KOCHA Nasreddine Nabi ameondoka nchini baada ya kumalizana na Yanga na kama kuna mtu anayetamani kusepa naye atakapomalizana na klabu mpya basi ni kocha wa viungo, Helmy Gueldich aliyefanya naye kazi kwa ufanisi, hata hivyo huenda dili lisiwepo tena kwa kutosana.
Nabi aliyeinoa Yanga kwa miaka miwili na nusu na kuwapa jumla ya mataji saba pamoja na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, amekuwa akihusishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini wapinzani wakuu wa AmaKhosi, yaani Orlando Pirates imeanza hesabu za kumbeba fundi huyo wa mazoezi mwenye elimu ngazi ya Profesa ya mazoezi ya kisasa.
Amakhosi wanataka kumchukua Nabi akawe kocha wao mkuu, lakini sharti kubwa walilopewa na kocha huyo ni kwamba anataka atue hapo na wasaidizi wawili na mmoja akiwa ni Helmy ambaye mashabiki wa Yanga wanamkubali sana kwa mazoezi na mzuka wake anapokuwa kazini.
Hata hivyo, Orlando wameamua kutimia mkono kwenye dili hili wakitaka kumchukua haraka Helmy ili akaimarishe benchi la ufundi la timu hiyo, hususani kitengo cha mazoezi ya viungo ya wachezaji wakivutiwa na ufanisi wake alipokuwa Yanga.
Akili hiyo ya Orlando inatokana na kunusa hesabu ndefu za watani wao Amakhosi ambao walikuwa wakivuatana na kocha wa viungo wa sasa Muzi Maluleke ambaye bado alikuwa na mkataba na klabu hiyo. Helmy mkataba wake na Yanga unafikia mwishoni mwezi huu, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa hawataki kusikia habari za kocha huyo atimke klabuni, lakini Wasauzi wamempania.
Nabi amemkataa Maluleke raia wa Afrika Kusini akidai sio mtaalamu mwenye mazoezi ya kisasa kwa wachezaji wa soka, hivyo anapambana Amakhosi kumuingiza Helmy kwenye benchi lake jipya.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa Helmy ambaye tayari yuko kwao Tunisia zinasema atalazimika kusubiri kujua muelekeo wa Nabi kutua Amakhosi ambapo endapo dili hilo litakwama atafanya maamuzi mengine ikiwa ni kama kumtosa, kusudi maisha yaendelee.
Wakiwa wawili ndani ya Yanga Helmy ameifanya timu hiyo kuupiga mwingi na kuwa na pumzi za kutosha tofauti na awali kabla ya kutua Jangwani, vijana wa Yanga walionekana wakikata pumzi haraka kiasi cha kutakiwa wazee wa dakika 45 tu.
Kocha huyo wa viungo amekuwa maarufu kwa mashabiki kutokana na midadi ya ushangiliaji wa mabao ya Yanga, ambapo huwa wa kwanza kuungana na wachezaji uwanjani kushangilia kila bao likifungwa tofauti na watu wengine wa benchi la ufundi la timu hiyo iliyotwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya ASFC, Ngao ya Jamii mara mbili na Kombe la Mapinduzi wakiwa na Nabi.