Home Habari za michezo MASTAA YANGA MTEGONI….MAMELOD , MAZEMBE, WYDAD NA AL AHLY WAKAA MKAO WA...

MASTAA YANGA MTEGONI….MAMELOD , MAZEMBE, WYDAD NA AL AHLY WAKAA MKAO WA KULA…

Habari za Yanga leo

Mastaa wa Yanga kwa sasa wanajiandaa na shamrashamra za kukabidhiwa taji la Ligi Kuu Bara ilililotwaa mapema msimu huu, lakini wanafahamu kwa sasa deni walilonalo ni kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ambayo lengo kuu la timu yao ni kufika hatua ya makundi.

Hata hivyo wakati wakifikiria hilo wanapaswa kufahamu kuwa kuna vigogo sita tayari vimeshakata tiketi ya kushiriki mashindano hayo vikiongozwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na hivyo kuwatega mastaa hao wa Yanga kujipanga kwelikweli ili kuweka heshima baada ya kazi ya msimu huu.

Yanga iliyofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2 dhidi ya USM Alger ya Algeria, ilichemsha msimu huu kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa kwa kutolewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

Kubeba ubingwa wa Bara, Yanga imejihakikishia kushiriki tena Ligi ya Mabingwa, kama ilivyo kwa Mamelodi ambayo msimu huu imeishia hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitolewa na watetezi, Wydad Casablanca ya Morocco kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yao kumalizika kwa sare ya 3-3.

Timu hiyo ilijihakikishia mapema kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini mwezi uliopita. Miamba hiyo ya Afrika Kusini, itaungana na Orlando Pirates iliyoshika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo, kuiwakilisha nchi hiyo kwenye michuano hiyo kwa msimu ujao, mashindano ambayo timu hizo zote mbili zimewahi kuchukua ubingwa kwa nyakati tofauti.

Wakati Mamelodi Sundowns wakichukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja ambayo ni 2016, Orlando Pirates wenyewe walitwaa taji la mashindano hayo mwaka 1995. Vigogo vingine vinne ambavyo tayari vina tiketi mkononi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni AS Vita na TP Mazembe vya DR Congo, Petro Luanda (Angola) na Coton Sport De Garoua ya Cameroon.

TP Mazembe imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara tano tofauti, AS Vita imechukua mara moja, Petro Luanda wamefika nusu fainali mara mbili wakato Coton Sport De Garoua yenyewe imewahi kutinga fainali mara moja.

Timu hizo sita, Yanga na Simba ambazo zitawakilisha Tanzania zinaungana na nyingine 12 ambazo nazo zimeshakata tiketi kufanya idadi ya timu ambazo zina uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kufikia 20.

Nyingine ni Primiero do Agosto (Angola), Power Dynamos (Zambia), Jwaneng Galaxy (Botswana), Green Mamba (Eswatini), APR (Rwanda), Vipers (Uganda), FC Nouadhibou (Mauritania0, ASKO De Kara (Togo), Bumamuru (Burundi), LISCR (Liberia), Bantu (Lesotho) na African Stars (Namibia).

Wakati baadhi ya wapinzani wa wawakilishi wa tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakianza kufahamika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limezitega Simba, Yanga na Azam FC pamoja na Singida Big Stars zitakazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuzipa miezi miwili tu ya kujiandaa na mashindano hayo, kabla ya kipute rasmi cha msimu ujao kuanza.

Kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya CAF, mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yataanza Agosti 18 na Kombe la Shirikisho Afrika yataanza Agosti.

Ni kalenda ngumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania ikiwa wataanzia katika raundi ya kwanza kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa timu za Simba, Yanga na Geita Gold, kutokana na muda mdogo wa maandalizi ambao zitapata kutokana na kuchelewa kumalizika kwa Ligi Kuu na pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Wawakilishi hao wa Tanzania, watakuwa na siku takribani 68 ambazo wanapaswa kuzitumia kufanya usajili, wachezaji kupumzika na kufanya maandalizi ya msimu mpya kabla ya kuanza kibarua kilicho mbele yao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mapema hivi karibuni, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Wasafi FM wamepanga kuhakikisha wanafanya vyema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Malengo yao ni kufika hatua ya makundi.

‚ÄúTutazidi kufanya kazi kila siku ili kuhakikisha klabu inafikia mafanikio, ili kutimiza mahitaji ya mashabiki na wanachama wa klabu yetu. Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao lengo letu ni hatua ya makundi,” alisema Hersi.

SOMA NA HII  KISA SIMBA....NAMUNGO WATUA DAR KIBABE....'PAPA'AH MOLINGA AONGOZA MSAFARA...PLANI ZAO NIKO HIVI...