Home Habari za michezo PAMOJA NA YANGA ‘KUSHINE’ ….SIMBA NAO WAKO NJEMA AISEE…MAMBO HAYA YAMEWAPA HESHIMA...

PAMOJA NA YANGA ‘KUSHINE’ ….SIMBA NAO WAKO NJEMA AISEE…MAMBO HAYA YAMEWAPA HESHIMA CAF…

Habari za Simba

Simba ya kibabe Afrika, ndio ndoto ya kila shabiki wa timu hiyo wakati Wekundu wa Msimbazi wakitaka kuisahau njozi mbaya ya kumaliza msimu wa pili bila ya taji lolote na huku wakijiandaa na michuano ya pesa ndefu ya Super League itakayowakutanisha na miamba ya Afrika.

Michuano ya Caf Super League imepangwa kuhusisha timu 24 ambazo zitakuwa zinapanda na kushuka daraja, huku timu itakayofika fainali itacheza mechi 21, lakini kwa msimu huu wa kwanza ligi hiyo itahusisha timu nane tu – tano zikiwa ni Mabingwa wa Afrika na tatu zilizofanya vyema katika miaka ya hivi karibuni, ambazo ni Simba ya Tanzania, Horoya ya Guinea na Petro Atletico ya Angola.

Timu shiriki ambazo zimewahi kutwaa ubingwa wa Afrika zitakazokuwamo ni mabingwa mara 10 wa CAF, Al Ahly ya Misri, Esperance Tunis (Tunisia), Wydad Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) na TP Mazembe ya DR Congo.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino wakati akitambulisha michuano hiyo alipoenda kusherehekea miaka 80 ya klabu ya TP Mazembe nchini DR Congo, alisema kwamba lengo la Super League ni kulitangaza soka la Afrika na kuiwezesha kila nchi wanachama (53) kuwa na uwanja wenye viwango vya kimataifa vya FIFA kwa kuvikarabati na kuviendeleza.

MWAKA UISHE TU

Huu mwaka na uishe tu. Takriban kila shabiki wa Simba atakwambia hivyo baada ya kuishuhudia timu hiyo ikimaliza msimu wa pili bila ya taji lolote.

Kiufupi, haya sio maisha ambayo Wanasimba wameyazoea baada ya timu yao kutawala soka la nchi kwa miaka minne mfululizo na kutingisha katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Caf.

Lakini sasa nchi ikiwa imeshikwa na mahasimu wao na mabingwa wa kihistoria, Yanga, ambao mbali na kuzoa mataji ya ndani, wamefika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kitu ambacho Simba haijawahi kukifanya – Wekundu wanapaswa kufanya uamuzi mgumu kuirejesha timu yao pale juu.

(NB: Simba iliwahi kufika fainali ya Kombe la CAF, michuano ambayo haipo tena).

Suala la kukosa tena ubingwa msimu ujao, ni jambo ambalo hamna shabiki wa Simba anatamani hata kuliwaza.

Matamanio ya kila mmoja ni kuona Simba inainyima Yanga kupiga hat-trick ya makombe ya Ligi Kuu Bara na pia iweze kujibu mbwembwe hizi za Yanga kufika fainali Afrika, kwa kufanya makubwa CAF kuanzia kwenye Super League na pia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Lakini ili kufanya vyema dhidi ya wababe wa Afrika ni lazima uwe na kikosi imara na kipana.

Ili kuwa na kikosi imara cha ushindani, kila klabu shiriki ya Super League itapewa dola 2.5 milioni (Sh5.9 bilioni) kwa ajili ya maandalizi. Na bingwa atavuta dola 11.5 milioni (Sh27 bilioni).

USAJILI BOMBA

Hii ina maana kwamba Simba washindwe wenyewe kusaka wachezaji wa ubora wa juu kwa sababu mkwanja huu unaokaribia Sh6 bilioni sio pesa ndogo.

Simba ilimteua Mels Daalder, raia wa Uholanzi kuwa msaka vipaji (skauti mkuu) kama sehemu ya mikakati ya klabu hiyo ya kuimarisha kikosi chao, ambacho kukosa upana kumewagharimu msimu huu.

Tofauti na Yanga, Simba ilionekana kuwa katika wakati mgumu pale ilipopanga kikosi cha wachezaji ambao hawakuwa wakianzishwa mara kwa mara na kama ilivyotarajiwa mara nyingi hawakuwa na madhara kwa wapinzani wao.

Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kusajili au tuseme kutumia vyema zile Sh6 bilioni za Super League kuleta majembe ya maana.

Na ukizungumzia kusajili, mashabiki wengi wanaamini kwamba Simba inapaswa kubomolewa yote na kusajili wakali wengine kwa sababu kwa misimu miwili haijashinda taji lolote.

Lakini ukweli ni kwamba Simba hii bado inatisha, tukubali tukatae. Hii ni timu kali kabisa ya kutingisha Afrika na takwimu zinaonyesha.

Simba hii ambayo wengine wanaiona ni mbovu ndiyo ambayo imekaribia zaidi kufika nusu fainali ya Afrika msimu huu kuliko wakati mwingine wowote iliocheza robo fainali za Caf baada ya kutolewa kwa β€˜matuta’ na mabingwa watetezi Wydad kule Casablanca.

