Home Habari za michezo HIKI HAPA ‘KITASA CHA KAZI’ WALICHOMALIZANA NACHO SIMBA…JAMAA HAPITIKI KIRAHISI AISEE…

HIKI HAPA ‘KITASA CHA KAZI’ WALICHOMALIZANA NACHO SIMBA…JAMAA HAPITIKI KIRAHISI AISEE…

Tetesi za Usajili Simba

HUKO Msimbazi mambo yamenoga baada ya kumsainisha beki wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Wonlo Coulibaly baada ya kitasa huyo kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hiyo ilikwamia hatua ya nusu fainali ikifungwa na USM Alger ya Algeria.

Hivi karibuni,  uongozi wa Simba walisafiri kwenda Ivory Coast kufanya mazungumzo na staa huyo mwenye umri wa miaka 31 na sasa mambo yamekwenda vizuri hivyo msimu ujao ataonekana na uzi Wekundu wa Msimbazi.

Simba kwa sasa inasaka beki wa kati wa kusaidiana na Henock Inonga baada ya Joash Onyango kuelezwa ameomba kuondoka ili arudi Gor Mahia ya nchini Kenya alikokuwa anacheza kabla ya kusajiliwa Simba misimu miwili iliyopita. Coulibaly pia anamudu kucheza kama beki wa pembeni wa kulia na kushoto sambamba na eneo la kiungo mkabaji, hivyo kunaswa kwake kutaibeba Simba.

Kiongozi mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kuweka jina lake liwekwe hadharani kuwa, klabu hiyo tayari imemalizana na mchezaji huyo na muda wowote atatua jijini Dar es Salaam, ili kukamilisha taratibu nyingine.

“Wafuatiliaji wazuri wa michuano ya CAF wanajua kazi aliyofanya beki huyo ni mpambanaji na ataisaidia sana Simba kwenye michuano mbalimbali, tumeamua kujenga kikosi cha mchezaji anayeingia na kutoka wanafanya kazi yenye kuleta tija na siyo presha.

“Simba tunasajili mastaa wenye viwango vya juu, ambao wataleta matunda yatakayoifanya klabu yetu kufanya vizuri na kuwapa raha mashabiki baada ya kushindwa kuchukua mataji ndani ya misimu miwili tofauti, tunajua wanaumia na hilo ndilo jukumu letu kama viongozi.”

Ukiachana na beki huyo, uongozi wa Simba ulikuwa unafanya mazungumzo na winga wa timu hiyo hiyo, Kramo Aubin, kiongozi huyo kalizungumzia hilo kwa kusema;

“Ndio tumeanza timu yetu ya skauti ipo kazini, msimu ujao Simba hatuna mchezo mchezo, hatutaki maneno mengi bali vitendo.”

Kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alishawapa uongozi wa Simba ni wachezaji wa aina gani anawahitaji kwenye kikosi chake msimu ujao na moja ya mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni alikiri hilo.

“Nahitaji kila nafasi iwe ushindani, anayeingia na kutoka wafanye kazi sawa, tayari viongozi nimewapa ripoti ya nini nakihitaji naamini wanaifanyia kazi kikamilifu.”

SOMA NA HII  SAFARI YA ABDULRAZACK HAMZA KUTOKA AFRIKA KUSINI...HADI SIMBA