WAKATI leo ni siku ya pili tangu kufunguliwa dirisha la usajili kwa msimu ujao, mabosi wa Yanga wamepokea simu nzito kwa kocha wao, Miguel Gamondi akitaka ifanyike akili mpya ya mastaa wapya watakaosajiliwa ikiwa na maana ni kama amefumua usajili mzima uliokuwa umepangwa.
Yanga ilikuwa tayari imeshaanza usajili mdogo mdogo wakianza na kuwatema wachezaji watano wakiwemo kipa Erick Johola, beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ pamoja na mawinga Tuisila Kisinda, Dickson Ambundo na Bernard Morrison ‘BM33’.
Hata hivyo, wakati mastaa hao wakitemwa kocha Gamondi bado mezani kwake ameganda na mafaili ya wachezaji wake waliotumika msimu uliopita na kushtuka kwamba kuna kundi kubwa la wachezaji wenye umri mkubwa ambao Yanga haitaweza kuwategemea katika msimu miwili ijayo.
Kocha huyo raia wa Argentina amewataka mabosi hao kwanza kutochukua wachezaji wenye umri mkubwa akitaka mastaa wapya wawe na umri mdogo au wa katikati ili waweze kuleta nguvu kubwa ndani ya kikosi chake.
“Unajua alipofika hapo kwenye umri akaona jinsi wachezaji wengi walivyo na umri mkubwa ametuambia hataki kuona timu yake inawategemea wachezaji wenye umri mkubwa wengi na badala yake anataka kwenda na wachache pekee ambao ataona wanafaa,” alisema bosi wa juu wa Yanga na kuongeza;
“Kwa maana hiyo katika usajili wetu huu wa sasa tutakuwa na kazi ya kuangalia sana vijana wapya na sio tena wachezaji wenye umri mkubwa. Kuna umri ametupa (Gamondi) tutauzingatia katika watu ambao tutawaleta.”
Bosi huyo wa Yanga alifunguka pia kwa mchezaji kama ni kijana, kocha Gamondi anataka mwenye ubora na kitu cha ziada ili apate nafasi ya kusajiliwa kitu ambacho pia kitazingatiwa.
“Kuna wengine vijana tutaachana nao, sio kwamba kila kijana atabaki. Anataka kuwa na watu ambao wana nguvu na ubora wa kupigania nafasi ya kucheza, na sio tu kwa kuwa kijana asiye na ubora, hilo hataki,” alisema kigogo huyo na kuongeza;
“Hata katika hawa wapya anaowataka anataka kuona mchezaji mwenye kitu cha ziada na tunamshirikisha kila hatua ya mchezaji tunayempata ili tupate baraka zake kabla ya kufanya maamuzi.
Kwa agizo hilo jipya la Gamondi kufumua usajili mzima wa Yanga kwa sasa ni wazi wachezaji wenye umri mkubwa na wale vijana, lakini walioshindwa kuonyeha makubwa chini ya Nasreddine Nabi aliyeondoka wanapaswa kujipanga upya kwani wakati wowote linaweza kuwakuta.
Katika kikosi cha Yanga kilichoanza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wenye umri mdogo walikuwa ni Clement Mzize aliyezaliwa miaka 19 iliyopita akifuatiwa na Dickson Job na Kibwana Shomari waliozaliwa miaka 23 iliyopita kila mmoja.
Wamo pia wachezaji weye umri mkubwa zaidi ambao ni Morrison, Djuma Shaban, Lomalisa Mutambala ambao wote walizaliwa miaka 30 iliyopita, huku baadhi ya majembe mengine yanayoanzia benchi akiwamo Zawadi Mauya umri ukiwa umemtupa mkono kwa sasa.