WATU WANAJICHANGANYA

Ni Simba hii hii inayosemwa ni mbovu ndiyo iliyowapoteza na kuwafunga mabingwa watetezi wa CAFCL, Wydad pale Kwa Mkapa katika mechi yao ya mkondo wa kwanza wa robo fainali, ambayo kama Wekundu wa Msimbazi wangetulia wangeweza kuimaliza mechi hapahapa kwa kuwafunga mabao 2-0, au zaidi. (Kumbuka ile nafasi aliyoikosa Clatous Chama katika dakika za lala salama, kati ya nafasi nyingine kadhaa walizopoteza).

Simba inayosemwa ni mbovu ndio timu ambayo licha ya kuanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kusuasua kwa vipigo viwili, ilifuzu robo fainali kwa kishindo ikiwamo kutoa kipigo kikubwa zaidi katika michuano hiyo ya Caf mwaka huu cha mabao 7-0 dhidi ya Horoya.

Pia ikaifunga kwa bao 1-0 bingwa wa Afrika Wydad Dar es Salaam huku pia ikiumaliza unyonge wa miaka miwili dhidi ya Yanga kwenye ligi kwa kuifunga 2-0 katika Dabi ya Kariakoo

Hamna timu mbovu inayoweza kufanya yote haya kwa mpigo: kumfunga bingwa wa Afrika, kumpasua bingwa wa Tanzania, kutoa kipigo kikubwa zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kutoa kipigo kikubwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara na kuongoza kwa mabao Ligi Kuu Bara (72) huku pia ikiwa imefungwa machache zaidi 15, ikiipiku Yanga iliyofungwa 18 licha ya kubeba ubingwa mapema.

SIO KINYONGE

Licha ya kutotwaa taji lolote, Simba haiko kinyonge huku takwimu hizo ni zikithibitisha kwamba Simba inaweza kupambana Afrika na kwenye Super League, lakini ili kufanya vizuri zaidi itahitaji kuboresha kikosi kiwerevu, sio kwa kukurupuka kwa mtazamo kwamba Simba yote ni mbovu.

Kuifumua Simba yote na kukimbilia kusajili timu mpya, kunaweza kukawa na madhara yake ikiwamo kuchukua muda kwa wachezaji kuzoeana, kuchelewa kuzoea staili ya timu, au kuchelewa kuzoea ligi mpya na mazingira mapya ya maisha kiujumla na hivyo timu kuchukua muda kukaa kwenye mstari. Kumbuka, ukichelewa wenzako wanakuacha.

Kufunga mabao mengi zaidi ya yeyote kwenye kunamaanisha kwamba Simba haina tatizo kubwa kiasi hicho katika umaliziaji, na kuruhusu mabao machache zaidi katika ligi kunamaanisha kwamba Simba sio mbovu kiasi hicho katika kujilinda hasa ikizingatiwa mara pekee ambayo timu haikujilinda vyema ilikuwa ni dhidi ya Raja Casablanca ambapo ilifungwa 3-0 Dar es Salaam na 3-1 kule Casablanca, Morocco. Ukiacha hizo kuna mechi chache sana ambazo Simba imeruhusu mabao mawili msimu huu.

Lakini kama wasemavyo, risasi moja inaua, basi Simba inapaswa kusajili kiwerevu, sio kwa kubomoa timu, bali kuongeza watu wachache na zaidi kuweka mifumo ya kufanya hata hili bao moja iwe gumu kupatikana dhidi yao.

HAT TRICK KAMA ZOTE

Ukitaka kujua Simba ni kali kuliko inavyofikiriwa na kusema mtaani angalia idadi ya hat trick iliyonayo kwa sasa kwenye Ligi Kuu iliyosaliwa na mechi za raundi moja tu kabla ya kufikia tamati.

Katika Hat trick nane zilizopo kwenye ligi, tano zimefungwa na wachezaji wa Simba, John Bocco na Saido Ntibazonkiza kila mmoja akiwa na mbili, huku Jean Baleke akiwa na moja.

Saido juzi usiku alifunga mabao matano wakati Simba ikishinda 6-1 dhidi ya Polisi na kuweka rekodi ya kuhusika na mabao mengi ndani ya msimu huu akifikisha mabao 27, akifunga 15 yakiwamo manne alipokuwa na Geita Gold, huku akiasisti 12, zikiwamo sita alipokuwa na Geita kabla ya kutua Simba.

Nyota hao watatu pekee yao wamefunga jumla ya mabao 28, ikiwa ni karibu ya nusu ya mabao ya timu hiyo yaliyofungwa kwa sasa kwenye Ligi Kuu, Bocco akifunga 9, Saido (11) na Baleke manane.

REKODI ZA ROBERTINHO

Kocha Mbrazil, Roberto Oliveira, alitambulishwa na Simba Januari 3, 2023 na tangu hapo ameiongoza timu hiyo katika mechi 22 za michuano yote, ameshinda 15, vipigo vitano (Raja 3-0, 3-1, Horoya 1-0, Wydad 1-0 na Azam 2-1) na sare mbili (Azam 1-1, Namungo 1-1).

SOMA NA HII  VIJANA WA IBENGE WAINGIA DOSARI...SAFARI YAO YAKWAMA...LIGI YA MABINGWA AFRIKA