila msimu bingwa wa nchi huvuna Sh 100 Milioni inazopewa bingwa wa msimu kutoka kwa Wadhamini Wakuu wa ligi hiyo, Benki ya NBC na kwa kutwaa mara mbili, Yanga imekomba Sh 200 Milioni.
SH100 MILIONI ASFC
Chini ya Nabi, Yanga imeendelea kutunisha akaunti yake ya fedha kwa kuvuna mamilioni mengine kutokana na kubeba mataji mawili kwa misimu miwili tofauti ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC).
Kwa msimu wa kwanza Yanga ilivuna Sh 50 Milioni za ubingwa wa michuano hiyo na bonasi ya Sh 50 milioni na msimu huu wa pili ijkavuna tena kiasi kama hicho cha ubhingwa mbali na Kombe na Medali.
SPORTPESA SH412 MILIONI
Yanga kuwa bingwa wa ligi katika misimu miwili mfululizo pia walivuna fedha kutoka kwa wadhamini wao wa klabu wakuu kampuni ya SportPesa ambapo kwa ubingwa wa kwanza walichukua sh 100 milioni, lakini msimu uliomalizika kiasi hicho kiliongezeka na kufikia sh 150 milioni na kuifanya Yanga jumla kuchukua sh 250 milioni.
Ukichanganya na bonasi ya kutwaa Kombe la ASFC, Yanga imekusanya tena Sh 162 kutoka SportPesa, ikiwamo Sh50 Milioni za msimu uliopita na 112 za msimu huu kulingana na mkataba mpya uliosainiwa mwaka jana ulioboresha kiwango cha bonasi kwa kufika fainali au kubeba taji.
Ukizikusanya fedha hizo za bonasi kwa kutwaa mataji hayo manne yaani mawili ya Ligi Kuu na mengine ya ASFC, Yanga imekomba jumla ya Sh 412 Milioni na kuitunisha akaunti yao ya fedha.
SH2.3 BILIONI ZA CAF
Msimu huu uliomalizika Yanga ikaupiga mwingi zaidi nje ya mipaka ya Tanzania chini ya Nabi kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza washindi wa pili baada ya kuukosa ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria waliotoka sare ya 2-2.
Hatua hiyo, imeiwezesha Yanga kuandika historia katika uhai wa klabu hiyo tangu iasisiwe mwaka 1935 kwa kufika fainali ya kwanza ya CAF, ambayo pia imewapa kiasi cha Dola 1 Milioni (kiasi cha Sh 2.3 Bilioni) za ushindi wa pili wa michuano hiyo na kuzidi kuutunisha mfuko fedha chini ya Nabi.
Ukichanganya hesabu za fedha zote ambazo Yanga imevuna chini ya Nabi kwa misimu miwili aliokuwa nao ni zaidi ya Sh 4 Bilioni, ambapo ni mbali na bonasi nyingine zinazotokana na mipaka mingine minono iliyonayo klabu hiyo kutoka Azam TV ya kurusha maudhui ya timu hiyo, Haier na wengine walionao, kiasi kwamba kocha huyo anaondoka Jangwani akiwa hana deni analodaiwa.